POLISI mkoani Morogoro inamshikilia dereva wa basi la Kampuni ya Shabiby lenye namba za usajili T 341 EEU, Said Malugula akituhumiwa kusababisha ajali iliyojeruhi abiria 22, baada ya basi hilo kupinduka eneo la Kihonda kwa Chambo mkoani Morogoro.

Kamanda wa Polisi Mkoa Morogor, Alex Mkama amesema leo Mei 25, 2024 kuwa ajali hiyo ilitokea saa 12: 20 asubuhi ya leo, wakati basi hilo likielekea mkoano Dodoma.

Amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi hilo , ambaye alikuwa anapita magari mengine ya mbele yake bila kuchukua tahadhari, ambapo gari hilo liliacha njia na kupinduka na kusababisha abiria kujeruhiwa.

“ Tunamshikilia dereva wa basi hilo na taratibu za kumfikisha mahakani zinaendelea,” amesema Kamanda Mkama na kuongeza kuwa basi hilo lilikukuwa na abiria 57, ambapo waliojeruhiwa ni 22, wanawake 15 na wanaume saba

By Jamhuri