Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Dhamira njema inayoonyeshwa wazi Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni wazi kuwa itafanikisha kiu ya mchakati wa mabadiliko ya sheria ya habari nchini.

Hatua hiyo inatokana na wasaidizi wa Rais Samia kuonyesha kwa vitendo na hatua kwa hatua katika kukutana na wadau wa habari kwenye vikao vya pamoja na kujadili mchakato huo.

Hivi karibuni Rais Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Deogratius Nsokolo, amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa mchakato kuhusu mwenendo wa mabadiliko ya sheria ya habari nchini kumekuwa na mafanikio makubwa.

“Kitendo cha viongozi mbalimbali wakiongozwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye tangu aingie madarakani amekuwa ni rafiki wa waandishi wa habari kutokana na kuonyesha nia ya kufanyiwa kwa marekebisho baadhi ya vifungu vya sheria ya habari vilivyoonekana kuwa ni mwiba katika sekta ya habari.

“Rais Samia tangu alipoungia madarakani, alikuwa karibu na sekta ya habari na kutoa matumaini ya kufanyiwa marejeo kwa sheria hi ya mwaka 2016. Na tayari matokeo yake ni wadau wa habari Serikali kukaa kwa pamoja na kuainisha vipengele gani ambayo wangependa viondolewe,” amesema.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema kuwa
Serikali na wadau wameshamaliza kazi ya kuainisha vipengele hivyo, kinachotarajiwa mapendekezo hayo kupelekwa bungeni.

Amesema, kazi iliyobaki sasa ni upande wa Serikali kukamilisha mchakato na kisha mapendekezo hayo kupelekwa bungeni kwa mujibu wa sheria za nchini.

“Wito wangu, mchakato huo uende kwa kasi ile ile kwa sababu mabadiliko hayo yatawezesha waandishi wa habari kuwa huru zaidi, pia kufanya kazi zao kwa weledi kwa sababu, vile vitu ambavyo tuliviona ni vikwazo, vitakuwa vimeondolewa.

“Mambo hayo yanayokwaza uhuru wa habari yakiondolewa, yatasaidia sana maendeleo ya nchi yetu kwa sababu, habari ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi,” amesema.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema mchakato huu unakwenda vizuri sana kwa kuwa,rais aliyepo madarakani ana dhamira njema na sekta ya habari.

Balile amesema kuwa baada ya wadau wa habari kufanya vikao na serikali, wadau wanasubiri matunda ya vikao hivyo kwa kupelekwa mapendekezo ya wadau wa habari bungeni.

“Katika mchakato huu, tumekuwa tukishiriki kuzungumza na waziri husika ili tukubaliane katika sehemu mbalimbali ya vifungu vya sheria ya habari,” amesema Balile na kuongeza:

“Tulifanya mkutano wa mwisho Novemba ambao tulisema, sasa huu uwe mkutano wa mwisho ili sheria ya huduma za habari ipelekwe bungeni.” amesema.

By Jamhuri