📌Asisitiza kutoa elimu ya afya kwa jamii

📌Aupongeza Mfumo wa M-mama uliobuniwa na Watanzania

📌Jumla ya vituo 2,799 vimejengwa na vingine kufanyiwa ukarabati kuanzia mwaka 2017 hadi 2024

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza kuweka Mpango Mkakati wa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu uliofanywa na Serikali katika vituo ngazi ya Afya ya Msingi inatunzwa.

Dkt. Biteko ametoa agizo hilo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi nchini Tanzania tarehe 25 Machi, 2024 jijini Dodoma ambapo amesema kuwa miundombinu bora inawezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa urahisi zaidi.

Dkt. Biteko amewataka kujadili kwa kina namna bora ya kubuni mbinu zitakazowezesha kuongeza kasi ya kuajiri wataalam wa kada mbalimbali za afya hasa zile zenye upungufu mkubwa.

Pia, ameagiza kuainisha mikakati ya utoaji wa elimu ya afya kwa jamii ili wananchi waelimishwe kuhusu njia za kuzuia magonjwa, umuhimu wa chanjo na njia zingine za kudumisha afya bora.

Dkt. Biteko amesisitiza kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya huduma za afya ya msingi ili kuweza kufahamu maendeleo ya utekelezaji wa Afua mbalimbali za afya na kutambua maeneo ya kuboresha.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameupongeza Mfumo wa M-mama uliobuniwa na Watanzania .

“Kwa furaha kubwa nasimama mbele yenu siku ya leo nikifurahia kuona maono ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha mfumo wa usafiri wa dharura kwa wajawazito, waliojifungua na watoto,” amesema Dkt. Biteko.

Amesema, M-mama inaratibiwa katika hospitali za mikoa kupitia waratibu waliopewa mafunzo kwa kupiga namba 115 ambapo waratibu wa m-mama katika kila mkoa wanaweza kutoa huduma hizo.

“Napenda kuwashukuru wadau wetu wa maendeleo Vodacom Tanzania, Vodafone Foundation, USAID, Benki ya Dunia na wadau watekelezaji wa mfumo wa ‘Touch Health’ na ‘Pathfinder International’ kwa mchango wao katika kushirikiana na Serikali kuleta huduma hii inayohitajika kwa wote,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine amesema, serikali imeweza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha miundombinu ya utoaji huduma ambapo kuanzia mwaka 2017 hadi Januari 2024, jumla ya vituo 2,799 vimejengwa na vingine kufanyiwa ukarabati, zikiwemo Zahanati 1,762, Vituo vya Afya 910, na Hospitali za Halmashauri 127.

Pia, majengo 83 ya kutolea huduma za dharura na majengo 28 kwa ajili ya wagonjwa mahututi na nyumba za watumishi 150 zimejengwa. Gharama ya ujenzi na ukarabati huo imefikia shilingi bilioni 937.2 ikiwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa huduma za afya zinapatikana kwa kila mtu katika jamii yetu.

Awali, Dkt. Biteko amehimiza kuwezesha watu, familia na jamii kwa ujumla kuzingatia afya bora na kuhamasisha utekelezaji wa sera na miongozo inayolenga kulinda afya ya jamii.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Godwin Mollel amesema kuwa wataalam wa sekta hiyo wamejitoa kuhakikisha wanatoa huduma bora ya afya nchini hususan ya msingi na kuwataka washikamane kujenga sekta hiyo muhimu.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI anaeshughulikia Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Mhe. Festo Dugange amemshukuru Rais Samia kwa kufanya mageuzi katika Sekta ya Afya. Amesema mkutano huo unawezesha kujadiliana masuala mbalimbali na kubadilishana uzoefu na namna ya kuboresha afya ya msingi kwa watu wote.

Please follow and like us:
Pin Share