📌 Asema amekuwa mfano Kitaifa na Kimataifa

📌 Apongeza Baraza la Vyama vya Siasa kukusanya maoni Miswada ya Sheria za Uchaguzi

📌 Awasisitiza kwenda bungeni kutoa maoni ya miswada

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kustawisha ustawi wa kidemokrasia nchini, sambamba na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi na kijamii ili kuwaletea Maendeleo watanzania.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 4 Januari, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifunga Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini ulioshirikisha wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa ili kujadili miswada ya Sheria za Uchaguzi na Muswada wa Sheria za Vyama vya Siasa.Mkutano umeandalilwa na Baraza la Vyama vya Siasa.

Miswada iliyokuwa ikijadiliwa ni muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa mwaka 2023.

“ Rais wetu amekuwa ni mfano wa kuigwa, kitaifa na kimataifa kwa kuhakikisha kuwa demokrasia yetu inazidi kustawi na kuifanya Serikali kuendeshwa kwa misingi ya haki, utawala bora na kwa mujibu wa sheria tulizojiwekea na bila kusahau kuzingatia maoni ya watu ambao ni muhimu katika kuboresha utendaji wetu.” Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko amepongeza Baraza la Vyama vya Siasa kwa kuandaa mkutano huo ambao ni muhimu kwa maslahi ya Taifa na kueleza kuwa Baraza hilo kwa kwa mujibu sheria linajukumu pia la kuishauri Serikali kuhusu utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa na masuala mengine yanayohusu vyama vya siasa na demokrasia.

Amesema kuwa, mkutano huo umekuwa wenye tija kwani washiriki wameweza kutoa maoni yao kwa kuzingatia maslahi ya nchi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaasa wajumbe wa Mkutano huo kuitikia wito wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson wa kwenda bungeni kuanzia tarehe 6 hadi 10 Januari ili kutoa maoni kuhusu miswada ya sheria za uchaguzi na mswada wa sheria ya vyama vya siasa.

Amewashukuru wajumbe hao kwa kutoa maoni ambayo ni bora na kwa kujadiliana kwa uungwana kuhusu miswada hiyo, kwani hakuna chama kilichoonesha kuwa kina umiliki wa kutoa mawazo bali wote walisikilizana huku akieleza kuwa yale waliyojadiliana itakuwa ni muendelezo wa kujenga maridhiano ya kitaifa.

Kuhusu sheria zilizopo nchini amesema kuwa, endapo kuna sheria inaonekana ina changamoto baada ya kuitumia kwa muda mrefu, “wito wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sote kukaa na kuridhiana kama Taifa wapi tuboreshe na Bunge ni Taasisi mahiri yenye uongozi mahiri ambao watapokea maoni yetu na kuyafanyia kazi na mahali ambapo Serikali itapaswa kupeleka muswada sheria ya marekebisho bungeni itafanya hivyo.”

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama, amesema kuwa, lengo la mkutano huo lilikuwa ni kukutanisha wadau wengi wanaohusika na masuala ya demokrasia ya mfumo wa vyama vingi nchini ili kutoa maoni yatayoboresha miswada kwa kupitia utaratibu utakaozingatia sheria na kanuni za upitishwaji wa miswada katika Bunge la Tanzania.

Amesema kuwa, mkutano huo umekuwa na mafanikio makubwa na wadau wametoa maoni yao kwa amani na ushirikiano mkubwa, hivyo amepongeza Baraza la Vyama vya Siasa, kwa kuandaa mkutano huo na kusema kuwa, Serikali itaendelea kuliunga mkono Baraza hilo katika utekelezaji wa mipango yake.

Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Fransis Mutungi amesema kuwa, zao la mkutano huo ni muongozo uliotolewa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati alipopokea taarifa ya kikosi kazi alichokiunda cha kuratibu maoni ya wadau wa Demokrasia ya vyama vingi vya siasa ambapo moja ya masuala aliyoelekeza ni kufanyika kwa maboresho ya sheria za uchaguzi na sheria za vyama vya siasa.

Amemshukuru Rais kwa jitihada zake katika kukuza na kuendeleza demokrasia nchini kwani kukutana kwa Baraza hilo kunatokana jitihada hizo za uwepo wa demokrasia nchini.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria Mkutano huo ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hamza Hassan Duma, Mkuu wa Mkoa wa Da es Salaam, Albert Chalamila na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma.