Jana ilikuwa siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwagalla, lakini kiongozi huyo aliisherehekea akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akipatiwa matibabu.

Dk Kigwangalla alisherehekea siku yake akitibiwa baada ya kupata ajali mwishoni mwa wiki iliyopita, eneo la Magugu wilayani Babati mkoani Manyara.

Katika ajali hiyo ofisa habari wa wizara hiyo, Hamza Temba alipoteza maisha huku waziri huyo akijeruhiwa pamoja na wasaidizi wake wawili kati ya wanne. Hata hivyo, licha ya kutimiza umri wa miaka 43, waziri huyo hakukosa cha kusema; akisisitiza ajali aliyoipata imempa funzo kubwa na mtihani mzito.

“Nimefikisha miaka 43 ya kuzaliwa kwangu leo (jana). Alhamdulilah. Asante Allah kwa kunifikisha leo hii. Mimi ni shuhuda wa nguvu zako na upendo wako…Umenipa mtihani na funzo kubwa kwenye maisha yangu, naomba uendelee kunipa ulinzi wako,” aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Kadhalika katika ujumbe wake huo, Dk Kigwangalla amemuomba Mungu amjalie maisha mema na marefu yenye faida kwake na viumbe wa Mola.

Pia amewashukuru na kuwaombea afya njema, furaha na mafanikio familia yake, ndugu, jamaa na viongozi wakuu pamoja na wananchi waliomuombea dua.

“Kwa wapiga kura wenzangu wa Nzega, poleni nilikuwa nakuja ziara yetu ya jimbo ndio nikapata ajali hii. Mzidi kuniombea dua ili nipone haraka niendelee kuwatumikia. Kwa sasa naendelea vizuri alhamdulilah japo nina maumivu makali sana,” ameandika.

Kadhalika, aliandika katika ukurasa wake wa Twitter akimlilia Temba, akisema: “Nimeangalia simu yangu na kukutana na picha za ziara yetu ya ‘PoriKwaPori’ na ndiyo nauona ukweli kuwa mdogo wangu, bwashee wangu, huyu kijana mdogo mchapakazi na aliyekuwa na matumaini makubwa, sitamuona tena na kumtania.”

Kisha akaongeza, “niseme nini tena? Qaalu inna lillah wainna ilayhir rajiuun,”

Tangu alazwe hospitalini hapo, jana kwa mara ya kwanza pia Dk Kigangwalla alituma ujumbe katika ukurasa wake wa Facebook akimshukuru Mungu kwa jinsi alivyomnusuru katika ajali hiyo.

Dk Kigwangalla alipata ajali Julai 4 wakati gari alilokuwa akisafiria lilipoanguka likikwepa twiga aliyekatiza barabarani.

Baada ya ajali hiyo ambapo alipata majeraha mbalimbali mwilini, alipelekwa Hospitali ya Selian mjini Arusha na baadaye kusafirishwa kwa helikopta hadi Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu alimtembelea jana na kumtakia uponyaji wa haraka.

“Ni kwa bahati mbaya unasherehekea siku yako ya kuzaliwa ukiwa hapa lakini kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Samia.

Wakati huohuo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu ya Muhimbili (Moi), Dk Respicius Boniface alisema kuwa waziri huyo atahamishiwa kwenye taasisi hiyo.

Dk Boniface alisema jana kuwa, lengo la kumhamishia kwenye taasisi hiyo ni kuendelea na matibabu ya viungo vilivyovunjika.

“Nimemtembelea Waziri Kigangwala na kusema kweli hali ya afya yake inaendelea vizuri, ameumia kifuani, mikono na miguu na anaendelea kupata matibabu Muhimbili na atakapoimarika zaidi atahamishiwa katika taasisi yetu kuendelea na matibabu mengine,” alisema.

Dk Boniface alikuwa akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu programu inayoendeshwa na taasisi hiyo ya uchunguzi wa umri kwa wachezaji wa timu ya Taifa ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17 ambao watashiriki michuano ya Cecafa itakayoanza jijini hapa mwishoni mwa wiki.

Please follow and like us:
Pin Share