Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Mwenyekiti wa Waganga wafawidhi wa hospital za rufaa Tanzania bara Dk. Stanslaus Ibenzi ameeleza kuwa kwa sasa Hospitali hiyo haielemewi na wagonjwa kutokana na Serikali kuwekeza zaidi kwenye maboresho ya huduma za afya.

Dk.Ibenzi ameeleza hayo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa utendaji kazi wa Hospitali hiyo na kueleza kuwa tayari Hospitali hiyo imeshahamia kwenye kitita kipya cha mafao ya NHIF cha mwaka 2023 kilichopendekezwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa wote(NHIF).

Aidha amesema huduma nyingine zinaendelea kutolewa kama kawaida huku wakiwa wamejipanga vyema kutoa huduma bora kwa wananchi na kwamba wataendelea kufuatia utendaji wa kitita hicho ili kubaini changamoto zitakazojitokeza na kuziwasilisha katika Mamlaka husika ili kuendelea kutoa huduma zilizobora kwa wananchi.

“Tupo katika wendelezo wa uboreshaji wa huduma za afya,tayari serikali imeboresha kitita cha kutolea huduma za NHIF ambapo kuna dawa nyingi ambazo zimeongezwa, ” Amesema

Pamoja na mambo mengine amesema Hospitali hiyo imeboresha huduma mbalimbali ikiwemo madaktari bingwa kufanya kazi ndani ya saa 24 pamoja na kuongeza muda wa wagonjwa wanaokwenda kwa ajili ya kliniki ya magonjwa mbalimbali kutoka muda wa awali ambao ulikuwa mwisho saa tisa alasiri.

Amefafanua kuwa,”Awali wagonjwa wanaokuja kwajili ya kuwaona madaktari kwa kliniki mbalimbali walikuwa wanawaona mwisho saa tisa alasiri lakini sasa hivi daktari anawaona wagonjwa hadi watakapoisha,pia tumeongeza muda wa ndugu kuwaona wagonjwa wao”amesema Dkt.Ibenzi.

Pia alizingumzia mpango wa Hospitali hiyo kuhusu wanachama wanaotumia bima za NHIF,kutokana na baadhi ya Hospitali za binafsi nchini kusitisha huduma kwa wanachama hao kuanzia leo Machi 1,2024,ameeleza kuwa
kuwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma kutakuwa na Mpango wa dharura wa utoaji huduma .

“Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma umekuja na Mpango wa dharura wa kutoa huduma kwa wanachama hao ili waweze kuwa na mwendelezo wa huduma hizo kwani sisi kila siku tumejiandaa vizuri kutoa huduma kwa ubora,”ameeleza

Amesema kuwa hospitali hiyo ina wagonjwa wengi ikiwemo waliopangwa kufanyiwa upasuaji na wao kama hospitali wanavyumba vya kutosha vya upasuaji,wanazo mashine za Kutosha na wameongeza zamu za kutoa huduma kwa wateja.

Amesema,Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma kama hospitali nyingine za rufaa wamejipanga tumefanya ugatuzi tiba utakaokidhi huduma zote hali itakayosaidia mgonjwa anapoingia hospitalini hapo na kuondoka asichukue zaidi ya saa moja.

Pamoja na Mambo mengine Hospitali hiyo inatoa huduma za mgonjwa ya nje na dharula, huduma za dawa na vitaa tiba, uchunguzi wa mgonjwa, huduma tiba na afya ya motto, upasuaji, masukio, pua na Koo na nyinginezo.

By Jamhuri