Angali ana siku chache ofisini, tangu Dk. John Magufuli aanze kazi ya urais, wazalendo kadhaa wamejitokeza kumsaidia kutaja baadhi ya “biashara haramu” zinazokwenda sambamba na taarifa za ukwepwaji kodi hivyo kuliingizia taifa hasara ya mamilioni.

Miongoni mwa biashara hiyo ni chuma chakavu ambako baadhi ya wafanyabiashara, wanaifanya bila leseni hivyo kupata fursa ya kukwepa kodi sambamba na kuhujumu miundombinu ya reli, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Tanroad na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka nchini (Dawasco).

Taarifa za uchunguzi zinasema maeneo mengine yanayohujumiwa ni pamoja ubinafsishwaji kama vile viwanda vya nguo, misalaba makaburini, kadhalika meli iliyokamatwa kwa madai ya kuiba samaki nchini.

Mtanzania aliyejitokeza mapema kumtwisha Dk. Magufuli ‘bomu’ la biashara hiyo na kwamba kuna hujuma kubwa katika uchumi wa taifa ni Henry Batamuzi – Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kenwood ya Mlandizi, Kibaha mkoani Pwani.

Katika mahojiano na mwandishi wa habari wa JAMHURI yaliyofanyika wiki iliyopita, Batamuzi anasema: “Dk. Magufuli anaweza kufanya kazi zake kwa urahisi sana na akatimiza ahadi zake kwa Tanzania. Hasa hili la elimu bure na ataweza kufuta mpaka michango. Ni kusimamia tu. Fedha ziko katika biashara ya chuma chakavu.”

Anasema: “Hapa kuna utajiri mkubwa na kinachosikitisha ni kwamba vyombo vya usalama kama polisi wanamulika na kuweka nguvu kudhibiti biashara ya dawa za kulevya, lakini wanasahau kuna uhujumu wa uchumi mkubwa kwenye biashara ya chuma chakavu.”

Kwa mujibu wa Batamuzi amepita ofisi kadhaa nyeti za Serikali kutoa taarifa kwa mdomo kadhalika kwa maandishi kwa mamlaka mbalimbali, lakini anaona suala hilo linachukuliwa kwa wepesi ilihali linaigharimu nchi huku yeye akivuna chuki kubwa kutoka kwa wamiliki wa viwanda vya kuzalisha nondo, wanaonunua chuma na kusafirisha kwenda ng’ambo na madalali wanaofanya biashara hiyo bila leseni.

“Wadau hao niliowataja wanapata faida ya mabilioni ya shilingi bila kulipa kodi yoyote serikalini huku kukiwa na maofisa wa Serikali na asasi zake wanaoshiriki kufanikisha hujuma hii kwa shilingi ya Tanzania, miundombinu na kupoteza mabilioni kama si matrilioni,” anasema.

Anasema na JAMHURI limethibitisha kwamba taarifa hizi amezisambaza katika vyombo kadhaa vya Serikali huku mzalendo huyo, akisema: “Huu ni mtandao wa uhalifu ulioandaliwa na wahusika niliowataja. Unalindwa kwa gharama yoyote. Zinazimwa zisifanyiwe kazi serikalini na hata kwenye vyombo vya habari.”

Batamuzi ambaye Kampuni yake ina baraka za Serikali kufanya biashara hiyo, alikwenda Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambako alipeleka ombi la kununua chuma chakavu, lakini, akajibiwa: “Utajulishwa.”

Chini ya mwamvuli wa Kampuni yake, aliandika barua hiyo yenye Kumb. KWDTL/SCRAPS/100/12 ya Februari 15, 2012 iikiwa na viambatanisho vya uhalali wa kufanya biashara pamoja na vibali vya Baraza la Hifadhi ya Taifa na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Majibu ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo yalitolewa na H.T Kinanga Februari 27, 2012 yalisema: “Aidha utaratibu huo utakapokamilika utajulishwa ili uweze kushiriki katika zoezi la wazi la kununua vifaa hivyo.”

Majibu hayo yako kwenye barua yenye Kumb. Na. EA.251/450/01/134 ambako pamoja na maelezo hayo, pia ilisema wizara ipo kwenye utaratibu wa kufuta mitambo yake chakavu kwa mujibu wa sheria.

Lakini, Batamuzi anasema: “Inasikitisha na inauma sana kwa sababu nilikuta mitambo yote iliyokuwa idara ya upimaji na ramani imeuzwa eti kwa wafanyakazi kama motisha! Je, walionunua mitambo hiyo chakavu waliinunua wakaifanyia nini?

“Je, ukifanya ukaguzi utaikuta bado ipo nchini? Huu ni uthibitisho kwamba raia wa mataifa mbalimbali wanaishi nchini Tanzania na kufanya biashara mojawapo ya kuhamisha fedha zetu ni kununua chuma chakavu na kusafirisha katika nchi zao za asili na hii inatokana na ububu uliosababishwa na sheria mama ya fedha Na. 257 ya mwaka 2010.”

Kwa msingi huo huo, Batamuzi anaibuka akisema: “Uchunguzi ni lazima kwa hujuma hii kwa uchumi wa taifa na kama utapanua wigo wa uchunguzi wa makampuni binafsi na taasisi za serikali kama reli, Tanesco, Kampuni ya TTCL na Dawasco.”

Anasema kwamba vyuma chakavu vinavyozalishwa nchini kwa sasa vinauzwa kwenye viwanda vinavyozalisha nondo wakiwatumia madalali wakati chuma aina ya cast, non ferrous vinanunuliwa na Wahindi, Wapakistani, Wachina, Warusi na Walebanon wakiwa hawana uhalali wa kufanya biashara hiyo na wanasafirisha kwenda makwao.

“Wanafanya biashara yenye athari kwa shilingi ya Tanzania, miondombunu ya reli, tanesco na TTCL na mkongo wa taifa. Lakini kibaya zaidi inakuza deni la taifa.,” anafafanua Batamuzi kwenye mahojiano hayo.

“Ili kudhibiti hujuma hii, namshauri Dk. Magufuli pamoja na timu nzima atakayounda hasa Waziri wa Fedha na wale wa Viwanda na Biashara pamoja na Uwekezaji, wachukue hatua za haraka…

“…kwamba wenye viwanda vya kuzalisha nondo wanunue chuma chakavu (malighafi) kwa wenye leseni na malipo yawe kwa hundi ili kuweka kumbukumbu na kukomesha ukwepaji kodi kubwa. Hapo ndipo itakapoonekana dhana ya hapa Kazi tu.

…Wanaosafirisha chuma chakavu, nje ya nchi wawe na leseni za kuuza chuma nje (exporters). Nasema hayo kwa sababu ni wazi kuwa wafanyabiashara hao wa nje hawana leseni wala vibali vya NEMC vinavyowaruhusu kununua chakavu nchini,” anasisitiza.

Batamuzi anakwenda mbali akidai duniani kote, Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zisizosimamia sheria zilizotungwa na bunge na kuendesha nchi kana kwamba hakuna katiba na utaratibu, “Magufuli aondoe dhana hii,” anasema.

Anasema raia hao wa nje hususani wa kutoka China, India, Pakistan, Kenya, Burundi na Somalia wamenunua ardhi na kujenga viwanda vikubwa, vya kati na vidogo bila kupitia kituo cha uwekezaji (TIC), ingawa wanaitwa wawekezaji kwa mbinu ya kukwepa kodi.

2475 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!