Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa washiriki wa Mkutano wa 21 wa Taasisi za Fedha kutafakari kwa kina changamoto ya uhaba wa fedha za kigeni na hatua gani za muda mfupi na wa kati zinazopaswa kuchukuliwa zaidi ya hatua za urekebu zinazochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 21 wa Taasisi za Fedha unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC). Amesema ni muhimu kwa Mkutano huo kujadili nafasi ya kutumia viwango nyumbufu vya ubadilishanaji fedha (exchange rate flexibility) katika kudhibiti uhaba huo wa fedha za kigeni.

Aidha Makamu wa Rais amewataka viongozi na wataalam katika sekta ya fedha nchini kuhakikisha uwezo wa taasisi zao na sekta nzima unaimarika zaidi ili kuhimili misukosuko inapotokea.

Amewasihi kuangalia namna ya kuimarisha zaidi Idara na vitengo vya utafiti na masoko ya kifedha nchini. Amesema Menejimenti ya vihatarishi, usimamizi makini na ufuatiliaji wa mwenendo wa benki moja moja na sekta nzima ni jambo la muhimu sana katika kujenga sekta ya fedha iliyo imara na yenye uwezo wa kuhimili misukosuko.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Mkutano huo unapaswa kuangazia njia za kudhibiti mikopo chechefu, kupunguza gharama za mikopo na kupanua wigo wa mikopo nafuu hasa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, uchimbaji wa madini na viwanda vidogo. Pia amesema sekta ya fedha inao wajibu wa kushiriki katika jitihada za kuhifadhi mazingira na kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwani huathiri uzalishaji na mapato hususan katika sekta ya kilimo, utalii, ufugaji na hata uzalishaji katika viwanda vinavyotegemea malighafi zinazotokana na kilimo, misitu na maliasili.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa taasisi zote za fedha kuimarisha jitihada za kudhibiti madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na ukuaji wa kasi wa teknolojia ikiwa ni pamoja na changamoto za utunzaji na usiri wa taarifa, usalama wa mtandao wa kibenki, usambazaji wa taarifa potofu mitandaoni, udhibiti wa fedha haramu pamoja na kuwalinda watumiaji kwa kushirikiana kwa karibu na wadau wote.