Na Allan Vicent, JamhuriMedia, Tabora

Mfanyabiashara maafuru Wilayani Urambo Mkoani Tabora Ramadhani Ntunzwe (53) amejiua kwa  kujipiga risasi kichwani akiwa nyumbani kwake .

Kamanda wa Polisi Mkoani hapa SACP Richard Abwao amethibitisha kutokea tukio hilo Machi 6 mwaka huu majira ya saa 2 asubuhi katika Mtaa wa Urambo Kati, Tarafa ya Urambo Wilayani hapa.

Alifafanua kuwa mfanyabiashara huyo alijipiga risasi moja kichwani akitumia bastola aina ya Pietro Beretta Chinesse yenye namba za usajili h57086ycat 5802.

Kamanda aliongeza kuwa bastola hiyo alikuwa anaimiliki kihalali ila Jeshi la Polisi linaendelea na uchuguzi ili kubaini chanzo cha kujipiga risasi, watatoa taarifa baada ya uchunguza kukamilika.

Awali Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Sudi Sadiki alieleza kuwa alipigiwa simu na ndugu wa marehemu baada ya kukuta marehemu amejipiga risasi nyumbani kwake ndipo alipotoa taarifa kwa polisi na askari wakafika na kuchukua mwili huo.

Majirani wa karibu wa marehemu Joseph  Jilya na Seleman Kahwa walisema kuwa marehemu alikuwa mkombozi kwao kwa kuwa alikuwa anawauzia bidhaa kwa bei ya chini tofauti na maduka mengine na alikuwa akitoa msaada kwa makundi mbalimbali  ya watu wasiojiweza pamoja na kuwafuturisha waumini katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kamanda Abwao aliwataka wale wote wanaomiliki silaha kuzitumia kwa malengo yalikusudiwa ya kujilinda na sio kujitoa roho, haya sio matumizi sahihi ya silaha.