Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango anatarajia kuongoza shughuli ya kuaga mwili wa Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, hayati Ali Hassan Mwinyi katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam leo.

Akitoa ratiba ya mazishi ya kiongozi huyo, Msemaji wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema mazishi hayo yatafuata mila na desturi za kizanzibari, pia taratibu za mazishi zitaendeshwa kwa dini ya Kiislamu.

Matinyi amesema pale ambapo kuna taratibu za kiserikali Jeshi la Wananchi Tanzania ndilo litabeba jukumu hilo.

“Jeneza litabebwa kwenye gari ya kubebea mizinga na litabebwa na makamanda wa jeshi wenye cheo cha kanali, wakishindikizwa na makamanda wenye cheo cha brigedia jenerali au jenerali wa nyota moja,”amesema Matinyi.