Na Allan Vicent, JamhuriMedia, Shinyanga

Kasi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) mkoani Shinyanga imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kupitia mradi wa Afya Hatua wa tohara kinga ya hiari kwa wanaume kwa kushirikiana na AFYA PLUS.

Hayo yamebainishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt Yudas Ndugile alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari hivi karibuni wakati wa ziara ya Maafisa wa Shirika la THPS Mkoani hapa.

Amesema kuwa mradi huo unaotekelezwa na serikali kwa ushirikiano na THPS na Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (The US Centre for Disease Control- CDC) kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) umeleta neema kubwa kwa wakazi wa Mkoa huo.

Dkt Ndugile alibainisha kuwa kati ya Januari 2022 hadi Desemba 2023, mradi huo uliwafikia wanaume 73,927 wenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea kutolewa katika kliniki 35 zinazotoa huduma za tohara na huduma mkoba zilizofanyika katika vituo 145 vya kutolea huduma za afya Mkoani hapa.

Alifafanua kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka wa 3 wa mradi huu 2023/2024 jumla ya wanaume 26, 752 wenye umri wa miaka 15 na zaidi wamefikiwa, sawa na asilimia 29 ya lengo la kufikia wanaume 91,022 katika mwaka huo wa fedha.

‘Katika robo ya kwanza tu tumefanya vizuri sana na hii ni kutokana na  ushirikishwaji na ushirikiano mkubwa tunaopata katika ngazi ya Mkoa, Halmashauri na ngazi za jamii,’ alisema.

Aliongeza kuwa mwitikio wa wanaume kupata huduma ya tohara ni mkubwa sana, ndiyo maana wamefikia malengo hayo mapema, hivyo akatoa wito kwa wanaume na watu wazima wote kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo katika vituo vilivyoainishwa.

Dkt Ndungile alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wadau na mashirika mbalimbali kutoa huduma za afya katika Mkoa huo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini Mkoani hapa Dkt. Peter Mlacha alikiri kuwa Tohara Kinga imesaidia sana kupunguza maambukizi ya VVU miongoni mwa jamii na kuondokana na imani potovu kuhusu tohara.

Mratibu wa Huduma za Tohara kutoka Shirika hilo Dkt. Challo Charido alisema kuwa tohara kinga kwa wanaume inapunguza maambukizi ya VVU kwa asilimia 60 na kuimarisha usafi, kinga ya magonjwa ya zinaa na saratani ya uume na mlango wa shingo ya uzazi kwa wanawake.

Alieleza kuwa mradi wa AFYA Plus kwa kushirikiana na THPS na Timu ya Usimamizi wa Afya ya Mkoa/Halmashauri inaunga mkono utoaji wa huduma za tohara kinga kwa wanaume.

Meneja Mradi wa Afya Hatua wa THPS Mkoani hapa Dkt. Amos Scott alisema kuwa huduma ya tohara kinga ya hiari kwa wanaume imekuwa msaada mkubwa sana katika kudhibiti maambukizi ya VVU katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga.

Amebainisha kuwa mradi huo utatoa huduma jumuishi katika vituo vya afya vilivyoko katika Mikoa ya Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga na kwa jamii katika Mikoa ya Kigoma, Pwani na Tanga kuanzia mwezi Oktoba, 2021 hadi Septemba 2026.

By Jamhuri