Zanzibar

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza haja kwa watendaji serikalini kubadilika na kutofanya kazi kwa mazoea ili mipango iliyopangwa na serikali itekelezeke. 

Rais Dk. Mwinyi amesema hayo baada ya kusikiliza mada zilizowasilishwa na makatibu wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) wakati wa mafunzo ya upangaji wa vipaumbele.

Dk. Mwinyi amesema kazi iliyobaki ni utekelezaji na lengo ni kuimarisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

“Sijaridhika na utendaji serikalini. Sijasema hivi kwa kumnyooshea kidole mtu bali ni kutokana na hali halisi ilivyo. Watendaji si wepesi kufanya mipango itekelezeke,” amesema akirejea kauli aliyoitoa siku ya ufunguzi.

Amesisitiza mabadiliko na kutaka kila mmoja kujiona ana wajibu katika ofisi yake kutekeleza mipango iliyopangwa kwa kuwa haitakuwa vema kiongozi kumaliza kipindi chake bila kuonyesha mradi hata mmoja alioutekeleza.

“Mimi sipo tayari kusikia wawekezaji kwetu kwa ajili ya kuwekeza wakizungushwa. Uwekezaji unataka fedha, hivyo si jambo la busara wakazungushwa. Wapokeeni na kuwakaribisha wafanye kazi,” amesema na kuongeza:

“Bado kuna hali ya kutojali na hapo ndipo niliposema kwamba siridhiki na utendaji wa serikali. Mliopo hapa ndio wakuu wa taasisi zetu. Inawezekanaje upo katika kipindi chako cha uongozi kwa miaka mitano hata mtu mmoja hajakemewa?

“Ina maana hakuna anayefanya kosa! Hayo ndiyo yanayotufanya tushindwe kufanikiwa, ningependa kusikia kila mtu anachukua hatua ili kufanya ofisi zetu zifanye kazi vizuri zaidi.”

Rais Mwinyi amesema kuwa anaamini semina hiyo itawasaidia watendaji kubadilika kwani wameshajua mipango na majukumu ya serikali, lililobaki ni kwenda kupanga jinsi ya kuwezesha.

Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said, amempongeza Dk. Mwinyi kwa kuhudhuria katika uwasilishwaji huo wa mada mbalimbali zilizotolewa na makatibu wakuu.

Amesema mafunzo hayo yamewapa mwanga mkubwa wa kutekeleza mipango na upangaji wa vipaumbele vyake sambamba na kuyafanyia kazi maoni yake aliyoyatoa. 

Please follow and like us:
Pin Share