Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alipoutangazia umma kufunguliwa kwa Daraja la Tanzanite, nikarejea kwenye kisa kilichotokea siku ya uzinduzi wa ujenzi wake.

Siku ya uwekaji wa jiwe la msingi mwaka 2018, Rais John Magufuli, na Spika Job Ndugai, walitaniana. Wasukuma na Wagogo ni watani. Rais Magufuli akasema kukamilika kwa daraja hilo kungewafanya Wagogo wafike ‘kulishangaa’ maana ni zuri.

Japo ulikuwa utani, ndani yake kulikuwa na ujumbe muhimu. Ulihusu matumizi ya vitu kama hayo madaraja ya kisasa kwa ajili ya utalii wa ndani.

Kwenye makala niliyoiandika mwaka huo, nilisema utani huo ulinikumbusha tukio lililoniumiza moyo siku chache kabla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa daraja hilo.

Siku moja nikiwa na mwanangu, tulipanda pantoni tukaenda Kigamboni.

Wakati wa kurejea tukavutiwa na mandhari ya Jiji la Dar es Salaam. Tukaona majengo marefu na mazuri ambayo yamechangia kubadili mandhari ya jiji hilo. Nikamwita mwanangu ili apate picha zenye mwonekano wa nyuma wa hayo majengo.

Nikaanza kuchukua picha kwa mbwembwe. Ghafla, akanifuata askari. Akanizuia nisichukue picha. Nikamhoji sababu za kunizuia nisichukue picha. Akanionyesha ilani ndani ya jengo la abiria inayozuia uchukuaji picha! 

Kuona hivyo nikawa sina nguvu tena. Nikakubali kwa shingo upande kuacha kuchukua picha. Mwanangu alinung’unika mno.

Hali hii inawatokea wenyeji na wageni wengi katika miji na majiji yetu nchini. Mathalani, hakuna ruhusa ya kupiga picha katika Daraja la Nyerere jijini Dar es Salaam ambalo ni la kisasa na lenye mvuto wa pekee.

Kwenye daraja ninaweza kuelewa sababu za zuio hilo, japo kimsingi hazina mashiko katika ulimwengu wa leo. Napata shida kila nikiwaza sababu za kuwapo zuio pale Kigamboni (Feri) kwa abiria watalii wa ndani kupiga picha. Sijaelewa kabisa. Hatudai kupiga picha ofisi au kambi za vyombo vya ulinzi na usalama, hapana!

Mwaka 2004 nilikuwa sehemu ya ujumbe wa Tanzania uliozuru Misri. Tukiwa Cairo, wenyeji wetu walitupeleka 6th October Bridge kutalii. Hili ni daraja refu na zuri kweli kweli. Ni kivutio kikubwa mno cha utalii. Wageni na wenyeji hupiga picha muda wote wakifurahia kazi ya wanadamu.

Sisi hapa tunazuia watu kupiga picha hata maghorofa! Tunazuia watu kupiga picha Daraja la Nyerere. Tunatoa sababu za usalama. Sidhani kama kweli ni usalama tu. Yawezekana ni udhaifu wetu wa kuelewa raha na fahari ya kutumia miundombinu hii katika kukuza utalii wa ndani. 

Kama kuna tishio la usalama ni wajibu wa mamlaka kuweka taratibu za kiusalama, lakini si kuzuia wasio wahalifu kufaidi raha zilizoletwa na serikali yao. Kuzuia upigaji picha ni sawa na kusalimu amri kwa wahalifu. Kinachotakiwa ni kuweka taratibu za usalama, basi.

Kwa teknolojia ya leo madaraja yote haya yanaonekana vizuri kwenye google kutoka popote duniani. Kama ni kudhani kuwa mtu akisimama pale juu anaweza kutega bomu, basi ufanyike utaratibu wa utambuzi wa kisasa kuwabaini wenye nia mbaya.

Daraja la Tanzanite limekamilika. Kuna ujenzi wa Daraja la Busisi – Kigongo. Hili ni daraja refu na zuri. Watu wangependa kupiga picha. Kuwazuia wananchi kufaidi mandhari hii si jambo zuri hasa wakati huu ambao utalii wa ndani umeonekana ni jambo la manufaa.

Natambua hatari iliyopo leo ya ugaidi, hata hivyo zipo njia za kisasa za kukabiliana na tishio hilo. Njia iliyobuniwa ya kuwazuia watu kupiga picha ndiyo njia dhaifu kuliko zote. Rais Samia ameanza kuwapa Watanzania uhuru. Napendekeza uhuru huo ukolezwe kwa kuwapa fursa ya kufaidi mandhari nzuri.

Madaraja na majengo ni sehemu ya vivutio vya utalii. Katika Jiji la Chicago nchini Marekani huwezi kufika ukakosa kupelekwa Sears Tower ambalo siku hizi linaitwa Willis Tower. Jirani zetu Rwanda wana mabasi na maeneo maalumu kwa ajili ya kutembeza watalii. 

Sisi jiji kama Dar es Salaam tungeweza kutumia madaraja, majengo marefu, makazi kama ya Mwalimu Nyerere, Mzee Mwinyi, Mzee Kawawa, majengo ya wapigania Uhuru kule Kurasini, Ikulu, na kadhalika kwa ajili ya watalii wa ndani na nje.

Desemba 18, mwaka jana nilikuwa jijini Mwanza, wanangu wakakamatwa na kuonyeshwa mtutu wa bunduki na walinzi wa Rock City Mall kwa sababu tu umepiga picha. 

Fikiria jengo lile mtu haruhusiwi kupiga picha!! Unajiiuliza, wanaofanya hivyo hawajawahi kusafiri duniani? Unamzuia mtu kupiga picha ndani na nje ya jengo zuri kama lile?

Kwa kuongezea, mwaka 2018 nilishauri na narejea leo kushauri uwepo utaratibu kwa uongozi wa Ikulu kuruhusu kupokea watalii wa ndani, hasa wanafunzi ili wafaidi nyumba na ofisi hiyo kuu ya nchi.

Kunaweza kuandaliwa utaratibu wa mara moja moja kwa wanafunzi wa shule za msingi au sekondari kuzuru Ikulu na kuona rais wetu anafanya kazi katika mazingira yepi. 

Watoto watafurahi kuiona ofisi ya rais, watafurahi kuona mandhari ya Ikulu – watabaki na kumbukumbu hiyo kwa maisha yao yote. 

Hilo naamini litakuwa jambo jema na la kuvutia kwani litawafanya watoto watakaopata fursa hiyo kujivunia nchi yao. Fikiria mtoto wa shule ya msingi akapiga picha na Rais Samia wakiwa Ikulu atakuwa na mtazamo gani kuhusu nchi yake!

Ikulu ya Dar es Salaam tangu utawala wa Rais Magufuli, pamekuwa kama eneo wasilotakiwa watu kupita wala kuchungulia. Sawa, usalama wa rais wetu ni muhimu sana, lakini si kwa namna ya kuwafanya Watanzania waione Ikulu kama mahali wasipostahili kujivunia. 

Nashauri uwepo utaratibu kama wa White House ambako wageni kwa wenyeji hufurika kila siku kupiga picha za kumbukumbu.

Tunapaswa kubadili mtazamo uliodumu wa kuamini kuwa utalii wa ndani maana yake ni kwenda kuwaona nyumbu hifadhini. Utalii wa ndani ni pamoja na kuzuru maeneo yenye mvuto, madaraja na ofisi kama Ikulu. Tuwape Watanzania wigo mpana wa kupata raha ya haya yanayotekelezwa na serikali yao.

By Jamhuri