Na Fauzia Mussa, Maelezo Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapuinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema  Serikali inatoa fursa  kwa wawekezaji katika sekta ya Mafuta na Gesi Asilia  ili kuweza kutekeleza  shughuli hizo.

Akizindua duru ya kwanza ya uwekezaji wa vitalu vya mafuta na gesi asilia kwa maeneo ya baharini katika hoteli ya golden tulip, uwanja wa ndege  Zanzibar amesema hatua hiyo itaitangaza Zanzibar kuwa sehemu ya uwekezaji wa mafuta na gesi asilia.

Amesema Zanzibar imepata sifa ya kutambulika kuwa ni mahali pazuri na salama kwa makampuni kuwekeza  hivyo uzinduzi huo umelenga kuwakaribisha wawekezaji katika sekta ya mafuta na gesi Asilia kwa kufungua na kuharakisha shughuli za utafutaji  wa nishati hiyo. 

Amesema Serikali inaamini kuwa Uchumi wa Buluu unafursa nyingi za kukuza mipango ya maendeleo ya kiuchumi yenye lengo la kupunguza umaskini na kutengeneza fursa za ajira nchini.

Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Dhamira ya Serikali katika uchumi wa buluu ni kuimarisha uchumi wa nchi kwa haraka na kupata maendeleo endelevu katika sekta mbalimbali ikiwemo ya vyanzo vya nishati ya uhakika.

Aidha amesema Serikali imefanya mapitio ya mifumo ya kisheria na kimkataba ya Mafuta na Gesi Asilia uliolenga kuimarisha masharti ya fedha ili  kuvutia uwekezaji na  kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji Nchini.

Kwa upande wake waziri wa uchumi wa buluu na auvuvi Mhe. Shaaban Ali Othman amesema  vitalu vinane vipo tayari kwa uwekezaji na kuwataka  wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kupeleka  maombi .

Amefahamisha kuwa  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Mafuta  na gesi  asilia namba 6 ya mwaka 2016 na mapitio ya Modeli ya Mkataba wa kugawana uzalishaji wa mafuta na gesi asilia ya mwaka 2017, kwa lengo la kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji katika utafutaji, uchimbaji, na uendelezaji wa mafuta na gesi Asilia ili kuwavutia wawekezaji.

Hata hivyo Mhe. Shaaban   amesema kuwa uwekezaji huo hautaathiri hali za wananchi na umelenga kuinua uchumi wa nchi na kuzingatia maslahi ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Nao baadhi ya washiriki katika uzinduzi huo akiwemo  Mkurugenzi mwendeshaji Jumuiya ya maendeleo ya mafuta na gesi asilia (ZPDC)Mikidadi  Ali Rashid  na Mkurugenzi mwendeshaji Mamlaka ya udhibiti wa utafutaji wa mafuta na gesi asilia (ZPRA) Adam Abdulla Makame wamesema tayari imeshaandaa utaratibu maalum wa kupokea maombi kutoka kwa wawekezaji.

Hata hivyo wamesema matarajio yao baada ya kutangazwa vitalu hivyo ni kuwa  kampuni mbalimbali zitajitokeza  kufanya maombi na kufanya tathmini ili kukamilisha zoezi la kumpata mwekezaji.

Itakumbukwa kuwa Shughuli za utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa upande wa Zanzibar, zilianza miaka ya 1950 wakati Kampuni ya British Petroleum (BP) kwa kushirikiana na Kampuni ya Shell zilipofanya uchunguzi wa kina na kuchimba visima viwili kwa pande zote mbili za visiwa vya Zanzibar.

Aidha hatua mpya ya maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi Zanzibar ilianzishwa mwaka 2015 kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Petroli Na 21 ya mwaka 2015 ya Tanzania iliyoiruhusu kila upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusimamia shughuli za Mafuta na Gesi Asilia wenyewe.