Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,

Makamu wa Rais Dkt. Phillip Mpango, anatarajaiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ugawaji wa Tuzo za Rais kwa Mzalishaji Bora wa Mwaka (PMAYA), zitakazotolewa siku ya Ijumaa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Kwanza wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), Hussein Sufian amesema Dkt. Mpango atamwakilisha Rais Samia Suluhu Hasssan na kwamba tukio hilo litahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa.

Hawa Bayuni ambaye ni Meneja wa Mambo ya Nje wa kiwanda cha ALAF ambacho ni mmoja wa wadhamini akizungumza kuhusu Tuzo za Rais Kwa Mzalishaji Bora wa Mwaka (PMAYA) ambazo zinatarajiwa kutolewa na Makamu wa Rais Dk. Phillip Mpango siku ya Ijumaa.

Amesema Rais ndiye mlezi wa tuzo hizo na ndiye amekuwa akizitoa kila mwaka kwa mzalishaji tangu kuanzishwa kwa tuzo hizo mwaka 2005 na kwamba nia ni kutambua mchango wa wenye viwanda katika ukuaji wa uchumi.

Amewataja mfadhili mkuu wa tuzo hizo kuwa ni Benki ya Taifa ya Biashara NBC akifuatiwa na Tanga Cement Ltd, ALAF Ltd, Kilimanjaro Cables, Coca Cola Kwanza , Kiwanda cha Sigara (TCC) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Sufian amewataka wenye viwanda nchini na wanachama wote wa CTI kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika maono yake ya kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Mtanga Noor mbaye kutoka Kiwanda cha Saruji Tanga  ambacho ni mmoja wa wadhamini wa tuzo hizo akizungumza kuhusu Tuzo za Rais Kwa Mzalishaji Bora wa Mwaka (PMAYA) ambazo zinatarajiwa kutolewa na Makamu wa Rais Dk. Phillip Mpango siku ya Ijumaa.

“PMAYA inatoa changamoto kwa makampuni makubwa na madogo kuongeza na kuboresha uzalishaji wa bidhaa zao na huduma wanazotoa tunashukuru sana kwa msaada tuliopata kutoka kwa wadhamini wa tuzo hizi. Nawahamasisha wenye viwanda waendelee kuzalisha bidhaa bora zitakazoweza kushindana kwenye soko la dunia” amesema

Amesema lengo la PMAYA ni kutoa zawadi kwa kampuni zilizoonyesha ubunifu kwenye matumizi ya teknolijia na kampuni ambazo zimeongeza uuzaji wa bidhaa nje ya nchi na kuisaidia nchi kuwa na fedha nyingi za kigeni.

“Kama mnavyofahamu ili uchumi ukue lazima pia nchi iwe na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni kwa hiyo serikali inaweka mazingira mazuri ili viwanda vya ndani viweze kuuza zaidi nje ya nchi ili ipate fedha za kigeni,” amesema.

Aidha, amesema kazi ya kuwatafuta washindi wa tuzo hiyo amepewa mtu binafsi wa kampuni ya Data Works ambaye amewatembelea wazalishaji na kutumia vigezo vilivyowekwa na siku ya Ijumaa atatoa majina ya kampuni zilizokidhi vigezo na kutajwa kuwa washindi kwenye mashindano ya mwaka huu.

Makamu Mwenyekiti wa Kwanza wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), Hussein Sufian akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu Tuzo za Rais Kwa Mzalishaji Bora wa Mwaka (PMAYA) ambazo zinatarajiwa kutolewa na Makamu wa Rais Dk. Phillip Mpango siku ya Ijumaa. Kushoto kabisa ni Mtanga Noor kutoka Tanga Cement, James Meitaron kutoka NBC.Kulia kabisa ni David Tarimo kutoka Kilimanjaro Cables na Hawa Bayumi kutoka ALAF Limited.

Amesema Jumuiya ya Ulaya (EU) imedhamini mjadala wa watumiaji wa bandari ya Dar es Salaam hasa wenye viwanda kuhusu namna utoaji wa huduma kwenye bandari hiyo inavyoweza kuboreshwa na kwamba mjadala huo utafanyika siku hiyo ya Ijumaa asubuhi.

“Mwisho lakini si kwa umuhimu napenda kuishukuru serikali kwa kuboresha mazingira ya biashara na kuendelea kusukuma ndoto kuhakikisha Tanzania inakuwa kwa uchumi wa viwanda ili viwanda vilivyopo vikuwe na viendelee na hatimaye vitoe mchango mkubwa kwenye ustawi wa nchi yetu,” amesema Sufiani.

Naye Mkurugenzi wa Makampuni Makubwa na Uwekezaji kutoka benki ya Taifa ya Biashara (NBC), ambao ndio wadhamini wakuu James Meitaron, alishukuru CTI kwa kuwaamini kuwa wadhamini wakuu wa tuzo za mwaka huu.

“Tunajivunia kuwa sehemu ya ukuzaji wa viwanda nchini mwetu tunamshukuru Rais Samia kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara na kustawisha biashara, benki yetu ni ya tatu kwa ukubwa wa mali na mtandao wa matawi tunaahidi kuendelea kuwa karibu na wafanyabiashara na wenye viwanda,” amesema