Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Babati

Kampuni ya Uwindaji wa Kitalii ya EBN Hunting Safari Ltd ambayo inafanya shughuli zake katika kitalu cha uwindaji cha Hifadhi ya Jamii ya Qanyamapori ya Burunge wilayani Babati imetoa gari aina ya Land Cruiser ili kusaidia shughuli za uhifadhi na Kupambana na ujangili katika eneo la Burunge WMA.

Gari hilo ambalo limegharimu shilingi 205 milioni limekabidhiwa na Katibu wa EBN Hunting Safari Ltd , Charles Sylvester kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Babati,Anna Mbongo ambaye nae aliwakabidhi viongozi wa Burunge WMA.

Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo, Sylvester amesema gari hilo ni sehemu ya makubaliano ya mkataba baina ya EBN na Burunge WMA ambapo baada ya miaka mitano gari jingine jipya litatolewa.

“EBN ina Imani gari hili litatumika vizuri ikiwepo kusaidia kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na Binaadamu lakini pia kukabiliana na ujangili”alisema

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Babati,Anna Mbongo kwa niaba ya Mkuu ya Mkuu wa wilaya ya Babati, Lazaro Twange alipongeza Kampuni ya EBN kwa kutekeleza makubaliano ya mkutano kwa wakati.

Alisema gari hilo pamoja na fedha nyingine ambazo zimetokewa na EBN vinapaswa kutumika vizuri kuendeleza uhifadhi na kutatua changamoto za wananchi.

Katibu wa EBN Hunting Safari Ltd Charles Sylvester akimkabidhi kadi ya gari Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Babati Anna Mbogo kwa ajili ya kusaidia uhifadhi Burunge WMA

“Vijiji 10 ambavyo vinaunda hifadhi hii ya Burunge vimekuwa na Maendeleo makubwa na tunaimani wananchi wataendelea kushiriki katika uhifadhi ili waendelee kunufaika”alisema

Meneja Mkuu wa Chemchem Association ambayo inashirikiana na EBN,Clever Zulu akisoma salamu za wakurugenzi wa EBN, alisema wanaimani kubwa kuimarika uhifadhi katika eneo hilo.

Zulu alisema EBN Hunting Safari Ltd itaendelea kushirikiana na Burunge WMA na wananchi wa Wilaya ya Babati na mkoa wa Manyara katika kuendeleza uhifadhi nakuvutia watalii zaidi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Burunge WMA, Patricia William alisema EBN imekuwa na ushirikiano mkubwa katika kuendeleza uhifadhi na Utalii Burunge WMA na wanaimani kuendelea kupata ushirikiano mkubwa.

“Gari hili ni sehemu ya makubaliano yetu na watatua gari jingine na tunatarajia pia wataendelea kushirikiana na WMA katika kulinda hifadhi hiyo ili kuendeleza Utalii”alisema

Katibu wa Burunge WMA,Benson Mwaise aliahidi kutunzwa kwa gari hilo na kuwa litasaidia sana katika kazi za kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na Binaadamu lakini pia Kupambana na ujangili.

Afisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Babati Emmanuel Laizer alitaka Burunge WMA kutumia gari hilo kupunguza migogoro ya wanyamapori kuharibu mazao ya wananchi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Babati Anna Mbogo akimkabidhi kadi ya Gari Mwenyekiti wa Bodi ya Burunge WMA Patricia William kulia Katibu EBN Hunting Safari Ltd Charles Sylvester

By Jamhuri