Mwakinyo abadilishiwa mpinzani, apewa mjeshi

Ikiwa imesalia siku moja kufikia Januari 27, 2024 siku ya pambano la ‘Mtata Mtatuzi’, Bondia Hassan Mwakinyo amebadilishwa mpinzani wa kucheza nae na kupewa Elvis Ahorgah kutoka Ghana.

Mwakinyo ambaye awali alitakiwa kucheza na Mbiya Kanku kutoka Congo, wakiwania mkanda wa WBO Afrika, amelalamikia baadhi ya watu kumtumia meseji za vitisho mpinzani wake hadi kufikia hatua ya kuogopa kuja kucheza nae.

Mwakinyo amewatoa hofu mashabiki wake kuwa licha ya mpinzani wake wa sasa kuwa mzuri ulingoni, atapambana na kuhakikisha mkanda unabaki nyumbani.

Aidha Ahorgah amesema amepitia mapambano kadhaa ya Mwakinyo na kugundua ni bondia mzuri lakini yeye ni mzuri zaidi yake, huku akitoa ombi kwa majaji na marefa kutenda haki.

Mwakinyo na mpinzani wake wanatarajiwa kupima uzito kesho maeneo ya Darajani majira ya saa 10 jioni na kupanda ulingoni katika ukumbi wa ndani wa uwanja wa Amani visiwani Zanzibar.