Tuepuke kuishi maisha ya majivuno. Mwandishi Nadeem Kazi anatufundisha kwamba: “Hatuwezi kupanda juu kwa kuwashusha wengine chini.” Tunapanda juu kwa kuwasaidia wengine kupanda. Katika maisha lazima pia tujifunze kuwasaidia wengine. Huwezi kufanikiwa kiroho, kiuchumi, kifamilia, kiutawala, kielimu, kimaadili na kiafya kwa kuwaangusha wengine chini. Yule anayejitolea kuwasaidia wengine ndiye huinuliwa na watu aliowasaidia kuinuka.

Bila shaka umewahi kujiuliza: “Kwa nini fulani amefungua biashara yake lakini imestawi kwa miaka michache halafu ikafa?” Napenda nilijibu swali hili katika mada hii tunayoendelea nayo. Iko hivi, mtu  yeyote anapoanzisha biashara au mradi huwa ana unyenyekevu na upole wa hali ya juu sana kwake yeye mwenyewe na kwa wasaidizi wake kama anao na kwa wateja wake pia. Mara biashara inapostawi majivuno yanaota mizizi. Majivuno yanapoota mizizi na kukomaa anaanza kuwaona wafanyakazi wake kama vikaragosi. Anawadharau. Huo ndio unakuwa mwanzo wa anguko la  biashara yake ama mradi wake.

Padri Yohane Vianei ni padri Mkatoliki aliyeishi maisha ya unyenyekevu  sana. Siku moja alipata barua mbili ambazo haijulikani ziliandikwa na nani. Barua moja ilimtaja kama mtakatifu, barua nyingine ilimtaja kama mnafiki na mpiga porojo. Padri Vianei baada ya kuisoma barua ya kwanza alisema: “Hainiongezei chochote.” Ya pili alisema: “Hainipunguzii chochote.” Mbele ya Mungu tunapimwa kwa kuishi maisha ya unyeyekevu. Mimi najitahidi kuishi maisha ya unyenyekevu ili nipate nafasi katika ufalme wa Mungu.

Maisha ya majivuno hayana faida yoyote, isipokuwa yana hasara isiyolipika kwa urahisi. Mwandishi James Mathew Barrie anasema: “Maisha ni somo lefu katika unyenyekevu.” Tuishi maisha yanayotawaliwa na upendo. Maisha ni upendo. Maisha yanazungumza katika upendo. Ukitaka kuuona upendo, ishi upendo. Upendo ni lugha ambayo kiziwi anaweza kuisikia na ambayo kipofu anaweza kuiona. Uruhusu upendo uyatawale maisha yako. Usiruhusu hata siku moja ipite pasipo kupanda mbegu ya upendo wa kweli, upendo usio wa kinafiki, upendo utokao moyoni na upendo ushindao majaribu.

Yesu Kristo aliwahimiza wanafunzi wake kwa nasaha hii: “Pendaneni kama nilivyowapenda ninyi.’’ [Yn 13:34]. Ni lazima tujitahidi kuyajenga maisha yetu katika msingi wa upendo. Furaha kamili ipo katika kuishi maisha ya upendo. Tupendane. Mwandishi Freidrich Rucket anasema: “Upendo ni kitu kikubwa sana ambacho Mungu anaweza kutupa, na kitu kikubwa sana ambacho tunaweza kumpa Mungu.”

Benjamin Edwin ni jina la rafiki yangu ambaye tulifahamiana kwa muda mrefu. Wiki moja kabla ya kupata ajali  mbaya ya gari iliyosababisha kifo chake, alinitumia ujumbe mfupi kwa njia ya simu ya kiganjani. Ujumbe huo ulikuwa unasomeka hivi: “Siku nikifa utatoa machozi lakini sitayaona. Utaniletea maua lakini sitayapokea. Utanisifia sana lakini sitakusikia. Utahuzunika sana lakini sitakuona. Utanisamehe makosa yangu yote lakini sitajua. Ninafahamu haya yote ipo siku yatatokea. Nipe zawadi ya ‘Upendo’ nikiwa ningali hai.”

Huo ndio ujumbe ambao rafiki yangu Benjamin Edwin aliniusia kabla ya kumaliza safari yake ya maisha ya hapa duniani. Namwomba Mungu ampokee Benjamin Edwin katika ufalme wake wa milele.

Katika makala hii ninaomba tupate fursa ya kutafakari maisha yetu. Sisi sote tulio dhaifu kiroho, kimwili, kiakili, kiutashi na kimapendo tunahitaji huruma ya Mungu. Tunahitaji huruma ya Mungu ili maisha yetu na matendo yetu yaongozwe na tabia ya upendo. Lengo letu la kwanza katika maisha ni kuwasaidia wengine, kama hatuwezi kuwasaidia wengine basi tusiwaumize.

Fumbua macho yako utazame. Tazama upya uhusiano wako na Mungu wako. Tazama upya uhusiano wako na mke/mume wako. Tazama upya uhusiano wako na watoto wako. Tazama upya uhusiano wako na majirani zako. Tazama upya uhusiano wako na kazi yako. Tazama upya uhusiano wako na wafanyakazi wenzako.

Baada ya kutazama umebaini nini? Je, umebaini kasoro za kiuhusiano? Jifunze kumwomba msamaha aliyekukosea na uliyemkosea pasipo kusita. Siku yako ya ushindi ni siku ile unayomwomba msamaha aliyekukosea na uliyemkosea. Kumbuka: Mungu anakutafuta ili urekebishe mambo ambayo hayaendi sawa. Usikate tamaa bado unayo nafasi ya kuboresha uhusiano na Mungu wako, mke wako, watoto wako, jirani zako na wafanyakazi wenzako. Oren Arnold [1900-1980] mhariri na mwandishi wa kujitegemea aliyezaliwa Texas, Marekani alikuwa na haya ya kusema juu ya zawadi za kutoa wakati wa Krisimasi. Alisema: “Kwa adui yako, msamaha. Kwa mpinzani wako, uvumilivu. Kwa rafiki yako, moyo wako. Kwa wateja wako, huduma nzuri. Kwa watu wote, upendo. Kwa kila mtoto, mfano mzuri. Kwako wewe, heshima.”

By Jamhuri