Na G. Madaraka Nyerere

Tumesikia hivi karibuni kuwa kati ya mashirika ya umma ambayo yanapata hasara kubwa ni Air Tanzania Corporation Limited (ATCL), shirika letu la ndege la Taifa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) iliyosomwa bungeni na mwenyekiti wa kamati hiyo, Albert Mtabaliba, ATCL imepata hasara kwa miaka mitatu mfululizo: sh. 94.3 bilioni mwaka 2014/2015, sh. 109.3 bilioni mwaka 2015/2016, na sh. 113.8 bilioni mwaka 2016/2017.

Tunafahamu kuwa matatizo ya uendeshaji ya ATCL ni ya muda mrefu, hayakuanza leo, kwa hiyo tunasikia marudio ya taarifa ambazo tumeshazisikia.

Kila ninaposikia haya maneno yasiyoisha, nakumbuka pia mafanikio makubwa ya shirika la ndege lingine jirani, Ethiopian Airlines.

Halafu linafuata swali: ndugu zetu – Waafrika wenzetu – wa Ethiopia wanakula chakula gani kinachowaletea mafanikio hayo ambacho sisi tumeshindwa kula?

Nimesisitiza Uafrika wa hao ndugu zetu kwa sababu ya sumu ya fikra za unyonge tunayolishwa na wengine na tunayojilisha sisi wenyewe na vizazi vyetu inayosimika mawazo kwamba Waafrika hawana mafanikio ya maana zaidi ya vita na maradhi.

Zaidi ya Uafrika kama sumu ya kufikirika inayokwamisha maendeleo, historia inatukumbusha kuwa kati ya mwaka 1987 hadi 1991 Ethiopia iliongozwa na serikali iliyofuata sera za kikomunisti, zenye msingi juu ya itikadi ambayo pia ilionekana kama kikwazo kwa maendeleo ya jamii na uchumi.

Lakini bado tunafahamu kuwa, hata kwenye mazingira hayo ya sera ambazo siku hizi zinaitwa kuwa si rafiki kwa biashara na uchumi shirika la ndege la Ethiopian halikufa na likashamiri.

Somo la mafanikio ya Ethiopian ni somo rahisi sana kulielewa; ni matokeo ya serikali kutoingilia uendeshaji wa shirika la biashara kwa kuteua menejimenti yenye uzoefu na kuwekeza vya kutosha kutimiza malengo yanayowekwa na menejimenti.

Mafanikio yanafuata kwa kuzingatia masuala hayo ya msingi. Serikali ya kikomunisti au ya kijamaa ingesisitiza mmiliki mkuu kuwa serikali au shirika la umma wakati serikali za itikadi nyingine zingeacha watu au mashirika binafsi kuwa wamiliki, lakini ili mradi linazingatiwa suala la kutoingilia usimamizi wa biashara basi uwezekano wa mafanikio unaongezeka.

Na serikali ya Ethiopia haikufanyia mzaha jukumu la kulinda uhuru wa menejimenti ya Ethiopian. Afisa wa kijeshi aliyewahi kujaribu kukiuka msimamo huu aliuwawa kwa kupigwa risasi hadharani na kutoa kinga dhidi ya yoyote mwingine mwenye wazo kama lake. Kuanzia hapo napata picha kuwa askari wa aina yoyote, hata mgambo, hakukaribia tena Ethiopian hata kuwajulia hali tu.

Ethiopian ina mmiliki mmoja tu, serikali ya Ethiopia, lakini ina uhuru wa kujiendesha bila kuingiliwa. Sina hakika iwapo ATCL inao uhuru huo, au kama haina ni kwa kiasi gani. Tunachoweza kusema ni kuwa kama Ethiopian inafanikiwa kwa sababu ya uhuru mkubwa wa maamuzi ya menejimenti yake, inawezekana mashirika mengi ya ndege ya Afrika, pamoja na ATCL, yanasuasua au kufa kwa sababu ya kukosa uhuru huo.

Ethiopian ilianzishwa zaidi ya miaka 72 iliyopita ikishuhudia mashirika mengi ya Afrika na hata katika nchi zilizoendelea yakianzishwa na kufa.

Katika uwepo wake imewekeza kwenye miundombinu ya matengenezo ya ndege zake, imeanzisha vyuo vya mafunzo mbalimbali ya masomo ya biashara ya usafirishaji wa anga, ikiwa ni pamoja na urubani, na menejimenti. Leo hii inamiliki ndege karibia 100.

Mwaka 2010 shirika hilo lilitimiza malengo yake ya Visheni 2010 ikiwa ni pamoja na kufikisha mapato yake hadi dola za Marekani 10 bilioni, likiwa na faida ya dola 121.4 milioni. Mafanikio haya yameendelea na kwa miaka mitano mfululizo hadi mwaka jana Ethiopian inaongoza kama shirika la ndege lenye faida kubwa barani Afrika.

Jambo moja linalosemwa kulinda na kukuza mafanikio ya shirika hili ni sumu nyingine nzuri ambayo serikali na menejimenti ya Ethiopian wamejishibisha: uzalendo.

Ni hali ya kuipenda nchi na kulinda maslahi yake kwa uwezo wote ambao raia anao bila kutegemea manufaa yoyote binafsi.

Wachambuzi wanasema kuwa, pamoja na uzalendo, sifa za mashirika ya ndege yanayofanikiwa ni kuwepo kwa visheni imara, kutokukata tamaa kwa menejimenti na wafanyakazi, na kuepuka vishawishi vya ufisadi.

Sina ushahidi wa ufisadi wa hivi karibuni wa ATCL lakini Tanzania inayo historia ya ufisadi ndani ya mashirika yake ya umma, ufisadi ambao ulianzishwa na menejimenti zake, na kupata baraka za bodi zake za wakurugenzi.

Kwa lugha rahisi kuelezea hali ya baadhi ya mashirika haya, tuliajiri fisi kuchunga bucha tukiamini kuwa minofu itazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka. Matokeo yake ni kuwa, kwa baadhi ya mashirika, tulipozinduka hata harufu ya mifupa hatukupata.

Ethiopian inasifika kwa umahiri wa kuongeza mapato na kudhibiti matumizi. Katika taarifa ya Kamati ya Bunge tumeambiwa kuwa ATCL imejiongezea hasara kwa kushindwa kudhibiti matumizi.

Inabidi kuuliza iweje tuko jirani na shirika la Kiafrika linaloendeshwa kwa ufanisi na faida kubwa halafu tushindwe kujifunza kutoka kwao? Sitashangaa kusikia wataalam wetu wamesafiri kwenda mbali na nje ya bara letu kutafuta ushauri wa namna ya kuleta ufanisi ATCL bila kwenda Addis Ababa kutafuta ushauri huo huo.

Haiwezekani kuendesha shirika kwa mafanikio kwa miaka 72 bila kuwa na uwezo mkubwa wa kufundisha misingi muhimu ya mafanikio hayo.

Yapo mengi ya kujifunza kutoka Ethiopian. Tukubali kurudi darasani tu.

Please follow and like us:
Pin Share