NA EDITHA MAJURA

Mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 14 katika Shule ya Msingi (xxx) mjini Dodoma, ameshindwa kuendelea na masomo kutokana na kupewa mimba na baba yake mdogo.

Mwanafunzi huyo (jina tunalihifadhi) alipaswa kuwa darasa la tano baada ya kufaulu mtihani wa darasa la nne mwaka jana.

Katika mahojiano maalumu na JAMHURI nyumbani kwao Nzuguni B, mtoto huyo amethibitisha kuwa ni mjamzito na kwamba anatarajia kujifungua muda wowote kuanzia Machi mwaka huu.

Hata hivyo, wakati msichana huyo anamtaja mtu aliyempa mimba kwa jina moja la Mathayo kuwa ni jirani yao, bibi anayemlea msichana huyo, Mdala Blandina, amesema Mathayo ni baba mdogo wa msichana huyo.

Kwa mujibu wa Blandina, familia za wawili hao (Mathayo na msichana huyo) zipo kwenye mgogoro kuhusiana na tukio hilo, ingawa baba wa msichana huyo alifariki Oktoba mwaka jana.

Blandina amesema wakati wa msiba huo ukitokea, msichana huyo alikuwa akijiandaa kufanya mitihani ya taifa ya darasa la nne.

Msichana huyo amesema wakati huo, ujauzito wake ulikuwa wa miezi mitano, lakini hapakuwa na mwanafamilia aliyefahamu.

“Hata mimi nimefahamu kuwa nina mimba baada ya kuona tumbo linazidi kuwa kubwa na nikawa nahisi kitu kinachezacheza tumboni, mwanzo nilikuwa sipati hedhi,”  amesema msichana huyo.

Amesema awali, alitaka kuitoa mimba hiyo lakini akahofia madhara anayoweza kuyapata kutokana na kuwa na muda mrefu.

“Baada ya kukosa siku zangu (hedhi) nilidhani ni kawaida na hata nilipogundua kuwa ni mjamzito ilikuwa vigumu kutoa kwa sababu ilishakuwa kubwa,” amesema.

Amesema mama yake mzazi alitengana na baba yake wakati akiwa mdogo, na kwamba jitihada zake za kumtafuta hazijafanikiwa, hivyo hajawahi kumuona.

Mlezi wa msichana huyo anayemtambulisha kuwa ni mama yake (hakutaja majina) amesema baada ya kuachana, baba wa msichana huyo alimuoa mwanamke mwingine, ambaye kwa sasa anaishi mkoani Tanga.

“Huyo mama alipokuja kwenye msiba wa mzazi mwenzake, alimuhoji binti yake kisha akamuita Mathayo ambaye alikiri kuhusika na ujauzito, akamtaka azungumze na wazazi wake, lakini badala ya kuleta mrejesho, ikaibuka vita ya maneno mpaka leo hatuelewi la kufanya,” amesema Blandina.

SHULENI

Mmoja wa walimu wa Shule ya Msingi Nzuguni, kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini, amethibitisha kumfahamu binti huyo na kwamba hajafika shuleni kwa muda mrefu kutokana na kuwa mjamzito.

“Shuleni hatujatangaziwa rasmi lakini wengi tunafahamu kuwa binti huyo ni mjamzito, tatizo kubwa ni uangalizi wa watoto wanapokuwa nyumbani, wazazi wengine wanawaachia watoto uhuru ambao unaishia kuwaingiza kwenye majanga,” ameeleza mwalimu huyo.

Mwalimu huyo amesema watoto wengi wanashiriki ngono katika umri mdogo, kutokana na mazingira yasiyofaa na kuomba wazazi kupunguza shughuli za kiuchumi ili waweze kutoa malezi bora kwa watoto wao kwa sababu wao (walimu) peke yao, hawatamudu kukabiliana na changamoto hizo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nzuguni ‘B’, Pauline Machibya, amesema hajapata taarifa kuhusu msichana huyo kutokana na kuhamia shuleni hapo hivi karibuni.

Wakati wa mahojiano hayo, mtangulizi wake, Lilian Lwiva, alikuwa shuleni hapo akimalizia mchakato wa kustaafu.

Lwiva, amethibitisha msichana huyo kusoma shuleni hapo na kwamba ni miongoni mwa wanafunzi watoro wa muda mrefu.

Amesema jina lake na watoro wengine wamepelekwa kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Nzuguni ‘B’ wiki iliyopita, kwa hatua zaidi za utekelezaji.

Amesema akiwa darasa la nne, mwaka jana, shule ilipelekewa taarifa kuwa binti huyo alifiwa na baba yake mzazi, baada ya hapo hakuonekana tena shuleni.

Hata hivyo, amesema taarifa zisizothibitishwa rasmi zinaeleza kuwa msichana huyo ni mjamzito.

“Tunachosubiri ni Serikali kuwakamata na kuwafikisha hapa wanafunzi watoro wakiwamo wanaoshukiwa kuwa na ujauzito wapelekwe polisi kupata kibali cha kupimwa na ikithibitika basi hatua za kisheria zichukuliwe,” amesema.

AFISA MTENDAJI ANENA

Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Siwazuri Kalikule, amethibitisha kupokea majina ya wanafunzi watoro kutoka shuleni hapo, lakini hajajua ikiwa miongoni mwao wana mimba.

“Kama kuna mwanafunzi mjamzito, atakuwa miongoni mwa hawa watoro na ili nielezwe kuhusu hilo ni lazima awe amepimwa na kuthibitika hivyo,” amesema.

Kalikule ameuandikia barua uongozi wa shule hiyo ujumuishe jina la mjumbe wa shina anapoishi kila mwanafunzi mtoro, ili iwe rahasi kuwafikia na kuchukua hatua.

Amesema shule hiyo inawahudumia wanafunzi kutoka Mtaa wa Nzunguni ‘B’ na ‘C’ hivyo kupewa majina bila maelekezo ya ziada ni vigumu kuwapata wanafunzi watoro.

VIONGOZI WA DINI WAONYA

Katekista wa Kanisa Katoliki anayeongoza Mitaa ya Nzuguni ‘C’ na ‘B’, Charles Matonya, ikiwa msichana huyo ni mjamzito, ni kosa sheria za nchi na amri za Mungu.

Amesema tukio hilo linaashiria mmomonyoko wa maadili kwenye jamii, hivyo haipaswi kufumbiwa macho.

Kwa upande wake, kiongozi wa Kanisa la Anglikana wa Mtaa wa Nzuguni ‘B’, Esau Mhulo, amekiri kuwa binti aliyepata mimba akiwa shuleni ni muumini wa kanisa hilo akitokea kwenye familia isiyoshiriki vizuri kanisani hapo.

“Hata bibi yake tumekuwa naye baada ya kupatwa na msiba wa baba wa binti huyu, lakini siyo waumini wanaohudhuria vyema shughuli za kanisa, ” amesema Mhulo.

Mhulo amesema matukio ya aina hiyo yanapotokea, yanashindikana kushughulikiwa ipasavyo kutokana na jinsi familia zinavyoyamaliza kwa makubaliano.

Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Elimu wa Wilaya wa Mkoa wa Dodoma, wanafunzi 67 walishindwa kufanya mtihani wa taifa wa kuhitimu Elimu ya Msingi, huku manispaa ya Dodoma, ikitajwa kuwa na wanafunzi 12 ambao walikosa kuhitimu masomo hayo kwa sababu ya mimba.

Alivyoanza kujihusisha na ngono

Msichana huyo amesema mwaka 2013, (akiwa na umri wa miaka 9) alikwenda kwenye muziki (disko toto) wakati wa kusherehekea Krismasi.

Amesema akiwa katika sherehe hizo alikutana na kijana anayemtaja kwa jina la Bakari.

“Akanitongoza na mimi nikashindwa kumkatalia, nilitoka naye kama mara mbili hivi baadaye tukaachana. Ilikuwa mpaka nimfate kule Shabiby (kituo cha daladala cha Nzuguni),”amesema msichana huyo.

Amesema kwamba Bakari anafanya biashara ya kusafirisha abiria kwa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda na alikuwa akimpatia fedha Shilingi 5000 kila walipokutana kimapenzi.

Msichana huyo amesema, alipoachana na Bakari mwaka 2014, alianza uhusiano wa kimapenzi na Mathayo mwaka huo huo 2014.

“Tumetoka mara nyingi tu nilikuwa sipati mimba kwa kuwa tulikuwa tunatumia kinga (kondomu), tulipozoweana akaanza kukataa kutumia kinga, baadaye nikawa sipati siku zangu na tumbo likaanza kuwa kubwa, kumbe nina mimba,” amesema msichana huyo.

Amesema binafsi anaijutia hali hiyo kwani hajui hatima yake wala mtoto anayetarajia kumzaa atamlea vipi.

By Jamhuri