Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA, Cape Town
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amewakaribisha Wawekezaji kuja Tanzania kuwekeza katika Utafiti, Uchimbaji pamoja kujenga Viwanda vya kusafishia Madini, ili kuongeza thamani kabla ya kusafirishwa kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi.
Amesema kuwa Sera nzuri za Tanzania katika Uwekezaji wa Sekta ya Madini pamoja na mambo mengine imelenga kuleta manufaa kwa Nchi na pamoja Wawekezaji.
Aliyasema hayo Oktoba 18, 2023, Jijini Cape Town nchini Afrika Kusini, wakati akizungumza katika Mkutano wa Mawaziri uliolenga kujadili Utajiri wa Madini Mkakati na namna ya kuimarisha Ushirikiano baina ya Nchi zenye utajiri huo na Nchi za Afrika, Mataifa yenye mitaji pamoja na Watengenezaji wa vifaa vinavyotokana na Madini Mkakati.
Dkt. Kiruswa alifafanua kuwa nchini Tanzania wapo Wawekezaji katika Madini ya Dhahabu(Barrick Co. Ltd) Graphite(Lindi Jumbo), Nickel (BHP) na Rare Earth Elements (Nguala REE project) miradi yote ikiwa katika hatua mbalimbali na kwamba Tanzania inakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika Sekta ya Madini.
Vilevile, Dkt. Kiruswa aliongeza kuwa tayari Umoja wa nchi za Ulaya (EU) upo katika mpango wa kujadiliana na Tanzania na kuingia Mkataba wa Makubaliano ili kushirikiana kufanya utafiti wa kina.
Dkt. Kiruswa anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo wa kilele wa Madini Mkakati barani Afrika mwaka 2023 ukiwa na lengo la kuiweka Afrika kama kitovu kikuu cha Uwekezaji wa Madini Mkakati.