Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA, Tanga.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ametoa wito kwa Waajiri na Maafisa Utumishi katika taasisi za umma kuwatambua watumishi wenye uwezo kiutendaji ili wapate motisha ya kuendelea kuchapa kazi na kuwafungulia milango ya kupanda vyeo.
Simbachawene ametoa wito huo wakati akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoa wa Tanga wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji, kusikiliza changamoto za watumishi na kuzifanyia kazi.
“Nimefurahi sana kumsikia Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mhe. Kalisti Lazaro akimzungumzia vizuri mmoja wa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe juu ya utendaji kazi wake, na ninyi Watendaji na Maafisa Utumishi muwasemee vizuri watumishi wanaofanya kazi kwa bidii, kwa kuwa ninyi ndio mnaowafahamu watumishi wenu” amesema Simbachawene.
Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iko wazi na imetoa uhuru wa kuongea na wao wakiwa ndio wasaidizi, wanamsaidia kwa kufanya ziara maeneo mbalimbali nchini ili kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuzifanyia kazi kwa lengo la kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Sisi tupo kumsaidia Rais wetu mpendwa, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivyo mtoe dukuku zenu, maoni na pongezi ili kuboresha utumishi wa umma kwa lengo la kuwahudumia wananchi ipasavyo” Mhe. Simbachawene.
Ameongeza kuwa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo mengi mazuri kwa watumishi wa umma ikiwemo kulipa madeni, kupandisha vyeo na stahiki nyingine mbalimbali, hivyo watumishi wana deni la kulipa kwa kuchapa kazi kwa bidii katika kuwatumikia watanzania.