Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA, Mbeya.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis amefanya ziara ya kukagua Mradi wa Kuhifadhi Ardhi katika Bonde la Ziwa Nyasa katika Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.

Katika ziara hiyo amejionea uzalishaji wa biogesi nishati ambayo inapunguza matumizi ya kuni na mkaa, uzalishaji wa miche bora aina ya michikichi pamoja na mashine ya kutotoresha vifaranga vya samaki.

Akiwa katika kata ya Ibanda amemtembelea mkulima na mfugaji Donald Sanga na kumpongeza kwa kuzalisha na kutumia nishati mbadala biogesi kwani ni hatua ya kuunga mkono Serikali kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala na kuepukana na kuni na mkaa zinazotokana na ukataji miti.

“Nampongeza sana mzee huyu kwa kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambae amekuwa akihamasisha matumizi ya nishati mbadala ili kulinda mazingira,” amesema.

Hali kadhalika, Naibu Waziri Khamis ametoa wito kwa uongozi wa Wilaya ya Kyela na Tanzania katika taasisi zao zikiwemo shule na vyuo kujifunza na kutumia tekonojia hiyo ya uzalishaji wa nishati mbadala ikiwemo biogesi ambayo huwezeshaji kupika bila kutumia kuni au mkaa.

Aidha, Naibu Waziri Khamis amewapongeza viongozi na wataalamu kwa kufanya matumizi mazuri ya fedha za mradi zilizotolewa na Serikali kwa kutekeleza vyema shughuli zinazotakiwa.

Amepongeza jitihada zinazofanywa na halmashauri hiyo za kupanda na kuigawa bure kwa wananchi miche ya ambayo wanaipanda na hivyo kuhifadhi mazingira huku akitoa wito wa kuongeza kasi ya uzalishaji wa miche hiyo ili ipandwe kwa wingi.

Pia, akiwa katika bwawa la samaki na mashine ya kutotoresha vifaranga vya samaki Naibu Waziri Khamis amehimiza elimu ya ufugaji wa samaki izidi kutolewa kwa wananchi kwani kufanya hivyo, itasaidia wananchi kuachana na uvuvi haramu na kuanza shughuli za ufugaji wa samaki majumbani.

Kwa upande wake Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa Kuhifadhi Ardhi katika Bonde la Ziwa Nyasa Dkt. Paul Deogratius amesema unatekelezwa pia katika Halmashauri ya Makete na Ludewa (Njombe), Mbinga na Nyasa (Ruvuma).

Amesema unafadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) kwa thamani ya shilingi bilioni mbili kwa lengo la kuiwezesha jamii kufanya shughuli mbadala kukabiliana na changamoto za kimazingira.

Dkt. Paul ameongeza kuwa mradi unawezesha wananchi kupata mafunzo mbalimbali ambayo yanawasaidia wananchi kuweza kutengeneza teknolojia za kuhifahi mazingira na kuwa unatarajiwa kupanuka katika halmashauri zingine.

Nae Mkuu wa Idara ya kilimo, Mifugo na Uvuvi Bw. Keneth Nzilano ameishukuru Serikali kwa kuutekeleza mradi huo katika halmashauri hiyo na kusema ni chachu kwa maendeleo.

Amesema kupitia fedha za mradi zilizotolewa wameweza kujenga bwawa la kufuga samaki na kitotoleshi cha vifaranga wa samaki ambapo kwa wiki wanaweza kuzalisha 300.