Watanzania tunakinyanyasa, kukibeua Kiswahili – 4

Nafikiri bila shuruti lugha yoyote ina taratibu na utamaduni wake katika matumizi, kadharika Kiswahili. Kuna lugha ya kaya, rika, fani, hadhi na kadha wa kadha. Lengo langu si kuzungumzia hayo, bali ni kuzungumzia Kiswahili kunyanyaswa na kubeuliwa.

Kwa hiyo, narudia kuomba na kupenda kwako Kiswahili kwa undani. Je, ni kweli lugha yetu ya Kiswahili inanyanyaswa na kubeuliwa katika matumizi yake ya kila siku? Kama ndivyo, nini sababu na tufanye nini kuepuka hilo?

 

Baada ya kukumbusha hayo, leo naangalia vinashibishi vinavyofanya lugha ya Kiswahili kunyanyaswa. Kwanza, hakuna ubishi kuhusu makundi mawili ya watumiaji Kiswahili kuhitilafiana kwa mujibu wa sehemu wanazotoka.

 

Nina maana kwamba kuna Waswahili wenye kutumia Kiswahili tu wala hawana lugha nyingine. Na kuna Waswahili wenye Kiswahili na lugha ya asili kutoka kwa mama zao. Kiswahili ni lugha ya pili waliyokutana nayo barabarani na shuleni.

 

Wote hawa wanatumia lugha ya Kiswahili katika shughuli zao za kila siku na wanaelewana. Lakini maelewano yao mara nyingine yana kasoro, inayotokana na matumizi ya mkondo wa sauti, mkondo wa herufi na istilahi katika pande mbili za mawasiliano yao.

Makundi yote haya mawili hayana budi kuangaliwa kwa pamoja katika matumizi ya lugha ya Kiswahili, bila kuzingatia fasili katika lugha na makosa ya kisarufi katika mazungumzo na maandishi.

 

Hapa nakumbuka maneno ya Profesa Tigiti Sengo, na namnukuu: ‘Dhana ya utamaduni wa lugha ya Kiswahili ni lazima iwe na mashiko maalumu kwa ajili ya kulea Kiswahili katika maendeleo, kama tusipokilea Kiswahili, kila mmoja akiwachiwa afanye analotaka, basi lugha hii itakuwa imeparaganyika.

 

‘Kwa hiyo tukianza, kwa mfano, tunapozungumza dhana ya utamaduni au mila ya Kiswahili, ni kwamba tuna adabu zetu, tuna heshima zetu na tuna uadilifu wetu.

 

‘Baba na mtoto wanapozungumza wanakuwa na lugha yao, mume na mke wanapozungumza wanakuwa na lugha yao, mwalimu na mwanafunzi wanapozungumza nao wana lugha yao, mtoto mdogo anapozungumza na mtu mzima na kadhalika.

 

Lakini hatuwezi tukachanganya, kwa mfano, mtoto mdogo na baba yake kuambiana mambo, poa au baridi. Haya yanaharibu lugha. Si kwamba hatuwaruhusu wenye kutumia watumie. Lakini lazima wajue maswali haya wanayowauliza ni akina nani, majibu haya wanayatoa kwa akina nani.

 

Nimenukuu maelezo hayo kutaka kuonesha na kusisitiza baadhi ya vinashibishi vinavyonyanyasa Kiswahili kutoka kwa Waswahili wenyewe. Yaani, utamaduni na mila kutozingatiwa, mashiko ya lugha kupuuzwa, malezi ya lugha kudharauliwa na usanifu wa lugha kukosa hamasa.

 

Haya yamedhihirika hivi majuzi na gazeti moja litolewalo kila wiki (si JAMHURI) kueleza kuwa mwana mrimbwende wa Tanzania 2012 kutoka Mkoa wa Kilimanjaro, ameshindwa kuzungumza lugha adhimu ya Kiwashili kwenye semina yake na wabunge kwa madai lugha ya Kiswahili inampa taabu kutokana na kukaa muda mrefu nje ya nchi (Kenya).

 

Kitendo hicho kilimtia fedheha na kuzomewa na wabunge hadi kudiriki kumuona kuwa ni limbukeni wa lugha hiyo aliyoitumia. kwani robo tatu ta watu wa Kenya wanajua kuzungumza Kiswahili.

 

Wabunge wetu nao na hadithi ya ngamia. Ngamia ni mnyama mwenye nundu kubwa mgongoni, lakini kila amuonapo ng’ombe mwenye nundu ndogo mgongoni humcheka. Hivyo, ndiyo ajabu ngamia kucheka nundu ya ng’ombe.

 

Wabunge walimzomea mtoto wao kwa kushindwa kutumia lugha yake ya pili Kiswahili, lugha yake ya kwanza Kichagga, yawezekana hata hao wabunge baadhi yao Kiswahili chao ni kutoka barabarani au shuleni!

 

Wabunge hawa hawa kila siku tunawasikia wanavyochanganya Kiswahili na Kiingereza kwa maana ya kutumia ‘Kiswakiinglish’. Sentensi moja ina maneno matatu ya Kiswahili na maneno matano ya Kiingereza.

 

Natambua kuwa wabunge wameruhusiwa kutumia lugha ya Kiswahili au Kiingereza bungeni, katika kujenga hoja imara na kufafanua hoja zao ili zieleweke kwa wananchi waliowatuma lakini si kuwachanganyia lugha.

 

Kutoka na mazoea yao ya kuchanganya lugha bungeni, na vyombo vya kusimamia usanifu wa lugha kutowasema wala Waswahili kuwazomea, sasa wamejenga mazoea hata ya kuchanganya mambo. Ndiyo maana wanachanganya siasa na kanuni za Bunge, ubabe na methali sanifu za Kiswahili, matokeo yake ni vurugu bungeni.

Please follow and like us:
Pin Share