Kwenye mtandao wa kijamii wa JF, ambao mimi ni mmoja wa wanachama wake, nimekutana na makala fupi, lakini yenye kuelimisha sana.

Imeandikwa na mwanachama anayetambulika kwa jina la Vuta Nkuvute. Mambo yaliyojaa busara na hekima kama haya, ni vema tukawa tunapeana, hasa kwa wasomaji ambao si wapenzi au watumiaji wa mitandao ya kijamii.

 

Makala ya Vuta Nkuvute imejitahidi kukidhi kiu niliyokuwa nayo baada ya kusikiliza uamuzi wa Serikali wa kufuta matokeo ya aibu ya kidato cha nne ya mwaka 2012. Mara baada ya kumsikiliza Waziri William Lukuvi, nilipigwa na butwaa. Kabla sijaendelea na makala haya, ni vema kwanza msomaji ukaona namna huyu ndugu Vuta Nkuvute alivyojaribu kueleza kiinimacho kilichofanywa na Serikali kwa uamuzi wake huu.

 

Ripoti ya Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Pinda, kuchunguza matokeo mabaya ya Kidato cha Nne ya mwaka 2012 imesomwa bungeni.


Tume hiyo iliyokuwa inaongozwa na Profesa Sifuni Mchome, iliainisha sababu za matokeo mabaya ya kidato cha nne na kupendekeza cha kufanywa.

Kati ya yaliyopendekezwa ni kusahihishwa/kupitiwa upya kwa mitihani ya watahiniwa wote wa kidato cha nne wa mwaka jana. Serikali ikaonekana kushabikia pendekezo hili la Tume ya Profesa Mchome. Ikasahau kujiuliza maswali muhimu na kujiridhisha na uchunguzi makini uliofanywa na Tume. Matokeo mabaya ya kidato cha nne kwa mwaka jana yasingeweza kuepukika. Zipo sababu ambazo ama zimefichwa, au hazikugunduliwa na Tume. Hizo ndizo zilizosababisha ubaya wa matokeo haya.


Kwanza, darasa husika halikuwa zuri tangu mwanzo. Watahiniwa wa kidato cha nne wa mwaka 2012 ni wale waliohitimu darasa la saba mwaka 2008. Wakati darasa la saba la mwaka 2007 walikuwa na wastani wa ufaulu kitaifa wa asilimia 53 ambayo ni sawa na daraja C, darasa la saba la mwaka 2008 (kidato cha nne 2012) walifaulu kwa wastani wa asilimia 45.

Niseme tu kuwa darasa hili halikuwa zuri kimasomo. Katika kuthibitisha hilo, wapo wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2012 na kushindwa mtihani ambao sasa wanajisomea Masomo ya Maarifa (QT) katika vituo mbalimbali hapa nchini kikiwemo cha Shule ya Sekondari ya Mzumbe.

Ukweli ni kwamba wanafunzi hao hawaoneshi kuwa waliwahi kusoma sekondari. Wanapelekeshwa hata na walioishia darasa la saba. Hapo mnasemaje waungwana? Pili, darasa la 2012 halikuwahi kuchujwa katika mitihani ya kidato cha pili waliyoifanya mwaka 2010.

Wote, waliofaulu na walioshindwa, waliendelea na kidato cha tatu mwaka 2011. Hawa waliopaswa kuchujwa na kurudia mitihani yao waliathiri kwa kiasi kikubwa matokeo ya mwaka 2012. Ndiyo waliohanikiza madaraja ya sifuri na la nne. Tatu, Baraza la Mitihani la Tafa lilibadili matumizi ya Alama za Maendeleo ya Mwanafunzi Shuleni (Continuous Assessment). Kabla ya mwaka 2012, CS zilitumika kama asilimia 50 ya matokeo ya mwisho.

Yaani, mtihani wa mwisho ulisahihishwa na kukokotolewa kwa asilimia 50 na hivyo kufanya asilimia 100 ukichanganywa na CS. Kwa maana hiyo, mwanafunzi ambaye katika somo fulani alipata CS ya 21 na kuendelea, alikuwa na uhakika wa alama D na kuendelea katika matokeo yake ya mwisho. Hii, yasemwa na wahusika wa NECTA, ilifanya shule nyingi kuwa ‘zinapika’ CS za wanafunzi wao na hivyo kunogesha matokeo ya wanafunzi hao na shule zao kwa ujumla. Mwaka huu, CS zote zilichukuliwa kama daraja F (yaani chini ya 21), na hivyo mwanafunzi kubaki na mtihani wa mwisho tu kama mkombozi wake.

Hii nayo ikaleta matokeo haya mapya ya kidato cha nne mwaka 2012. Hoja ya kuwa zilitumika alama mpya kupata madaraja A, B, C, D na F, haina mashiko sana. Hii ni kwa kuwa hata pale zilipotumika alama za zamani matokeo hayakuwa mazuri. Taarifa rasmi kutoka kwa wasahihishaji zinatoa mfano wa somo la Kiingereza ambalo baada ya kusahihishwa Tanzania nzima, ni mwanafunzi mmoja tu wa Shule ya Sekondari ya Ilboru aliyepata alama za daraja A.

Amini nawaambia, hii ya kusahihisha upya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012 ni janja ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kutaka kuwaridhisha wamiliki wa shule binafsi ambao wamemwaga lawama za kutosha serikalini, kuwa watakosa ‘wateja’ kwenye shule zao kutokana na matokeo haya mabaya mno.

 

Pia ni kutaka kurekebisha makosa ya kimawasiliano kati ya Wizara ya Elimu, Taasisi ya Elimu na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA). Kukosekana huko kwa mawasiliano na maelewano ndiko kulikosababisha kutungwa mitihani kinyume na ‘mitaala’, kutochujwa kwa wanafunzi walioshindwa kidato cha pili, kutotumika kwa CS kama ilivyozoeleka na kadhalika. Kiujumla, Waziri wa Elimu, Katibu Mkuu wa NECTA na Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania hawawezi kukwepa mzigo huu wa fedheha kwa Taifa. Huo ndiyo ukweli.

 

Ukisoma maneno ya ndugu Vuta Nkuvute, unaona wapi kwenye tatizo. Tena basi, inawezekana miongoni mwetu tupo tuliosahau kwamba uamuzi wa kufuta mitihani ya kidato cha pili, ulikuwa ni uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete! Tangu mapema kabisa, Rais Kikwete alionesha kutofurahishwa na uwepo wa mitihani hiyo.  Alichokiangalia yeye ni kile kitendo cha mtoto kukwaza kuendelea endapo anafeli mitihani, na wala hakutaka kutambua faida nzuri za mitihani hiyo kuwa chachu kwa watoto kujisomea kwa bidii. Kwa maneno mengine, matokeo mabaya ya mwaka jana ni matunda ya uamuzi wa mtu mmoja!

 

Uamuzi huo haukuwa na tofauti kubwa ukilinganishwa na ule wa aliyekuwa Waziri wa Elimu  wa wakati huo, James Mungai, wa kufutwa kwa mashindano shuleni, na kufutwa kwa baadhi ya masomo. Athari za alichokiasisi Mungai, bado tunachechemea nacho. Mambo makubwa kama haya, hasa yanayohusu mustakabali wa nchi, ni lazima yaamuriwe na wengi.

 

Kurejea usahihishaji mitihani ya kidato cha nne ya mwaka 2012 si mwarobaini wa kumaliza tatizo la kushuka kwa kiwango cha elimu katika Taifa letu. Wala kuwatimua viongozi wa NECTA au Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, si suluhu ya kuwa na matokeo mazuri kwa siku zijazo, kama hali ndiyo hii hii. Kweli, zinaweza kuwapo dosari za hapa na pale kwa watendaji, lakini kwa ujumla wake tatizo la kiwango cha elimu nchini mwetu linachangiwa na mambo mengi mno, tena yaliyo wazi. Hayahitaji kuundiwa tume wala kamati!

 

Juzi wakati nikienda Dodoma, tuliwapa lifti wanafunzi wanne kutoka Ihumwa hadi Dodoma mjini. Umbali wa Ihumwa-Dodoma ni zaidi ya kilomita 20. Wanafunzi hawa wanalazimika kila siku ya masomo kusafiri umbali wa kilometa zaidi ya 40 kwenda na kutoka shule. Hawa wanalala usingizi wa mang’amung’au maana hawajui wakifika barabarani watamkuta dereva gani mwenye huruma atakayewapa lifti.

 

Hawa wanafunzi wanapoona muda wa kurejea nyumbani unawadia, mawazo yanahama kutoka darasani au kwa yale waliyofundishwa siku hiyo, yanajielekeza kujiuliza ni msamaria mwema gani atawawezesha kurejea nyumbani, kilomita zaidi ya 20! Kwa hali kama hiyo, tusitarajie muujiza wa watoto wengi kufanya vizuri katika masomo.

 

Kwa watoto wa kike ndiyo kabisaaa! Naishi Kwembe. Kuna wanafunzi wanaosafiri kutoka Temeke hadi Kwembe. Wanaposhuka kwenye mabasi (ambayo hupanda kwa hisani), wanalazimika kusafiri, ama kwa miguu au kwa pikipiki hadi shuleni – umbali wa kilomita zaidi ya sita! Wengi wanatembea, maana hawana uwezo kifedha. Shule ya Sekondari Kwembe ni miongoni mwa shule ambazo wanafunzi wengi wa kike wanaacha masomo kutokana na mimba! Ndani ya lindi hili la mateso, lazima idadi ya wanaofeli iwe kubwa.

 

Shule zetu, kuanzia msingi hadi sekondari, hazina walimu wa kutosha, hazina vitabu vya ziada na kiada, walimu wanaishi mbali mno na shule, mishahara ya walimu ni duni. Shule hazina maabara kiasi kwamba tumefuta mitihani ya vitendo kwa masomo kama fizikia.

 

Wakati mataifa mengine walimu ni wale wanafunzi wanaofaulu madaraja ya kwanza na pili, kwa Tanzania walimu wengi ni wale waliopata daraja la nne! Mwanafunzi anapokosa kuendelea na masomo, tumezoea tunauliza, “hata ualimu amekosa?”

 

Sasa tufanye nini? Kwanza tukiri kuwa tuna matatizo makubwa katika elimu. Kujua na kukiri tatizo ni hatua murua ya kuelekea kulitatua. Kurejea usahihishaji ni kujipa matumaini yasiyokuwa na tija. Ni kukwepa tatizo muhimu kwa sababu nyepesi. Tujenge mabweni ya kutosha. Tuwekeze katika kununua vitabu. Tanzania ya pili katika Afrika kuwa na misitu – kukosa madawati shuleni si tu ni aibu, bali ni ujinga!

 

Walimu walipwe vizuri. Tupige marufuku twisheni. Kila mzazi atambue kuwa pamoja na kuzaa, ana wajibu wa kuzaa wale anaoweza kuwasomesha! Nimalize kwa kumpongeza ndugu Vuta Nkuvute! Hakika kilichofanywa na Serikali ni kama mbuni kufukia kichwa ardhini, ilhali kiwiliwili chote kakiacha nje. Hii ni kama malaria. Huwezi kupona malaria kwa kunywa panadol tu! Tukubali kunywa dawa zinazoponya, hata kama ni chungu.

Please follow and like us:
Pin Share