Uharibifu misitu: Janga linaloiangamiza Tanzania-2

Je, tufanye nini kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa? Kwanza, walinzi wa misitu wakiwapo hasa katika misitu iliyohifadhiwa kisheria, wataweza kuzuia watu wasiingie na kufanya chochote.

Pili, vijiji vijengewe uwezo wa kusimamia misitu inayopatikana katika eneo la ardhi ya kijiji husika. Tatu, utekelezaji wa Sheria ya Misitu uliolegalega na kuongeza nguvu katika ufuatiliaji na usimamizi, kutasaidia kupunguza rushwa na kuhakikisha wafanyabiashara ya mazao ya misitu wanafuata kanuni na taratibu zilizopo. Tusibweteke kwani hali ya mazingira nchini inazidi kuwa mbaya siku hadi siku.

 

Hebu fikiria na uangazie hali ya mazingira ilivyokuwa miaka ya1970, 1980 na 1990 na hali ilivo sana. Mambo yamebadilika sana na hali ya maisha inakuwa ngumu kila kukicha.

 

Upatikanaji wa mvua kwa nyakati hizi sivyo ilivyokuwa miaka 30 au 40 iliyopita. Miaka hiyo wakulima walikuwa na uhakika wa majira na upatikanaji wa mvua na hivyo walijiandaa ipasavyo kuliko ilivyo majira ya sasa.

 

Sehemu nilikozaliwa, wakulima walikuwa na uhakika kuwa ifikapo Septemba (kila mwaka) mvua zinaanza kunyesha, hivyo kuhakikisha kuwa tarehe Mosi Septemba mashamba yameandaliwa tayari kwa kuotesha mahindi na maharage.

 

Leo hii wakulima wa kwetu wilayani Muleba hawana uhakika wa mvua, maana wakati mwingine inafika hadi Desemba bado mvua ni za kusuasua tu. Hali ya mazingira imebadilika sana, kwa mfano ukame umeongezeka, vijito na mito iliyokuwa na maji mengi nikiwa mdogo, sasa imekauka na maisha yanazidi kuwa magumu sana hata migomba ambayo ni tegemeo kubwa kwa chakula na kipato, sasa imezongwa na changamoto nyingi ikiwamo ya ugonjwa usioeleweka unaojulikana kama  “mnyauko” unaosababisha mgomba ufe hata ukiwa umebeba mkungu wa ndizi. Unaharibika na haufai kupikwa wala kuuzwa. Yote haya ni matokeo ya uharibifu wa mazingira kiasi cha kuhatarisha maisha yetu.

 

Wakati wa mafunzo yangu kwa taaluma ya misitu (Julai 1974 hadi Mei 1977), nilipata fursa ya kutembelea maeneo kadhaa katika nchi yetu yakiwamo ya mikoa ya Tanga (sehemu za Lushoto hasa maeneo ya Mazumbai, Shume na Mlalo); Kilimanjaro (sehemu za milima ya Same hasa maeneo ya msitu wa Shengena/Chome na maeneo ya Mwanga milimani Ugweno na Usangi. Vilevile nilitembelea mara kwa mara misitu inayozunguka Mlima Kilimanjaro na wakati huo msitu ukifahamika kama Kilimanjaro Forest Reserve na sasa ni sehemu ya Kilimanjaro National Park (KINAPA).

 

Kwa enzi hizo – miaka ya 1970 – hali ya misitu na mazingira yanayouzunguka Mlima Kilimanjaro ilikuwa ya kuridhisha sana. Theluji kwenye kilele cha mlima ilionekana kuwa nyingi kuliko hali ya sasa ambako imepungua sana. Kulikuwa na vijito na mito mingi iliyokuwa na maji mengi sana iliyotiririka kutoka katika misitu inayouzunguka mlima na sasa mingi haina maji ya kutosha. Mfano, Mto Kikafu na mingine imekauka.

 

Zaidi ya hapo nilifika sehemu za Longai karibu na mpaka na Kenya, pia sehemu za Kilimanjaro Magharibi na maeneo ya kusini hadi Kahe. Vile vile kutembelea Mkoa wa Arusha na maeneo ya Mkoa wa Manyara zikiwamo sehemu za Ngorongoro na Serengeti.

 

Itendelea

Please follow and like us:
Pin Share