Kiwanda kidogo cha kuchenjua marudio ya madini ya dhahabu, kilichojengwa kwenye makazi ya watu katika Mtaa wa Kagera mjini Geita, mali ya Askofu wa Kanisa la Habari Njema la Geita, Triphone John, kimesababisha madhara yakiwamo ya kufa kwa mifugo.

Uchunguzi unaonesha kuwa kiwanda hicho kinatoa sumu aina ya synide ambayo inatumika kwenye shughuli hizo. Sumu hiyo imekuwa ikitiririka kuelekea kwenye makazi ya watu. Ng’ombe watano waliokunywa maji hayo, wamekufa.

 

Wakazi wa mtaa huo wamesema waliacha kutumia maji ya bomba tangu Aprili, mwaka huu, na kulazimika kwenda umbali mrefu kufuata huduma hiyo kutokana na kile kinachodaiwa sumu hiyo imepenya hadi kwenye vyanzo vya maji.

 

Ng’ombe waliokufa Aprili 22, mwaka huu, ni mali ya Eliangikaya Mshana. Wakazi wa mtaa huo wameomba uchunguzi ufanywe juu ya hatari hiyo.

 

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kagera, Said Mahuma, amesema wakati linatokea jambo hilo alikuwa safarini. Amekiri kwamba wananchi wameacha kutumia maji kutokana na hofu ya sumu.

 

Mmoja wa wakazi wa mtaa huo, Paulina Alex, mbali na kuwatupia lawama baadhi ya waandishi wa habari waliofika eneo la tukio na baadaye kushindwa kutoa taarifa hizo, anasema hawatumii maji ya bomba kwa hofu ya sumu. Pia anasema wamezuia watoto kucheza kwenye maji na tope kwa kuwa maji hayo hatari yanatiririka, hasa wakati wa mvua.

 

“Tunashangaa waandishi wa habari, tukio limetokea nasi tukahangaika kuwatafuta na wakafika na kutuhoji kero zetu kuhusiana na kiwanda hiki, wakawahoji viongozi wa Serikali waliokuwa eneo la tukio na Askofu mwenyewe, mwisho wa siku hatukuona habari zikiandikwa au kutangazwa.

 

“Mnaisaliti hata jamii…ni bora kama walikuwa wanahitaji chochote wangesema na tulikuwa tayari kuchanga ilimradi habari itoke na Serikali isikie kilio chetu…tulianza kuwa na shaka baada ya kuwaona waandishi wanapanda kwenye gari la…na kuondoka pamoja. Tukajua hapa kuna kitu,” amesema.

 

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka mjini Geita (GEUWASA), Clemence Chagu, anasema mamlaka hiyo imesitisha utoaji wa huduma ya maji kwa wakazi hao, kwa hofu ya kuleta madhara kwa binadamu na kwamba tayari mabomba yamekatwa.

 

Anasema mpango wa kutandaza mfumo mpya wa mabomba unafanyika ili kurejesha huduma ya maji kwa wakazi wa mtaa huo, baada ya kutambua wateja walioathirika na tatizo hilo zikiwamo ofisi za Shirika la Plan International.

 

Daktari wa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Dk. Thobias Kiputa, amethibitisha kufa kwa ng’ombe kutokana na maji yanayodaiwa kuwa na sumu. Amepeleka sampuli kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

 

“Hadi sasa haijajulikana sumu iliyosababisha ng’ombe hao kufa, mimi kwa nafasi yangu kama daktari wa mifugo nilifika eneo la tukio nikachukua sampuli na tayari zimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali,” amesema Dk. Kiputa.

 

Kwa upande wake, Askofu anasema yupo na anaendesha shughuli zake kihalali. Anasema kufa kwa ng’ombe hao hakuhusiani na kuwapo mtambo wake wa kuchenjua dhahabu.

 

“Hivi wewe ni nani? Tukio limetokea siku nyingi sana, kwanini wewe uendelee kulifuatilia wakati tayari waandishi wengine walikuja, umeona habari zimetoka? Sitaki kabisa tena kunipigia simu kuhoji kwamba mimi nimeua hao ng’ombe,” amesema Askofu John.

 

Ofisa Madini Mkazi wa Wilaya ya Geita, Juma Sementa, alikiri Askofu huyo kumiliki mitambo ya kuchenjulia madini kwenye makazi ya watu na kwamba leseni yake inamruhusu kuendesha shughuli hizo katika maeneo hayo kwa usimamizi wa hali ya juu.

 

“Hakuna link iliyotumika kupenyesha ile sumu. Tumefuatilia ukweli wa jambo hilo, hakuna sumu iliyopenya” amesema Sementa.

 

Anasema wafanyabiashara wa dhahabu wameruhusiwa kuendesha shughuli hizo kwenye makazi yao kutokana na maeneo yaliyotengwa kwa ajili hiyo kutokuwa na nishati ya umeme.

 

Naye, Ofisa Mazingira Wilaya ya Geita, Hellen Eustace, akizungumzia suala la Askofu huyo kumiliki mitambo ya kuchenjulia madini katika makazi ya watu, anasema tatizo hilo linatokana na majungu ya watu, na kwamba sumu inayodaiwa kuharibu mfumo wa maji haihusiani na shughuli hizo.

 

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Omari Mangochie, mbali na kukiri kuwapo kwa kiwanda hicho kwenye makazi ya watu, anasema tayari Serikali imewaagiza maafisa ardhi kufanya uchunguzi kubaini kama viwanja hivyo vilibadilishwa matumizi na hivyo kujengwa viwanda.

 

Sumu ya Synide ambayo hutumika kuchenjulia madini ya dhahabu, inatajwa kama moja ya sumu hatari kwa afya ya binadamu na viumbe hao wengine.

Please follow and like us:
Pin Share