Na Mwandishi Wetu, Jamhuri Media, Arusha

Taasisi ya Friedkin Conservation Fund(FCF) imepanga kutumia kiasi cha sh 1.2 bilioni ili kugharamia miradi ya maendeleo ya jamii, ikiwepo ya Elimu na Afya ambayo haikinzani na uhifadhi wa wanyamapori na Misitu, wilayani Meatu mkoani Simiyu.

Taasisi ya Friedkin Conservation Fund ni Taasisi tanzu ya kampuni ya Mwiba holding Ltd ambayo inafanya shughuli za Utalii katika eneo na Jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Makao wilayani Meatu, eneo la ranchi ya wanyamapori ya Mwiba na maeneo mengine kadhaa.

Meneja miradi wa Taasisi ya Friedkin Conservation Fund(FCF) Aurelia Mtui akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufungaji wa mikanda ya kielekroniki (collar) kwa Tembo 10 katika eneo la Ranchi ya Mwiba na makao WMA zoezi lililogharimu Sh 232 milioni ili kutatua migogoro na jamii, alisema taasisi hiyo imeongeza fedha za kusaidia Jamii.

Meneja wa Shirika la Friedkin Conservation Fund (FCF) Tanzania Aurelia Mtui.

Mtui alisema Taasisi hiyo mwaka huu imetenga dola 525,000 ambazo ni zaidi ya Sh1.2 bilioni ili kuchangia shughuli za maendeleo na miradi ya kijamii katika vijiji 29 ambavyo taasisi hiyo inafanyakazi.

Mtui alisema fedha hizo zilizotengwa mwaka 2023/24 zimeongezeka kwani mwaka 2021/22 zilikuwa zimetengwa na kutumika kiasi cha dola 430,000 ambazo ni zaidi ya Tsh. 989 milioni.

“Fedha za mwaka huu tunatarajia zitatumika katika ujenzi na ukarabati wa shule, vyumba za walimu, vituo vya afya na shughuli za uwezeshaji wananchi kuichumi, ikiwepo kusaidia ufugaji wa nyuki na uwezeshaji kwa wanawake” alisema

Mtui alisema FCF wameanzisha mradi wa usafiri wa baiskeli 200 shule ya sekondari Paji na kuanzia Julai mwaka huu kutakuwa na mradi wa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule ya msingi Makao.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Meatu Anthony Philipo akizungumzia mchango wa FCF na Mwiba Holding Ltd katika wilaya hiyo, alisema ni mkubwa katika kusaidia jamii, ikiwepo kudhibiti tembo kuharibu mali za wananchi.

Philipo alisema katika wilaya hiyo, kulikuwa na migogoro baina ya Tembo na wananchi na sasa inakwenda kupatiwa ufumbuzi kutokana na tembo kufungwa mikanda ya kuwadhibiti kuingia katika mashamba na makazi ya watu.

Afisa Wanyamapori wilaya ya Meatu Deusdedit Martin amesema changamoto ya Tembo kuingia katika makazi ya wilaya hiyo ni kubwa lakini pia halmashauri imekuwa ikitoa elimu kwa askari wa wanyamapori wa vijiji jinsi ya kudhibiti makundi ya tembo katika maeneo ya makazi na mashamba ya watu.

By Jamhuri