Kikwete kwa hili lazima nikupongeze


Jakaya Mrisho Kikwete (JK), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Kuna taarifa kwamba umewaongezea muda wa kazi viongozi wa ngazi ya juu katika vyombo vya ulinzi na usalama waliopaswa kustaafu kipindi hiki.

Kama ni kweli umefanya hivyo, umefanya uamuzi mzuri. Ninasisitiza kuwa umefanya uamuzi makini kumtaka hata Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, asistaafu kwa sasa bali aendelee kushughulikia mustakabali wa usalama nchini, angalau hadi baada ya Uchaguzi Mkuu, mwaka 2015.

Pengine unashangaa kwanini ninakupongeza, lakini jambo jema kuwataka wakuu wa ulinzi na usalama akiwamo Mkuu wa Majeshi, Jenerali Devis Mwamunyange, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Rashid Othman na Naibu Mkurugenzi wa Idara hiyo, Jack Zoka.

JK pokea pongezi hizi maana umeona mbali; umesoma alama za nyakati. Umefanya vizuri kukataa IGP Mwema asistaafu maana usalama wa raia na mali zao sio kitu cha mchezo, na ndiyo maana watu wanasema, “Usalama Wetu Kwanza.”

Nimjuavyo IGP Mwema anayekutana na wananchi moja kwa moja kila siku pamoja na changamoto alizopitia kikazi, alitamani kuona muda wake wa utumishi wake unaisha salama, Disemba 31, 2013.

Ninajua kama ni kweli, taarifa yako ya kukataa Mwema na wenzake wasistaafu, zimemshitua, lakini ninavyomjua kwa uadilifu na utiifu wake, itakuwa imempasa kusema, “Ndimi mtumishi wa bwana nitende ulivyonena.”

Kikwete, kama kweli umekataa, basi umefanya vizuri maana Tanzania inaelekea katika vipindi vigumu vya upigaji kura za maoni kuhusu Katiba Mpya, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (mwaka 2014) na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani (mwaka 2015).

Ninakupongeza JK kwa sababu ninajua si busara kipindi kama hiki cha kuelekea katika chaguzi hizo vyombo vya ulinzi na usalama viongozwe na “wanafunzi au wageni” ambao hawajazoea mikasa mizito inayohitaji uamuzi mgumu wenye maslahi kwa umma. Mwema ana uwezo na uzoefu mkubwa wa kuendelea kuimarisha ulinzi wa usalama na mali zao kuziwezesha chaguzi zijazo kufanyika salama salimini kwa manufaa ya umma.

Sisemi kwamba bila IGP Mwema Tanzania haiwezi kitu, la hasha. Wapo maofisa wengi wa Jeshi la Polisi wanaoweza kufanya vizuri kama yeye, lakini matukio nyeti ya kitaifa yajayo yanahitaji dereva mzoefu anayewajua wazuri na wabaya wake kikazi; kuanzia ngazi ya chini mpaka ngazi ya juu, maana kumjua adui ni nusu ya ushindi.

Huenda IGP Mwema ananiangalia kwa ‘jicho baya’ kutokana na haya ninayoyasema, lakini nashukuru hanijui kwa sura, hivyo sioni shida bali nakupongeza JK kwa kumkatalia na wenzake wasistaafu hadi wakamilishe juhudi zao za kulikarabati Jeshi la Polisi.

Juhudi hizo ni pamoja na dhana ya Polisi Shirikishi Jamii, Utii wa Sheria Bila Shuruti na kampeni ya “Familia Yetu Haina Mhalifu” iliyozinduliwa hivi karibuni. Isingekuwa busara kampeni hiyo kuishia njiani kama angeingia IGP mwingine na mipango yake mipya.

Kimsingi, kuwataka wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea na majukumu yao hata baada ya kuwa wamefikia umri wa kustaafu, kunawaonesha hata wengine kwamba wewe Rais na Amiri Jeshi Mkuu una moyo wa shukrani wa kutambua kazi bora ya mtumishi na ndiyo maana unapenda mema ambayo Mwema ameanzisha kwa wema, basi ayakamilishe vema na kama “aliyakoroga, basi ayanywe mwenyewe.”

Wengi tunapenda kuona IGP Mwema aendelee na juhudi alizokuwa nazo wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopita alipoonesha ubunifu na busara nyingi kukusanya vikundi mbalimbali vikiwamo vya kidini, kisiasa na kijamii kuvielewesha mbinu na umuhimu wa kuendeleza amani na utulivu hapa nchini kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa kitaifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, amenukuliwa na chombo cha habari hapa nchini akikiri wema wa IGP Mwema akisisitiza, “Ni mwepesi wa kushauri, si mtu wa kutumia ubabe, Mwema ni mtu wa kutumia busara.”

Amiri Jeshi Mkuu, ukitaka kujua umuhimu wa wewe kumuongezea Mwema muda wa kubaki kazini, jiulize tu, ni IGP gani aliyeingia na kuwaweka hata askari polisi katika hadhi ya ubinadamu kiasi cha kuwajengea makazi bora na kuwatoa katika nyumba zilizotenganisha familia mbili tofauti kwa kuta za makaratasi ya nailoni, maboksi au upande wa kanga?

Jiulize, ni IGP gani aliyeliendesha Jeshi la Polisi Tanzania kwa weledi na usasa na hivyo kuzaa matunda bora kwa taifa kama ilivyofanya IGP Mwema. IGP Mwema amekuwa mstari wa mbele kusisitiza haki, uwajibikaji na uelewano baina ya polisi na raia. Ndiyo maana hata nyumba za ibada sasa zina kamati za ulinzi na usalama ambazo zimesaidia “kusafisha hali ya hewa”.

 

Lakini pia, ni katika uongozi wa IGP Mwema namba za simu za viongozi wa Jeshi la Polisi kuanzia yeye mwenyewe, Makamanda wa Polisi wa Mikoa (RPCs) na Wakuu wa Polisi wa Wilaya (OCDs) zimetangazwa wazi na raia wamehamasika kuzitumia kufichua uhalifu na wahalifu.

Mkuu wa Nchi, pengine waovu wakiwamo maofisa wachache wa Jeshi la Polisi walioshindwa kuendeleza uovu au kushirikiana na wahalifu kutokana na kibano cha IGP Mwema, walikuwa wameanza maandalizi ya kusherehekea na kufanya karamu ya kula, kucheza na kudundika bila wasiwasi wakiamini muda wa kustaafu kwa kiongozi huyo umetimia na hivyo, milango ya uhalifu wao imefunguka na kizuizi cha kutenda uhalifu wao kimeondoka. Bila shaka sasa watakuwa wamepigwa butwaa!

Wanoweza kufurahia kustaafu kwa IGP Mwema katika utumishi, ndio wanaopandikiza sumu kwa umma ili kuchafua utumishi wake katika Jeshi la Polisi. Hao hawajui kwamba inapotokea kuchelewa kubaini uhalifu au kuwabaini wahalifu na kuwakamata, uzembe hauelekezwi kwa polisi pekee bali hata jamii yenyewe kwa kutoshiriki kikamilifu kuukataa na kuupiga vita uhalifu kwa kuwafichua wahalifu hivyo.

Unajua, Polisi ni chombo cha usalama wa raia na mali zao kinachoendeshwa kitaaluma kikiwa na miongozo, miiko na maadili. Ni taaluma ya sayansi ya kuzuia uhalifu, kupeleleza, kukamata na kuwafikisha watuhumiwa wa uhalifu mahakamani. Waliodhibitiwa na Mwema kufanya uhalifu au kushirikiana na wahalifu wangetaka nafasi hiyo ichukuliwa haraka mtu mwingine wanayemtaka na kumpigia debe kwa kumsukuma huyo aliyetenda vema aondoke wakidhani wanamkomoa, kumbe wanamtafutia analolitaka zaidi kuliko wao.

Hao, si ajabu wameanza kupangiana safu mpya za uongozi ndani ya polisi, wamesahau kuwa Jeshi la Polisi haliwezi kuzaa wahalifu bali jamii bila uhalifu. Na kwa ukweli usiopingika, Jeshi la Polisi halifugi wahalifu bali wahalifu hufugwa na jamii wenyewe kwa kuwahifadhi na kuwatunzia siri katika familia, ndiyo maana hawakamatwi japo wanafanya uhalifu na kuiangamiza jamii.

Said Mwema, ofisa mwenye cheo cha zaidi ya Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), utumishi wake umekuwa imara katika Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na kutokubali jeshi hilo kushinikizwa kukamata watu bila kuthibitisha kuwa anayekamatwa ni mlengwa anayetuhumiwa.

Utaratibu huo umesaidia kuepusha ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kuonea, kubambika kesi na kukamata kwa uonevu. Juhudi za IGP Mwema zikiwamo za kuanzisha kampeni ya ‘Familia Yetu Haina Mhalifu’, zinazolenga kuondoa mifumo mibovu iliyokuwapo katika jamii na kuiweka mifumo bora ya malezi ili kupata taifa lenye watu wema wanaouchukia uhalifu kwa dhati, bila shaka zinazidi kuwaumiza wahalifu na hivyo, kuwafanya washangilie kuondoka kwake maana amekuwa kisiki kwao!

1171 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!