*Baraza la Madiwani Arusha, Mkurugenzi, Mbunge kila mtu na lake

*Doita: Mbunge au diwani kutoa maelekezo nje ya vikao ni uchochezi

*RC, TCCIA wasema kazi inaendelea, wakagua maeneo mapya ya wamachinga

ARUSHA

Na Mwandishi Wetu

Utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kuwapangia maeneo mapya ya kufanyia biashara wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga linaonekana kuwa gumu jijini Arusha.

Rais amewaagiza watendaji wa serikali yake nchi nzima kuhakikisha wamachinga wanaondoka katika maeneo ya pembezoni mwa barabara kuu, juu ya mitaro na mbele ya ofisi na taasisi za serikali bila kutumia nguvu.

Ikiwa ni zaidi ya mwezi sasa tangu agizo hilo lilipotolewa, watendaji katika Halmashauri ya Jiji la Arusha bado wanasuasua katika utekelezaji wake, hali inayodaiwa kusababishwa na mgogoro mkubwa miongoni mwa viongozi.

Hadi Ijumaa wiki iliyopita, biashara ndogondogo zilikuwa zikiendelea katika maeneo yote ya katikati ya jiji, ingawa kulikuwapo juhudi ‘za kidiplomasia’ zinazofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella.

Mgogoro wa uongozi

JAMHURI limeambiwa kwamba mgogoro kati ya Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, kwa upande mmoja dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji, Dk. John Pima na Meya wa Jiji, Maximilian Iranghe, kwa upande mwingine ndicho chanzo cha kusuasua kwa uhamishaji wa wamachinga kwa wakati.

“Huu mgogoro wala si wa siri! Upo wazi na hata mtoto mdogo akiwa makini anauona. Hawa watu hawasalimiani, iwe kwenye mikutano ya ndani au ile ya hadhara.

“Na wakipata nafasi ya kuongea kwenye mikutano ya hadhara, wanapigana vijembe, vingine vya wazi kabisa,” anasema mkazi mmoja wa Arusha.

Wiki chache zilizopita Mbunge wa Arusha Mjini, Gambo, ameonekana kwenye mitandao ya kijamii akitoa kauli zinazoashiria kupingana na msimamo wa viongozi wengine jijini humo.

Gambo anasema kwenye mitandao hiyo kwamba yeye atasimama upande wa wamachinga.

“Mimi nimechaguliwa na watu, kwa hiyo nitakuwa upande wao,” anasema Gambo katika mikutano yake kadhaa na makundi mbalimbali ya wamachinga.

Gambo anaamini kuwa wamachinga wanastahili kuwapo maeneo yenye watu wengi na si pembezoni mwa miji.

Anasema: “Wakati Mongella akiwa mkuu wa wilaya hapa ndiye aliyetenga eneo la Samunge kwa ajili ya wamachinga, sasa iweje leo wataalamu walewale wanakuja na mpango wa kuwatoza ushuru?

“Samunge si soko, ni eneo la wamachinga na wanaosema vitambulisho vya wamachinga vimezikwa Chato hao ni waongo na wachonganishi wanaotaka kuwachonganisha wananchi na madiwani na mbunge wao.”

Hata wakati wa ziara ya Rais Samia mkoani Arusha, ingawa hakusema moja kwa moja, Gambo alionekana kuwa na msimamo tofauti na wenzake katika namna ya kuwapanga wamachinga.

Akizungumzia hali hiyo, Diwani wa Ngarenaro, Isaya Doita, anakiri kuwapo kwa maelewano duni kati ya mbunge na Baraza la Madiwani.

“Kwanza ieleweke kwamba mpango wa kulipanga Jiji la Arusha kwa kuwapa wamachinga maeneo ya kufanyaa biashara ulikuwapo hata kabla ya agizo la Rais ambaye pia ni mwenyekiti wetu. Hili agizo limesaidia kutupa msukumo mpya.

“Bahati mbaya sana sasa mtazamo wa mbunge ni tofauti na maelekezo yanayotolewa na Baraza la Madiwani. Yeye analeta ‘conditions’ (masharti) ngumu kabisa,” anasema Doita. 

Anasema wakati Baraza la Madiwani likipanga kuwapeleka wamachinga maeneo kama Mbauda, Machame Luxury, Kilombero No. 68 na Samunge; Gambo hataki.

“Kwa namna hali ilivyo, wala sioni tofauti kati ya ile Arusha nyakati za Chadema ya Lema (Godbless Lema, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya Chadema) na hii ya sasa,” anasema Doita, kuonyesha mkwamo wa maendeleo uliopo sasa sawa na ilivyokuwa awali. 

Doita anaendelea: “Tatizo ni kwamba watu hawajikubali! Hawajui kuwa ukiwa mbunge au diwani haupaswi kutoa maelekezo, bali ni kushauri na kufanya ‘lobbying’ (ushawishi) majukwaani.

“Kwa mbunge au diwani kutoa maelekezo nje ya vikao huo ni uchochezi.”

Doita, diwani mwenye ushawishi mkubwa katika Kata ya Ngarenaro, anashauri Chama Cha Mapinduzi (CCM) Makao Makuu kuingilia kati na kumaliza mgogoro uliopo kabla ya chama wilaya na Mkoa wa Arusha hakijasambaratika.

Anamsihi Mkuu wa Mkoa, Mongella, kuwaweka mezani mbunge, mkurugenzi na meya na kukemea matendo mabaya, kwa kuwa yeye ndiye kiongozi mkuu.

“Kuficha tatizo wakati ni wazi lipo, ni makosa. Kulifahamu tatizo unakuwa umelipatia utatuzi kwa asilimia 75. Sasa hapa kuna tatizo. Maagizo ya Mwenyekiti Taifa wa chama, Mama Samia, yanakwama. Tutafika kweli?

“Kuna tatizo jamani! Kuna ubinafsi ambao sijawahi kuushuhudia popote! Watu wanashindania hata maeneo ambayo hakuna haja ya kushindana. Mimi ninaona hatari mwaka 2025 jimbo litapotea pamoja na kata kadhaa,” anasema.

Wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa Arusha waliamini baada ya kata nyingi kuchukuliwa na CCM, maendeleo yangefanyika bila kuwa na upinzani kwenye Baraza la Madiwani, lakini sasa hali ni tofauti.

Mongella, TCCIA: Kazi inaendelea

Hata hivyo, Jumamosi iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mongella, amekagua maeneo yanayoandaliwa kwa ajili ya wafanyabiashara hao.

Akizungumza na JAMHURI, Mongella anapuuza dhana ya kuwapo kwa mgogoro wa kiuongozi jijini Arusha, akisema viongozi wanaendelea na kazi na kwamba yeye anatekeleza maagizo ya Rais Samia kwa umakini mkubwa.

“Tumepanga kuwahamishia wamachinga katika maeneo matano. Yapo ya katikati ya jiji na mengine ni ya pembezoni ili makundi yote yanufaike na mpango huu,” anasema.

Ukaguzi huo wa RC ulilenga kuhakikisha kuwa huduma muhimu zimekamilika, tayari kwa utaratibu wa kuhamia uliopangwa kuanza kutekelezwa jana uanze.

Anasema mipango yote imefanyika kwa kuwashirikisha viongozi wa wamachinga na kila kitu kinakwenda sawasawa.

Maeneo watakayohamia wamachinga ni Soko la Kilombero, Machame lililoko makao mapya, Ulezi Mianzini, Kwa Morombo, Samunge na Unga Ltd.

Akizungumzia suala la wamachinga, Ofisa Maendeleo ya Biashara na Kilimo wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Arusha, Charles Makoi, ameusifu utaratibu uliofanyika katika Jiji la Arusha, akisema utawarahisishia kuwatafuta wafanyabiashara na kujua matatizo yao.

“Hali hii itafanya wafanyabiashara hawa kutambulika na kukopesheka na mabenki. Walipokuwa wametawanyika hakuna chombo ambacho kingekubali kuwakopesha, hawakuwa kwenye maeneo rasmi,” anasema Makoi.

Anasema TCCIA wapo bega kwa bega katika kuwawezesha wafanyabiashara na wakulima kwa kuwapa mafunzo na mikopo hivyo waweze kunufaika wao, familia zao na taifa kwa ujumla.

Anasema awali haikuwa rahisi kuwapa mafunzo na kuwajengea uwezo, matokeo yake wakikopa kwenye vikundi, mmoja akishindwa kurejesha huwapa gharama wengine.

Kwa upande mwingine, Jumamosi hiyo hiyo, Meya wa Jiji la Arusha, Iranghe, naye alikuwa kazini akikagua maeneo mengine mbali na yale aliyokuwa akiyakagua Mongella.

Akizungumza na JAMHURI, Iranghe anasema tayari maeneo yaliyotengwa yapo tayari kwa matumizi.

Kuhusu kuwapo mgogoro kati ya Baraza la Madiwani, Mkurugenzi wa Jiji na mbunge, Meya wa Jiji la Arusha anasema kwa mshangao: 

“Mgogoro! Sidhani kama upo hata kama mbunge hatupo naye kwenye ziara za leo (yake na ile ya RC). Nitamuuliza mkurugenzi nione kama kuna kitu kama hicho.”

Taarifa za ndani

Taarifa ambazo JAMHURI bado halijazithibitisha zinasema kwamba katika kutekeleza agizo la Rais Samia, CCM imetoa wiki mbili kwa watendaji kuhakikisha wamachinga wanapangwa upya.

By Jamhuri