Gazeti la JAMHURI linalochapishwa na kusambazwa siku ya Jumanne kila wiki nchini na nchi jirani Afrika Mashariki, limeongoza dhidi ya vyombo vingine vyote vya habari Tanzania Bara na Zanzibar vilivyohusishwa kwenye utafiti wa ubora wa maudhui kwa vyombo vya habari nchini kwa mwaka 2022.

Utafiti wa Mradi wa Ubora wa Vyombo vya Habari Tanzania ‘Yearbook Media Quality in Tanzania’ uliofanywa na Watafiti wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (UDSM) umeweka bayana kuwa Gazeti hili la JAMHURI limevibwaga vyombo vingine vya habari 29 kuanzia baadhi ya magazeti mengine maarufu ya kila siku, televisheni kubwa nchini, redio mbalimbali na mitandao mashuhuri ya kijamii katika tasnia ya upashanaji habari.

Kipimo cha ubora wa vyombo vya habari kinawasilisha muhtasari wa uripoti wa vyombo vya habari kwa kuzingatia maeneo tofauti ya ubora katika kipimo kimoja. Kiwango cha wastani cha ubora kimeimarika kutoka asilimia 27 mwaka 2019 hadi asilimia 32 mwaka 2022. Vyombo vya habari vilivyoongoza kwa mwaka 2022, kwa misingi ya viashiria tisa, ni Jamhuri, Radio Free Africa, Mwananchi,Clouds FM na TBC Taifa.

Ikilinganishwa na mwaka 2019, magazeti ya Jamhuri na Mwananchi yameendelea kuwa kwenye nafasi zao za awali kwa kuwa miongoni mwa vyombo vitano bora vya habari nchini. Kwa upande mwingine, Radio Free Africa, TBC Taifa na Clouds FM vimeimarika mno ikilinganishwa na huko nyuma ambapo vyote viwili vilikuwa mkiani kwenye orodha ya 2019. Zaidi ya
hapo, baadhi ya redio za kimikoa zimeshuka katika orodha hiy

Katika kipimo cha ubora wa maudhui kwa vyombo vya habari Tanzania 2022, JAMHURI limeongoza kwa kupata asilimia 43, mbele ya Gazeti la kila siku la Mwananchi lililoshika nafasi ya pili kwa asilimia 41, huku nafasi ya tatu ikienda kwa Redio Free Afrika kwa asilimia 38.

Kwa mujibu wa utafiti huo kwa upande wa magazeti Gazeti la JAMHURI ni la kwanza, likifuatiwa na Mwananchi, Raia Mwema asilimia 36,Citizen asilimia 33,Dailynews asilimia 30,sita ni The Gurdian asilimia 27,saba ni Zanzibar Leo asilimia 24,nane ni Nipashe asilimia 24 na la 10 ni Habari Leo asilimia 23.

Vyombo vingine vya habari vilivyoshirikishwa katika utafiti huo ni TBC1,Hits Fm,Clouds FM, TBC Taifa, UTV, Dodoma FM, The Citizen, Micheweni FM, EFM,ITV, Arusha 1 FM, Star TV, ZBC TV, CG FM,ZBC Redio,Redio One,Zanzibar Leo, Wasafi FM, Highlands FM, Zenji FM na Safari FM.

“Matokeo ya utafiti huo yameganywa katika sehemu nne, awali ya yote inatoa picha ya jumla ya matokeo yalivyo na baadaye imeonyesha matokeo mahususi kuhusu magazeti, redio na televisheni na mwishoni inatoa picha ya matokeo yanayohusu uripoti wa vyombo vya habari Visiwani Zanzibar.

“Kwa mwaka 2022 sampuli ilijumuisha kazi za kuhabari 1887 ambazo ni habari na vipindi kutoka kwenye magazeti tisa, vituo 15 vya redio, saba vya kitaifa na nane vya kimkoa visivyokuwa vya kitaifa na vituo vitano vya televisheni” umesomeka sehemu ya utafiti huo.

Aina ya vigezo vya kitaaluma vilivyoangaziwa katika utafiti huo ni pamoja na habari za matukio,vyanzo vingi vya habari, mitazamo miwili au zaidi ndani ya habari, maoni ndani ya habari, ukosoaji kwa Serikali, vyanzo sababishi vya habari,muundo mzuri sana wa uandishi, ujumuishi wa usuli wa kihistoria kwenye habari, utoaji haki ya kujibu tuhuma kwa watuhumiwa.

Katika vigezo hivyo vya kitaaluma Gazeti la JAMHURI limekidhi vigezo vitatu vya ubora katika vipengele vitatu vya vigezo vya kitaaluma ikilinganishwa na vyombo vingine vya habari.

Sababu nyingine zilizochangia Gazeti la JAMHURI kushika nafasi hiyo ni kutokana na kuandika habari za kueleweka, muundo mzuri wa uandishi ambao unaunganisha sehemu mbalimbali za habari kwa ufasaha, lakini pia uwezo wa mwandishi kuelezea ama kufafanua takwimu kwa wasomaji.

Mengine yaliyobainika kwenye utafiti huo ni vyombo vingi kutoripoti habari zitokanazo na juhudi binafsi za vyombo hivyo na badala yake vimekuwa vikitegemea zaidi habari za matukio.

Ripoti hiyo imebainisha mada zilizoripotiwa na vyombo vya habari ni habari za maendeleo kwa asilimia 30, habari za masuala yenye utata asilimia 25, uchumi asilimia 22, siasa asilimia 10, ajali na uhalifu asilimia 8, utamaduni au habari asilimia 5 na utafiti kwa asilimia 1.

Katika ripoti hiyo inaonyesha kuwa masuala ya utafiti uliripotiwa kwa kiwango cha chini zaidi kwa asilimia 1 huku habari za masuala zinazohusu masuala yenye utata na maendeleo zikitawala kwa asilimia 25 na 30.

Kuna tofauti kubwa kati ya redio, televisheni na magazeti lakini hata hivyo kwa ujumla, magazeti yamefanya vema kwenye vigezo vingi ukilinganisha na televisheni na redio.

Matumizi ya wanawake kama vyanzo vya habari ni moja kati ya vigezo muhimu vya ubora wa uandishi wa habari kwani husaidia sio tu kuleta uwiano wa kijinsia, bali kupaza sauti za wanawake. Matokeo ya utafiti yanaonyesha kazi zilizokuwa na angalau mwanamke mmoja kama chanzo cha habari ziliongezeka kwa mwaka 2022, huku magazeti yakionesha ongezeko
la asilimia 9.

Kwenye Redio, kuna tofauti ya wazi kati ya habari na vipindi. Taarifa za habari zimetawaliwa na habari za matukio kati ya asilimia 90 hadi 100. Hata hivyo, hali ni tofauti kidogo kwa redio za Dodoma FM, CG FM, Clouds FM na Hits FM ambazo zinajitahidi kuleta uwiano kati ya habari za matukio na zile za kutafuta wao wenyewe.

Kwa upande wa vipindi vya redio, hali ni tofauti. Kwa wastani, asilimia 95 ya vipindi vya redio vilitokana na jitihada za vyombo vya habari vyenyewe. Asilimia hii ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na mwaka 2019 (ongezeko kutoka asilimia 73 hadi 95).

Utofauti pekee ulijitokeza kwa Zenji FM ambayo ilikuwa na asilimia 33 tu ya vipindi vinavyotokana na jitihada za vyombo vya habari vyenyewe.

Kwa wastani, asilimia 81 ya habari za kwenye TV zilitumia vyanzo vingi vya habari. Tofauti na taarifa fupi za habari redioni, taarifa za habari za TV ni ndefu na hivyo kuweza kujumuisha vyanzo 2 au zaidi vya habari kwenye habari zake. Hata hivyo, utofauti kwenye matumizi ya vyanzo vingi vya habari haufanani baina ya kituo kimoja cha TV na kingine.

TBC1 ilikuwa na asilimia 38 ya vyanzo hivyo (kwenye kazi zenye vyanzo viwili au zaidi vya habari) vingi vikitoka serikali kuu na kwenye mamlaka za serikali za mitaa, huku watu wa kawaida (25%) na wadau wa elimu (10%) wakijumuishwa. Sehemu kubwa ya vyanzo vya habari vya ZBC TV vilitoka serikalini (56%). Kwa upande mwingine, ITV na UTV vilikuwa na vyanzo vichache vya habari kutoka serikalini.

Hali kama hiyo ilibainika kwenye vipindi. ZBC TV ilikuwa na kazi nyingi zaidi zenye vyanzo vya habari ‘2 na zaidi’ na sehemu kubwa ya vyanzo vyake vikitoka serikalini (37%), ilihali vyombo vingine ikiwamo TBC1 vikiwa na vyanzo vya habari kutoka maeneo mbalimbali.