KAMATI ya Bunge ya Bajeti, imeishauri Serikali kufanya mapitio ya gharama za miamala kutoka mtandao mmoja wa simu kwenda mtandao au benki na kutoka benki moja kwenda benki nyingine.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Juni 4, 2024 na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Twaha Mpembenwe, wakati akiwasilisha utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2023/24 na maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya mafungu 8 ya wizara pamoja na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi mwaka wa fedha 2024/25.

“Kamati imebaini kuwa bado viwango vya tozo za miamala vimebaki kuwa juu katika kuhamisha fedha kutoka mtandao wa simu mmoja kwenda mtandao mwingine, au kutoka katika mtandao wa simu kwenda benki.

“Kamati inaishauri Serikali kufanya mapitio ya gharama za miamala kutoka mtandao mmoja wa simu kwenda mtandao au kwenda benki na kutoka benki moja kwenda benki nyingine.

“Lengo la mapitio hayo ni kuhakikisha gharama hizo zinaakisi punguzo la gharama linalotokana na matumizi ya mfumo wa TIPS.

“Hatua hii itasaidia kupunguza matumizi ya fedha taslimu na kufanya malipo kwa kupitia mifumo ya benki na mitandao ya simu na Serikali itakusanya mapato zaidi,” amesema Makamu Mwenyekiti huyo.