Wafanyabiashara wa mazao ya baharini wanaopeleka nje na kuingiza samaki wana kilio chao kikubwa. Wafanyabiashara wa samaki aina ya kamba kochi hai (live lobster), kamba walioganda (frozen prawns) na kaa hai (live crabs) wako taabani kiuchumi.

Mwanzo walikuwa wanalipia mrabaha (royalties) kwa kamba kochi dola 0.9 za Marekani ambazo ni sawa na Sh 2,050, sasa wamepandishiwa hadi dola 3.0 za Marekani ambazo ni sawa na Sh 6,750 kwa kilo. Kamba mrabaha ulikuwa dola 0.4 za Marekani ambazo ni Sh 914, sasa umepanda hadi dola 1.4 za Marekani (Sh 3,150) kwa kilo moja.

Wamepandisha kaa hai kutoka dola 0.6 za Marekani (1,310) hadi dola 1.0 ya Marekani (Sh 2,280). Baada ya hapo wamepandisha leseni ya kusafirisha nje kutoka dola 100 za Marekani ambazo ni Sh 228,000 hadi dola 2,500 za Marekani (Sh 5,700,000) kwa kila aina ya samaki. Kiwango hiki wamepandisha ghafla kwa ajili ya leseni ya mwaka 2019 na kuendelea, kikiwa na tofauti ya Sh 5,472,000. Haya ni maajabu.

Mfano, unapeleka kamba kochi pekee unalipia leseni Sh 5,700,000 kwa mwaka ambazo ni sawa na Sh 475,000 kwa mwezi. Ukiwa unasafirisha kamba kochi hai na kaa hai unatakiwa kuwa na leseni mbili – ya kamba kochi hai na kaa hai – ambazo gharama yake ni Sh milioni 11.4 ambazo kwa mwezi ni Sh 950,000.

Ukiwa unasafirisha kamba kochi, kaa na kamba unatakiwa kuwa na leseni tatu ambazo utalipia Sh milioni 17 kwa mwaka ambazo ni wastani wa Sh 1,425,000 kwa mwezi. Hizo leseni ni kwa kila mtu anayesafirisha nje, hairuhusiwi kutumiwa na watu au kampuni zaidi ya moja. Hizo fedha za leseni tu za kusafirisha kwenda nje bado mrabaha ambao unalipa kwa kila kilo unayosafirisha. Kwa mfano, kama unasafirisha kilo 2,800 za kaa hai kwa mwezi utalipia dola 1 kwa kilo unazidisha kilo 2,800 ambazo ni sawa na Sh 6,384,000 kwa mwezi. Kwa mwaka ni Sh 76,608,000.

Kama unasafirisha kamba kochi kwa mwezi kilo 2,800 unazidisha kwa dola 3 ni sawa  na dola 8,400 (Sh 19,152,000) kwa mwezi. Kwa mwaka ni Sh 229,824,000.

Hesabu hizi zinapigwa kwa fedha za kigeni, kwa maana dola ya Marekani, bei ya nje haibadiliki, lakini huku kwetu kila mara dola inabadilika thamani yake. Ni vigumu kuelewa sababu za kitoweo kupandishwa kwa dola 2.1 (4,788) ni karibu na bei ya kuku mmoja au kilo moja ya nyama ya ng’ombe. Haileti picha wanatumia vigezo gani, maana gharama za ndege zinaumiza mno wafanyabiashara.

Huko nje mteja anatakiwa kulipia ushuru kabla ya kutoa mzigo na gharama nyingine kabla ya kuuingiza sokoni. Ni kitu kingine wasichojua au wanafanya makusudi maofisa wa serikali. Wasafirishaji wa Tanzania hawapangi bei, bali bei wanapangiwa na wauzaji na ushindani kwenye soko na mataifa mengine. Hizi ni takwimu za mfanyabiashara anayesafirisha kilo 700 kwa wiki tu; na hizo kilo ni kwa msafirishaji mkubwa.

Aina hii ya samaki baharini si wengi kiasi cha kuweza kumudu kulipia leseni moja Sh milioni 5.7 kwa mwaka. Wasafirishaji wako wengi. Ni vizuri awali walivyokuwa wanatozwa kila kilo wanayosafirisha na bei ya kawaida ya leseni ya kusafirishia ya awali. Kuna gharama za ukaguzi wa mzigo, kutengeneza vibali Wizara ya Mifugo na Uvuvi,  gharama za cheti cha TCCIA n.k.

Hizo gharama zote bado haujaweka kodi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), leseni za biashara ya ndani, leseni ya manispaa ya kukusanya samaki. Hiyo leseni ya kusafirishia kama ni mpya inabidi uende kuifuata Dodoma au kama karatasi ya leseni imejaa, karatasi mpya nayo inabidi uende Dodoma kuifuatilia. Hapo kuna gharama za usafiri, malazi n.k.

Kuna gharama za kusafirisha mzigo, kuna gharama za ndege kilo moja dola 2.5 za Marekani (Sh 5,640), vifaa vya kufungia mzigo, gharama za Swissport uwanja wa ndege, gharama za wakala wa ndege, gharama za kuufikisha mzigo uwanja wa ndege, gharama za kutengeneza karatasi za kwenda na mzigo, gharama za kutuma vibali kwa mteja,  gharama za umeme, gharama za kuchota maji ya baharini, gharama za maji safi, gharama za wafanyakazi, gharama za kuwasiliana na mteja wa nje mara kwa mara, gharama za ununuzi wa samaki kutoka kwa wavuvi n.k.

Katika gharama zote hizo bado kuna wengine wanakufa kabla ya kusafirisha, walio dhaifu hawasafirishwi kwani wanaweza kufia njiani. Wanaokufa njiani wanakuwa wamenunuliwa bei sawa, wamelipiwa gharama zote, na mteja wa huko halipi kwa waliokufa au kuharibika.

Wanaweza kufa kwa sababu ndege ya kuunganisha imechelewa, au wamepelekwa kusiko, wameachwa kwenye kuunganisha ndege au kuwaweka sehemu yenye joto au baridi kali.

Wafanyabiashara wetu wanashindana na wa nchi nyingine kama Kenya, Msumbiji, Madagascar, India, Sri Lanka au Vietnam, maana soko la kuuzia ndilo hilo moja. Nchi kama Hong Kong, China, Dubai, Thailand na Singapore hazina mlolongo wa malipo na bei kubwa, maana wanahamasisha wafanyabiashara wao wa ndani waingize pesa za kigeni nyumbani.

Nchi nyingine zina unafuu wa ndege, mfano Kenya wana ndege ya moja kwa moja ya Hong Kong, China, India, Vietnam, Sri Lanka – ziko karibu sana na soko, bei za ndege ziko chini kuliko hapa na wanaokufa nchi nyingine ni wachache kutokana na urahisi wa ndege na hawakai sana njiani.

Kwa hali yoyote, wafanyabiashara wa Tanzania ni vigumu kushindana na nchi nyingine kwa sababu gharama zetu ni kubwa na changamoto ni nyingi. Wengine wanafanya kwa mazoea tu kwa sababu ni biashara waliyoizoea. Wengi wa mwanzo walioanza wamefilisika au kubadilisha aina ya biashara kutokana na changamoto nyingi na wakati mwingine wateja wao wa nje kutowalipa fedha zote kwa visingizio kuwa mzigo unakufa sana kutokana na kukaa safarini muda mrefu.

Bei za kununua kaa hai na kamba kochi hai kwa Tanzania ziko juu mno kuliko nchi yoyote. Awamu ya serikali iliyopita Wachina walivamia hii biashara ya kaa hai na kamba kochi hai mpaka visiwani na sehemu zote wanakopatikana kama Kilwa, Mafia, Mtwara, Tanga, Bagamoyo na kadhalika.  Wakawa wananunua kwa bei za juu sana ili wapate mzigo mwingi na ‘waue’ wafanyabiashara wazawa wadogo wabaki wenyewe kwenye soko.

Huko kwao walikuwa wanatumwa na wenzao na wanawapa bei nzuri kuliko wanazowapa Watanzania. Hadi leo wavuvi na watu wa kati hawajawahi kushusha hizo bei kwa sababu kwenye mipaka baadhi ya Wachina wanaotumia vibali vya utalii wamebaki na wanatumia leseni za wazawa wasio waaminifu kinyume cha sheria za Tanzania.

Kisheria, hii biashara ndogo wageni hawaruhusiwi kuifanya, na ndio baadhi yao wameomba leseni za mwaka (2019) wazawa halisi wengi watashindwa kumudu gharama.

Tunaomba serikali iwafuatilie kwa karibu Wachina wanaokuja kama watalii, lakini wanajihusisha na biashara hii ya samaki, na wengine wanafanya biashara nyingine Tanzania, lakini pesa wanazopata hapa wananunulia samaki kwa kutumia leseni za wazawa. Fedha wanazouzia zinabaki kwao. Nchi yetu inakosa fedha za kigeni.

Msumbiji nako wana kaa na kamba kochi wengi kutokana na ukubwa wa mwambao wa pwani yao na sehemu kubwa ya mikoko, kwa hiyo wanawapata kwa urahisi tofauti na Tanzania. Kule Msumbiji bei zinakuwa chini.

Kwa hiyo wanaowapeleka ng’ambo wakiacha biashara hii hakuna faida yoyote. Hapa nchini wananchi wengi hawali aina hiyo ya samaki. Wanawaona kama wadudu tu. Serikali itapata hasara. Ukiwapeleka sokoni hapa wanaliwa na watu wachache wa pwani na raia wa kigeni wachache kutoka China, Vietnam, Thailand, Ufilipino na kadhalika.

Watanzania baada ya kupata soko la nje hawa samaki ndipo walipoanza kuwa na thamani. Ndipo serikali iliweka gharama za mrabaha kwa kamba hai na kaa hai, lakini cha kushangaza kila wakati inaongeza gharama kwenye mazao hayo hayo tu bila kuangalia vyanzo vipya vya kuingiza mapato.

Serikali iangalie hilo jambo kwa jicho la tatu kabla mambo hayajawa mabaya kwa pande zote mbili. Ni vizuri ipunguze gharama za kusafirisha nje ili wafanyabiashara wamudu kodi za ndani, maana hata TRA wanajua wanaosafirisha bidhaa nje wanapata faida kubwa kumbe fedha karibu zote zinachukuliwa na serikali.

Hii inawaletea usumbufu maofisa wa TRA kwa kujua kuwa wanatengeneza faida kubwa kumbe sivyo. Hizi gharama kubwa ni za kuua biashara. Zinawakatisha tamaa wafanyabiashara wanaothubutu kufanya biashara za kimataifa kwa kuleta pesa za kigeni na kuleta ajira kwa Watanzania.

Ni vigumu sana kwa sasa kuanza hii biashara kwa mjasiriamali hata kama amepata soko.

Serikali iangalie gharama hizi, izipunguze ili pande zote mbili zinufaike na kuweka mazingira yaliyo bora na rafiki kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati waweze kukua na kulipa kodi zaidi na kuongeza ajira. Hapa tutambue kuwa tunashindana na mataifa mengine kwenye biashara hii.

Kutoza leseni moja Sh milioni 5.7 si sahihi kabisa. Mbaya zaidi kila aina ya samaki ina leseni yake tofauti, ni kama kuwa na duka la nyama ukatakiwa kuwa na leseni ya kuuza mbuzi, leseni ya kuuza kondoo, leseni ya kuuza ng’ombe, au kuku na kadhalika. Haiwezekani kila mnyama akawa na leseni yake. Kwa wafanyabiashara wakubwa ni sawa, lakini kwa wadogo ni kuwakomoa.

Hili la kupandisha gharama za leseni kwa kiwango kikubwa hivi au mrabaha linaleta taswira kuwa nchi hii haina mfumo mzuri wa biashara na ni kukatisha tamaa wafanyabiashara wa ndani. Kunawatisha hata wale wa nje wanaotaka kuwekeza Tanzania kwa kuona nchi ina mazingira ya kibiashara yasiyotabirika.

Maofisa wa serikali wawe wanapeleka maoni ya wadau ngazi za juu na baadhi yao waache woga wa kupeleka maoni yao au kutoa lugha mbaya. Kwa mfano wapo wanaosema: “Kama biashara hii hailipi, fanya biashara nyingine.” Au “Sisi tunatekeleza uamuzi uliotoka juu.” Au “Tafuteni njia zenu za kukutana na wakubwa wenyewe.”

Nchi nyingine wanaofanya biashara ya kusafirisha vitu nje wanaheshimika, wanalindwa na serikali na wanawekewa mazingira mazuri ya biashara kwa kuwa wanaleta pesa za kigeni na kutoa ajira. Hapa kwetu mambo ni kinyume. Tunaomba serikali itazame kilio chetu hiki ili tuwekewe viwango vya kodi na ada vinavyohimilika.

Wanaoingiza samaki kutoka nje ya nchi

Hawa nao wana kilio chao, maana siku zilizopita walikuwa wanalipia kasha (container) la futi 40 ushuru usiozidi Sh milioni 20. Kwa sasa wanalipa dola 67,000 za Marekani (Sh milioni 150). Hii imekuwa vigumu kwa wafanyabiashara kuuza hapa ndani na wananchi wa kawaida kumudu gharama za kununua kitoweo hicho.

Samaki waliokuwa wanaagizwa ni jamii ya vibua ambavyo watu wa hali ya chini na kati walikuwa wanamudu bei zake. Samaki wanaovuliwa nchini ni wachache na ghali.

Kwa hili serikali iliangalie upya, maana wafugaji wa samaki ni wachache. Hawatoshelezi soko la ndani. Ingekuwa vizuri tungesubiri samaki waongezeke kwenye maziwa na bahari ndipo ushuru uwe mkubwa. Uvuvi haramu ukitokomezwa na wafugaji wakaongezeka, samaki wataongezeka pia na kukidhi soko na bei kwa walaji itapungua.

Please follow and like us:
Pin Share