NA MWANDISHI WETU, MUSOMA
Upotevu mkubwa wa fedha umebainika kuwapo katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, baada ya Kamati iliyoundwa kufuatilia mapato kubaini wizi na udanganyifu wa kiwango cha juu.
Kamati hiyo ya watu 13 iliundwa mwaka jana na kuongozwa na Mwenyekiti wake, Dickson Mwandara, na Katibu alikuwa ni Alfred Kikute.
Ilifanya uchunguzi kwa kusimamia makusanyo ya mapato katika minada sita na masoko sita kati ya masoko 15. Minada hiyo ni ya Kiagata, Kiabakari, Buhemba, Mwibagi, Bisayre na Sirorisimba. Masoko yaliyokaguliwa ni ya Butiama, Isaba, Buhemba, Nyakanga, Mmazami na Nyakiswa.
Kumetolewa mfano kuwa kabla ya ukaguzi huo, vyanzo vya mapato kwa siku 90 (miezi mitatu) vilikuwa jumla ya Sh milioni 52 kwa mchanganuo wa: minada (Sh milioni 38), masoko (Sh milioni 12.351) na vyanzo vingine vilikuwa Sh milioni 16.606.
Lakini usimamizi wa Kamati iliyoundwa wa siku 40 pekee uliweza kukusanya Sh milioni 52.209. Watumishi wote wanaotuhumiwa kujihusisha na ufisadi huo bado wanashikilia nafasi zao licha ya kuwapo mapendekezo ya kuwang’oa.
“Kwa mfano, Februari 2017 minada miwili ya Kiagata kabla ya kamati zilikusanywa Sh milioni 4.486; mnada mmoja wa Mwibagi (Sh milioni 2), minada miwili ya Kiabakari (Sh milioni 9.631), mnada mmoja wa Sirorisimba (Sh milioni 1.034), mnada mmoja wa Buhemba (Sh milioni 1.39) na mnada mmoja wa Bisarye zilikusanywa Sh milioni 1.203. Jumla kwa minada yote zilikusanywa Sh milioni 19.747.
“Mwezi Machi zilikusanywa Sh milioni 14.212 kwa minada yote. Fedha nyingi sana zilikuwa zinapotea. Lakini utaona sisi tuliposimamia mnada, kwa mfano mnada wa Kiabakari – mnada mmoja pekee tulikusanya Sh milioni 9.588. Wao hizo zilikuwa ni makusanyo ya minada miwili! Mwibagi ambao wao walikuwa wakikusanya Sh milioni 2 tu kwa siku, sisi tulikusanya Sh milioni 4.365 kwa siku! Huu ni wizi wa hali ya juu sana,” kimesema chanzo chetu.
Kamati inasema uchunguzi na usimamizi iliyoufanya umebaini udanganyifu na upotevu mkubwa wa mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama. “Mfano, mapato ya mnada wa Kiabakari yamepanda kutoka Sh milioni 5.385 (zilizokusanywa) hadi kufikia Sh milioni milioni 9.588. Hili ni ongezeko la Sh milioni 4.203 ambalo ni asilimia 78.06.
“Mapato ya mnada wa Mwibagi yamepanda kutoka Sh milioni 2 hasi Sh milioni 4.3 ambalo ni ongezeko la asilimia 107.3. Kamati imebaini ukosefu wa uaminifu na uadilifu kwa baadhi ya watumishi na mgambo.
Kamati imebaini kuwa baadhi ya watumishi waliopewa jukumu la kukusanya ushuru minadani na masoko siyo waaminifu kwani wanashirikiana na wafanyabiashara kukwepa kulipa ushuru unaostahili.
“Kwa mfano, katika mnada wa Kiabakari gari aina ya Hiace iliyotumika kusafirisha mbuzi kwenda Tarime ilikatiwa ushuru wa mbuzi 32 (Sh 48,000) badala ya mbuzi 60 waliokuwamo ndani ya gari hilo ambao walistahili kulipiwa Sh 90,000.
“Wakata ushuru wa Halmashauri wamejenga tabia na mazoea ya kukata risiti za ushuru usiolingana na idadi halisi ya mifugo iliyouzwa baada ya makubaliano ya kuachiana ‘kitu kidogo’ kwa kaulimbiu ya kuachiana maji ya kunywa,” imesema Kamati.
Eneo jingine ambalo Kamati imebaini upotevu mkubwa wa fedha ni kwenye kampuni za uchenjuaji madini.
Kamati ilitembelea kampuni 18 za uchenjuaji madini ya dhahabu na kufanya mazungumzo na baadhi yao kwa lengo la kuwahamasisha walipe ushuru wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Kampuni hizo ni Dorica Ketamara, Ludovic Investment, Zone 5 Co, Wegima, Isack Mniko Gold Mine, Pekemwa Co., Nyamaswa Investment, Paphalbion/AGM Co., Gochama Processing Plant, SGL Co., MP Co Ltd, Manyawa Group, Majengo Gold Extraction, Simion Odongo & Partners, Hernan Afro Asia, Bina Com, Washington Gerald, na Chacha Marwa Magesa.
Uchunguzi wa Kamati ulibaini kuwa kampuni pekee zilizolipa ni Dorica Ketamara ambayo kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka jana ilikuwa imeilipa Halmashaur Sh milioni 3 pekee. Kampuni nyingine ya Washington Gerald iliyoanza uzalishaji mwaka 2015 ilikuwa imeilipa Halmashauri ya Butiama Sh 350,000 tu.
Kampuni ya Majengo Gold Extraction iliyoanza uzalishaji mwaka 2013 ndiyo iliyolipa kiasi kikubwa cha Sh milioni 4 pekee. Kwa kampuni zote hizo, ushuru uliolipwa kwenye Halmashauri kwa miaka yote -kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka jana ni Sh milioni 7.35.
“Kamati ilipotembelea wachenjuaji ilibaini yafuatayo; idadi ya wachenjuaji Wilaya ya Butiama ni 17 badala ya 12 ambao rekodi zao ziko Halmashauri. “Kamati ilibaini kuwa wachenjuaji hawajawahi kufikiwa, kujulishwa na kudaiwa ushuru na Halmashauri.
“Kampuni 15 za wachenjuaji zilistahili kuilipa Halmashauri ya Butiama ushuru wenye thamani ya Sh milioni 120 kwa wastani wa Sh milioni 8 kila moja kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 badala yake wamelipa Sh milioni 7.35 kwa wote; kiasi ambacho ni sawa na asilimia 6.125.
“Kamati ilibaini kuwa mwaka 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ilistahili kulipwa Sh million 136 kutoka kwa wachenjuaji 17. Wachenjuaji wawili – Isack Mniko na Dorica Kitamara – wote wa Sirorisimba walifikishwa mahakamani na baadaye ikakubalika nje ya Mahakama kuwa watailipa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Sh milioni 1.5 kwa kila mwezi hadi deni lote la Sh milioni 8 kwa kila mmoja litakapomalizika.
“Pamoja na makubaliano hayo, utekelezaji wake bado unasuasua, kwa mfano siku Kamati inatembelea Sirorisimba naye akaondoka kwenda kulipa deni siku hiyo,” imesema taarifa ya Kamati.
Kamati imewashutumu watumishi wa Halmashauri wanaopaswa kufuatilia malipo kutoka kwa wachenjuaji, lakini wameshindwa kufanya hivyo na kuisababishia Halmashauri ukosefu wa mapato.
“Kamati ilihoji mwanasheria wa Halmashauri ni kwanini wachenjuaji 15 waliostahili kulipa ushuru wa halmashauri hawajafikishwa mahakamani kama wale wawili, na mwanasheria aliijibu Kamati kuwa hajapelekewa majina hayo mengine kutoka Ofisi ya Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, na kwamba akipewa atayashughulikia,” imesema taarifa hiyo.
Kamati imeainisha changamoto kadhaa kwenye sekta ya madini katika Wilaya ya Butiama. “Kiburi, dharau na urasimu wa kuingia katika migodi ya kampuni za uchenjuaji. Mfano, kuingia katika mgodi au sehemu ya uchenjuaji, Kamati ilitumia zaidi ya saa mbili hadi tatu kuruhusiwa kuingia na kuonana na viongozi hasa kwa kampuni ya Bina Com ya Nyasirori na MP Company ya Magunga.
“Ushirikiano duni ulionyeshwa na wadau wa sekta ya madini waliopo wilayani Butiama. Mfano, kampuni ya Bina Com pamoja na kupata taarifa ya ujio wa Kamati hawakukubali wala hawakuwapo wakati Kamati ilipowatembelea.
“Kamati imegundua udhaifu mkubwa katika kusimamia na kufuatilia mapato ya Halmashauri katika sekta ya madini ikiwa ni pamoja na Halmashauri kutokuwa na takwimu sahihi za wadau wa sekta hii.
“Mfano, MP Company Limited ilianza kazi mwaka 2013, kupitia kwa foreman (msimamizi) wake alikiri kuwa kampuni yao haijawahi kuombwa/kudaiwa ushuru wowote wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, kauli ambayo iliungwa mkono na Ofisa Mapato wa Halmashauri.
“Alipoulizwa kwanini hajawahi kudai ushuru, alidai alikuwa haitambui, licha ya kukiri baadaye kwamba imekuwa ikichangia michango mbalimbali katika Halmashauri ikiwamo ya Mwenge na ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Magunga.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mwandara, amethibitisha kukamilika kwa ripoti na kuikabidhi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Solomoni Ngiliule, kwa utekelezaji.
“Tulikabidhi ripoti yetu kwa DED (Mkurugenzi Mtendaji) ndani ya muda sasa hatua za utekelezaji wa mapendekezo yetu atafutwe DED,” ameliambia JAMHURI. Hata hivyo, Ngiliule hakupatikana.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Magina Nyauko, amesema baada ya ripoti ya Kamati hiyo kuwasilishwa kwa DED ilijadiliwa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo na kuyakubali mapendekezo.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Nyauko inapingana na ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Anna-Rose Nyamubi, aliyesema ripoti hiyo inatarajiwa kujadiliwa hivi karibuni kwenye Baraza hilo.
Kwa upande wake, Nyauko anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo aliunda ‘timu’ ya maboresho ya ukusanyaji mapato hususani kwenye minada, miongoni mwa wajumbe wakiwa ni madiwani wenye wajibu wa kufuatilia mwenendo wake.
Mbali na kusema kikao cha Baraza la Madiwani kitakutana hivi karibuni kuijadili ripoti hiyo, Nyamubi, ameng’aka akisema; “Suala hilo siyo langu na kwa kawaida sitoi taarifa kwa njia ya simu…”
Taarifa za uhakika kutoka Butiama zinasema ripoti hiyo haijajadiliwa, na yote hiyo ni kutokana na baadhi ya viongozi wa Halmashauri kuhusishwa kwenye ufisadi huo.
Wingi wa kodi
Kamati imebaini kuwapo kwa kodi nyingi wanazotozwa wafanyabiashara wanaochinja na kuuza nyama minadani na hivyo kuwa kero kubwa kwao na mwishowe kwa wananchi wanaonunua nyama.
“Mfano, mfanyabiashara anaponunua mbuzi mmoja hutozwa kodi/ushuru kati ya Sh 6,500 hadi 7,500 kabla hajaanza kuuza nyama kwa mchanganuo ufuatao: Mchinjaji (BAKWATA) hulipa Sh 1,500 kwa mbuzi na Sh 4,000 kwa ng’ombe; ushuru wa ukaguzi (Sh 1,500) kwa mbuzi na Sh 2,500 kwa ng’ombe; ushuru wa mwamba (Sh 1,000) kwa mbuzi/kondoo na Sh 2,500 kwa ng’ombe; wachunaji (Sh 1,000 hadi 1,500 kwa mbuzi) na Sh 2,000 hadi 2,500 kwa ng’ombe. Ushuru wa soko (Sh 1,500 kwa mbuzi/kondoo) na Sh 5,000 kwa ng’ombe.
“Mkaguzi anapokagua nyama anachukua nyama kati ya kilo 1 hadi 2 kwa kila ng’ombe anayechinjwa; na nusu kilo kwa mbuzi anayechinjwa. Kero hii ilijitokeza katika mnada wa Kiabakari na Kamati ilimuhoji Ofisa Mifugo Kata ya Kukilango na kukiri kuwapo kwa hali hiyo akisema ni makubaliano.
Majibu hayo yalipingwa na wafanyabiashara na kuiambia Kamati kuwa wanalazimishwa bila ridhaa yao kwani wakipinga hutishiwa nyama zao kufukiwa kwa madai kuwa hazifai.
“Kero hii pia iko Nyankanga ambako wafanyabiashara wanaomba wapewe eneo wajenge mwamba wa kuchinjia kwani uliopo ni wa mtu binafsi anayewatoza Sh 2,500 kwa mnyama. Kamati iliona hii ni kero kubwa sana kwa wadau hawa na imekuwapo kwa kila mnada katika Wilaya ya Butiama,” imesema Kamati.
Dosari nyingine imebainika kuwapo kwenye matumizi ya mashine za kielektroniki (EFD). Wakati wa uchunguzi wa Kamati, ilibainika kuwa mashine nyingi zimesajiliwa kwa jina la Edwin Kagugu japo zinatumiwa na watu wengine. Kagugu ndiye msimamizi wa fedha wa Halmashauri ya Butiama.
“Mashine nyingi zinatumika kwa muda mfupi na kudaiwa kuishiwa chaji na hivyo kushindwa kukusanya mapato yote. Kamati ilibaini hii ilikuwa mbinu chafu iliyobuniwa na watumishi wasio waadilifu ili kuzorotesha juhudi za kukusanya mapato.
“Mashine kutoa risiti zisizo na ID number inayoonyesha ni mashine namba ngapi imetoa risiti hiyo japo wakati wa mwisho kila mashine inaonyesha ID number. Kwa hali hiyo Kamati inat ia shaka kuwa huenda kuna mchezo mchafu; pia mashine kusoma tarehe na muda tofauti,” imesema Kamati.
Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ni miongoni mwa halmashauri katika Mkoa wa Mara ambazo hazina huduma za kijamii za kutosheleza mahitaji ya wananchi. Ina uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa na madawati katika shule za sekondari.
Pia inakabiliwa na uhaba mkubwa za zahanati, hata pale zilipo kumekuwa hakuna dawa na vifaa tiba.
Mnada wa Kiabakari ambao umebainika kuingiza wastani wa Sh milioni 9 kwa siku, huku minada ikiwa mara tatu kwa mwezi, hauna huduma kama za vyoo na maji, hali inayowafanya wananchi wengi kujisaidia ovyo.

By Jamhuri