MugabeRais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, ameamua kuweka pamba masikioni,  baada ya kupuuzia wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, kwa viongozi wa Afrika kuacha kung’ang’ania madaraka kwa muda mrefu.

Hakuna ubishi kwamba kauli hiyo ya Ban Ki-moon iliwalenga zaidi Rais Mugabe na Yoweri Museveni ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita alichaguliwa tena kuongoza Uganda kwa miaka mitano ijayo. Ana miaka 30 madarakani baada ya kushika hatamu mwaka 1986.

Rais Mugabe amezungumza na wananchi wa Zimbabwe na kuwaambia, “Achaneni na habari za Ban Ki-moon. Achaneni na ushawishi wake, mimi nitaendelea kuongoza mpaka Mungu atakaposema ‘Mugabe njoo’.”

Mugabe aliyetimiza miaka 92 Jumapili iliyopita, anasema hana mpango wa kuachia ngazi.

Kiongozi huyo mwenye rekodi ya pekee ya kuwa madarakani kwa muda mrefu, amefanya Zimbabwe isimfahamu rais mwingine zaidi ya mwamba huyo aliyeingia madarakani tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1980.

Maisha yake na afya yake yamekuwa yakitatiza akili za wakereketwa wa Chama cha ZANU-PF, lakini amewathibitishia kwamba yuko fiti na ana uwezo wa kufanya kazi.

Hata wapinzani wamekuwa na shaka na kiongozi huyo. Mpinzani wake mkuu, Morgan Tsvangirai, anasema: “Nchi inakumbwa na njaa, uchumi unashuka, hakuna anayejali kwa matatizo ya nchi. Ni kama hakuna serikali chini ya ZANU-PF ambayo inatukuzwa pasipo sifa za kidemokrasia.”

Mbali ya Tsvangirai, pia makundi mbalimbali yanapinga mpango wa Rais Mugabe anayesisitiza hadi Mungu amwite siku ya kifo ndipo itakuwakuwa mwisho wa urais wake Zimbabwe.

Makundi hayo yameanza kuandamana, na tayari Polisi nchini Zimbabwe wameanza kuwakabili wapinzani hao kwa kuwarushia mabomu ya kutoa machozi pamoja na maji ya kuwasha.

Taarifa kutoka Zimbabwe zinasema kwamba kuna malengo ya kuzuia maandamano yaliyopangwa na maelfu ya maveterani wa kivita mjini Harare.

Maveterani hao walieleza sababu za maandamano yao kuwa ni kupinga wazo ama pendekezo la mke wa Rais Robert Mugabe, Grace, kupendekezwa kuwa ndiye rais ajaye wa nchi hiyo.

Rais Mugabe aliyetimiza umri wa miaka 92, pamoja na pendekezo hilo, Grace Mugabe amesema kwamba mpaka sasa hana matarajio ya kuwa rais ingawa inaonekana dhahiri kwamba yeye ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuwa mgombea wa nafasi hiyo.

Makamu wa Rais wa sasa nchini humo, Emmerson Mnangagwa, anatajwa kuwa ndiye chaguo la vyama vya upinzani nchini humo na hata ndani ya chama tawala cha ZANU-PF na ana mashiko kwa wapigania uhuru walio wengi wa Zimbabwe.

By Jamhuri