Mgombea urais wa Chama cha Republican, Donald Trump (pichani), amempongeza kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, siku chache baada ya kiongozi huyo wa dini kutilia shaka kuhusu imani yake ya kidini.

Papa amesema kuwa pendekezo la Trump la kujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico si la mtu mwenye imani ya dini ya Kikristo, hatua iliyoibua hisia kali kutoka kwa mfanyabiashara huyo.

Akizungumza na makada wa chama chake kwenye Ukumbi wa Carolina, bilionea huyo ambaye ni mwekezaji mkubwa wa hoteli, alikuwa na sauti ya maridhiano.

Wanachama wa chama hicho wanatarajiwa kumchagua mwakilishi kwa tiketi ya kugombea urais ya chama hicho siku chache zijazo.

Trump anaongoza kura ya Jimbo la Carolina Kusini na alikuwa katika runinga ya kitaifa katika eneo la Columbia kujibu maswali.

Alipoulizwa kuhusu mgogoro wake na Papa Francis, alisema kwamba hawezi kuuelezea kama vita, ijapokuwa alisema baadaye kwamba asingependa kutofautiana na kiongozi huyo wa dini.

Amesema kuwa Papa Francis hana haki yeyote kumhukumu iwapo ni muumini au la “inasikitisha,” alisema Trump.

Mapema Papa Francis alisema kuwa wazo la Trump la kujenga ukuta kati ya Mexico na Marekani si la Kikristo. Alisema kuwa kwa mtu yeyote ambaye katika karne hii ya 21 anayetaka kujenga ukuta badala ya kujenga daraja huyo si Mkristo.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki aliyasema hayo katika siku yake ya mwisho ya ziara nchini Mexico.

Trump anayepigiwa upatu kutwaa tikiti ya chama cha Republican katika uchaguzi mkuu ujao, amependekeza kujenga ukuta na ua katika mpaka kati ya nchi yake na mexico ili kuwazuia wahamiaji kuingia nchini Marekani.

Licha ya kuwaambia waumini wa Kanisa Katoliki kuwa hatawazuia kutumia uhuru wao kumchagua rais wanayempenda, Papa Francis amesema kuwa iwapo Trump anapanga kujega ua basi “si Mkristo”.

Mtazamo huo wa Papa Francis bila shaka unatarajiwa kuwapa wapinzani wa Trump fataki, huku wakiendelea na kura za mchujo ambapo msimamo wa kidini wa mgombea unatazamwa na wapiga kura wengi kuwa kigezo muhimu. Mmoja kati ya Wamarekani watano ni Mkatoliki.

By Jamhuri