Na Mwandishi wetu, JamhuriMedia, Songea
Viongozi wa Serikali kutoka Mkoa wa Ruvuma, Mtwara nchini Tanzania na Mkoa wa Niassa nchini Msumbiji wamekutana katika kikao cha pamoja kilicholenga kuimarisha ushirikiano wa maendeleo na usalama katika maeneo ya mipakani yanayounganisha mikoa hiyo mitatu.
Kikao hicho cha siku mbili kilichofunguliwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Nyasa kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas,katika ukumbi wa mikutano wa Heritage Cottage manispaa ya Songea mkoani Ruvuma , kilihudhuriwa na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na maafisa wa sekta mbalimbali kutoka pande zote mbili.
Lengo kuu lilikuwa kujadili namna ya kuimarisha ulinzi wa mipaka, kukuza biashara halali na kuimarisha mahusiano ya kijamii na kiuchumi kati ya wananchi wa Tanzania na Msumbiji.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Peris Magiri alisema ushirikiano wa karibu kati ya mikoa hiyo ni muhimu katika kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa sambamba na kuchochea maendeleo ya wananchi wanaoishi katika maeneo ya mipakani.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Serikali ya Mkoa wa Niassa nchini Msumbiji Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Niassa Celestino Vianeque alieleza kuwa Msumbiji inaendelea kuthamini uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya wananchi wa pande zote mbili, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za uhalifu wa kuvuka mipaka.
Katika kikao hicho, wajumbe watajadili masuala mbalimbali ya kiusalama ikiwemo biashara haramu, usafirishaji wa bidhaa kinyume cha sheria, ujangili na uhamiaji usio rasmi na kuimarisha doria za pamoja katika maeneo ya mipakani.
Aidha Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Ruvuma Marco Chilya alisema kuwa kikao hicho ni utaratibu waliojiwekea wa kuendelea kufanya mikutano ya mara kwa mara ili kufuatilia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na kuhakikisha ushirikiano kati ya Ruvuma na Niassa unaendelea kuzaa matunda kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili na kuimarisha usalama mikoa ya kusini.







