Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Wabunge wameipongeza Serikali kwa usikivu na umakini wake kwa kukubali kufanyia marekebisho baadhi ya tozo, kodi na ada mbalimbali zilizokuwa zikipendezwa kwenye Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwakanwa fedha 2026/2027, iliyopitishwa jana bungeni Jijini Dodoma.
Miongoni ya maamuzi yaliyowakuna wabunge ni kuondoa nia ya kutoza ushuru wa bidhaa kwenye pikipiki (bodaboda), tozo ya shilingi kumi kwenye sukari inayozalishwa hapa nchini, na kuondoa pendekezo la kuanzisha kodi zuio kwenye mazao ya kilimo, uvuvi na ufugaji.
Awali akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Fedha Bungeni, Dodoma, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), alisema kuwa Serikali imefanya majadiliano ya kina na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, na kuafikiana maeneo kadhaa yaliyokuwa yanapendekezwa na Serikali katika maboresho ya kodi na tozo mbalimbali.
“Muswada huu unakusudia kurekebisha Sheria mbalimbali za kodi na zisizo za kodi kwa lengo kubadili viwango vya kodi, tozo na ada zinazotozwa chini ya
Sheria mbalimbali za kodi pamoja na kuboresha mazingira ya biashara, kuweka
na kuboresha taratibu za ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya Serikali, ili
kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi, hususani katika sekta za kimkakati
ikijumuisha viwanda, kilimo, nishati na afya ili kuongeza tija na uzalishaji, kukuza
ajira na kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali” alisema Mhe. Balozi Omar.
Alifafanua baadhi ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa niaba ya wananchi kuwa ni pamoja na
Kupunguza kiwango cha ushuru wa bidhaa wa asilimia 20 kwenye
magari yenye umri wa miaka nane lakini hayazidi miaka kumi
iliyopendekezwa kwenye Muswada hadi asilimia 18;
Kupunguza ushuru wa bidhaa wa asilimia 40 uliopendekezwa kwenye
Muswada kwa magari yenye umri wa zaidi ya miaka kumi lakini hayazidi
miaka ishirini, hadi asilimia 35;
Kupunguza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwa magari yenye miaka
inayozidi ishirini na kuendelea uliopendekezwa kwenye Muswada kutoka
asilimia 50 asilimia 40;
Kuondoa pendekezo la kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha
asilimia 5 kwenye thamani ya dau la michezo ya kubahatisha kama
ilivyokuwa imependekezwa kwenye Ibara ya 9 ya Muswada;
Kuweka masharti kuhusu msamaha katika Framework Agreements
baina ya Serikali na kampuni za madini, ambapo tumekubaliana na
Kamati kwamba, msamaha husika hautahusisha bidhaa za mafuta,
utatolewa kwenye kipindi cha ujenzi wa mradi pekee na utamaliza muda
wake pale tu kampuni husika zitakapoanza uzalishaji wa madini. Aidha,
kampuni itakayotumia vibaya misamaha husika itachukuliwa hatua za
kisheria ikiwemo kusitishiwa misamaha husika na kurejesha kodi yoyote
waliyosamehewa;
Kuondoa pendekezo la kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha
asilimia 5 kwenye pikipiki kama ilivyokuwa imependekezwa kwenye
Ibara ya 11(g) ya Muswada;
Kuondoa pendekezo la kutoza kodi ya zuio kwa kiwango cha asilimia
moja (1) kwenye malipo yanayohusu mazao ya kilimo, wanyama hai,
maziwa, Samaki, na mabondo kama ilivyokuwa imependekezwa kwenye
Ibara ya 25 ya Muswada;
Kuondoa pendekezo la kutoza kodi kwa utaratibu wa malipo ya mkupuo
kwa asilimia moja (1) katika mapato yanayotokana na mazao ya kilimo
kama ilivyokuwa imependekezwa kwenye Ibara ya 28 ya Muswada;
kupunguza kiwango cha kodi kwa walipa kodi chini ya utaratibu wa
makadirio kutoka kiwango cha asilimia 4.5 kinachopendekezwa kwenye
Muswada hadi asilimia 4 kwa mapato yanayoanzia shilingi 11,000,001
hadi 200,000,000;
Kuongeza wigo wa matumizi ya asilimia 5 inayotokana na mgawanyo wa
mapato ya tozo ya maendeleo ya reli kutumika pia kwa ajili ya ujenzi wa
miundombinu kwa ajili ya uongezaji thamani;
kuondoa tozo ya shilingi kumi kwa sukari inayozalishwa nchini
iliyopendekezwa kupitia Muswada huu na na badala yake kuweka tozo
kwa sukari inayoagizwa nchini.



