Home Makala HATUPANGI KUSHINDWA, TUNASHINDWA KUPANGA (12)

HATUPANGI KUSHINDWA, TUNASHINDWA KUPANGA (12)

by Jamhuri

Ukiua muda unaua fursa

Muda una mbawa za kupaa, utumie vizuri. William Shakespeare, mshairi na mwigizaji alilalamika: “Nilipoteza muda; sasa unanipoteza.” Ukiwa mtoto, muda unatambaa. Ukiwa kijana muda unatembea. Ukiwa umri wa kati, muda unakimbia. Ukiwa mzee muda unapaa. Unakimbia kwa spidi mithili ya feni kwenye namba tano.

Muda uliobaki kwa kila mmoja ni kama salio ambalo hujui ni kiasi gani. Kama ungekuwa unanunua siku moja kwa gharama ya Sh laki moja ungeitumiaje? Ukiua siku moja, unaua saa ishirini na nne za furaha.

Paulo wa Tarsus alitoa ushauri: “Tumieni vizuri muda mlio nao.” (Waefeso 5:16).

Kama kila siku, kila mtu angewekewa katika akaunti yake Sh 86,400, fedha hizo azitumie kabla ya siku kwisha, bila shaka hakuna shilingi ambayo ingebaki. Kila mtu ana sekunde 86,400 kila siku. Je, tunaziua au tunazitumia vizuri? Jua “hazina zote za dunia haziwezi kurudisha kitambo cha muda kilichopotea.” (Methali ya Ufaransa).

Jifunze thamani ya dakika tatu. Jioni ya Aprili 16, 1912, meli kubwa sana iliyoitwa TITANIC ilizama na kuua watu zaidi ya 1,500. Kisa, kutokuthamini dakika tatu. Hii ni mojawapo ya sababu iliyosababisha mamia ya watu kuingia katika kaburi la maji.

Kwa mujibu wa Gazeti la Washington Post, nahodha alipigiwa simu. Dakika ilipita! Dakika nyingine ilipita! Nahodha alikuwa anashughulikia mambo yake madogo madogo. Dakika ya tatu muhimu ilipita! 

Baada ya kumaliza shughuli zake ndogo alichukua simu. “Kuna mlima wa barafu mbele! Rudisha meli nyuma!” Ilisikika sauti kutoka kwenye simu. Nahodha alikuwa amechelewa. Alipoteza dakika tatu, zikawapoteza abiria. Aliua dakika tatu, zikaua abiria. Mlima wa barafu mbele ulitengeneza tundu la futi 300 ambapo maji yalipenya na kuingia kwenye meli. Watu zaidi ya 1,500 waliiaga dunia. Nahodha aliua dakika tatu, akaua fursa ya kuokoa watu. Nahodha aliua muda, muda ukaua watu.

“Muda: ambao binadamu anajaribu kila mara kuua, lakini unaishia kumuua,” alisema Herbert Spencer (1820 -1903) mwanafalsafa wa Uingereza.

Kadiri ya simulizi ya baadaye, mwanamke aliyepanda meli hii huko Southampton alimuuliza mhudumu wa meli: “Ni kweli kwamba meli hii haiwezi kuzama?” Mhudumu alijibu: “Mama, Mungu mwenyewe hawezi kuizamisha.” Kumbuka mbele ya Mungu tunabaki kuwa viumbe.

Usiseme hauna muda wa kutosha. Una saa zilezile kwa siku, alizonazo Bill Gates, Aliko Dangote, Donald Trump na Salim Awadh Bakhresa. 

Una saa zilezile kwa siku alizokuwa nazo Reginald Mengi (1943 –2019), Ali Mufuruki (1959 –2019), Mama Maria Teresa wa Calcutta (1910 – 1997), Ruge Mutahaba (1970 – 2019), Steven Charles Kanumba (1984 – 2012). Wale ambao wanatumia muda vibaya ni wa kwanza kulalamika kuwa muda ni mfupi.

Kwa wahubiri, Mark Twain, alipendekeza kujua umuhimu wa dakika ishirini. Alisema: “Baada ya dakika ishirini za mahubiri hakuna mdhambi anayeokolewa.” Ni kama alisema ndani ya dakika ishirini kuna fursa ya kuwavuta na kuwashawishi watu wamwelekee Mungu.

Fursa zipo kila mahali, fungua macho utazame na uone. Kuwa tayari kupokea mawazo na kuyafanyia kazi. “Fursa yako kubwa ipo ulipo sasa hivi,” alisema Oliver Napoleon Hill (1883-1970) mtunzi wa vitabu wa Marekani anayejulikana kwa kitabu chake ‘Think and Grow Rich’ (1937).

Kuna mambo manne yakienda hayarudi: neno lililotamkwa, mshale uliorushwa, maisha yaliyopita na fursa iliyodharauliwa. Ukiua muda, unaua fursa.

You may also like