Nahodha wa Liverpool na mchezaji wa timu ya taifa ya Uingereza, Jordan Henderson, ameeleza masikitiko yake kwa Sadio Mane na Mohamed Salah baada ya wachezaji hao kushindwa kushiriki Michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea huko nchini Qatar. 

Mohamed Salah ameshindwa kushiriki Michuano ya Kombe la Dunia baada ya timu yake ya taifa ya  Misri kutofuzu kushiriki Michuano hiyo huku Sadio Mane akipata majeraha nyakati za mwisho kabla ya kujiunga na timu yake ya taifa ya Senegal kuelekea Michuano hiyo mikubwa duniani kwa ngazi ya nchi. 

Kiungo huyo wa Liverpool na England amenukuliwa akisema, “Sijaongea na Mo kusema ukweli. Ninaamini atakuwa sehemu fulani akifurahia mapumziko yake huko.”

“Hakutegemea kuona timu yake na yeye hawajafuzu kushiriki Michuano hii [Kombe la Dunia]. Wachezaji Bora duniani huwa wanapenda kucheza Kombe la Dunia na yeye ni miongoni mwa hao,” aliongeza. 

“Kwa hakika upande wa Sadio [Mane] ilikuwa kinyume kabisa cha matarajio. Nilizungumza naye niliposikia amepata majeraha na alionesha kujisikia vibaya sana kukosa Michuano ya Kombe la Dunia,” alihitimisha kiungo huyo wa Uingereza na Liverpool ambaye amecheza pamoja na Mohamed Salah na Sadio Mane ambaye ametimkia Bayern Munich ya Ujerumani.