Hifadhi ya Serengeti kuongezwa

Serikali inakusudia kuongeza ukubwa wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, ameliambia Bunge kuwa wizara yake imetayarisha mapendekezo ya kubadili mpaka wa hifadhi hiyo.

Kwa sasa ukubwa wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyoko katika mikoa ya Mara na Simiyu ni kilometa za mraba 14,763. Eneo linalokusudiwa kujumuishwa ni la Pori Tengefu la Ghuba ya Speke, lenye ukubwa wa kilometa za mraba 57 na sehemu ya ukanda wa maji wa Ziwa Victoria yenye ukubwa wa kilometa za mraba 81.

Katika hotuba yake ya bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020, Dk. Kigwangalla amesema: “Hatua hiyo itahakikisha upatikanaji wa malisho na maji kwa wanyamapori muda wote, kuimarisha usimamizi wa mazalia ya samaki, kupunguza migogoro na kufungua fursa za maendeleo ya utalii Kanda ya Ziwa na kuimarika kwa ustawi wa wananchi.

“Utekelezaji wa mapendekezo ya kubadili hadhi maeneo hayo unashirikisha wadau wote na fidia stahiki zitalipwa pale itapolazimu kuhamisha wakazi,” amesema.

Katika mkakati huo wa kuimarisha uhifadhi, waziri huyo amesema wizara inaendelea na mpango wa kubadilisha hadhi maeneo ya hifadhi.

“Katika kutekeleza azima hiyo, wizara inakamilisha taratibu za kubadili hadhi mapori ya akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa hifadhi za taifa,” amesema.

Pia amelihakikishia Bunge kuwa mchakato wa kubadili hadhi ya mapori ya akiba Kigosi, Moyowosi na Ugalla unaendelea. Hakuna aina ya mabadiliko yanayokusudiwa, lakini kama ni upandishaji hadhi, basi mapori hayo yatakuwa hifadhi za taifa.

Pamoja na Serengeti, hifadhi nyingine za taifa na ukubwa wake kwa kilometa za mraba kwenye mabano ni: Ruaha (20,226), Katavi (4,471), Mkomazi (3,245), Mikumi (3,230), Tarangire (2,850), Udzungwa (1,990), Kilimanjaro (1,668), Saadani (1,100), Manyara (648.7), Arusha (552), Rubondo (457), Kitulo (412.9), Gombe (56), Mahale (37.5) na Saanane (2.18).

Habari zaidi kuhusu Hotuba ya Bajeti ya Waziri Kigwangala soma Uk. 11, 12, 13, 14, 15 & 16.