Ofisi ya Uhamiaji Wilaya ya Ngara mkoani Kagera imekuwa ikisababisha usumbufu kwa wananchi wilayani humo kuhusu uraia wa baadhi yao.

Inaelezwa kuwa utaratibu wa maofisa Uhamiaji wilayani humo wa kuvizia mabasi na magari yanayofanya safari zake ndani ya wilaya na kuwakamata wasafiri wakihisiwa kuwa wahamiaji haramu, umekuwa na usumbufu mkubwa.

JAMHURI limeelezwa kuwa ukaguzi huendeshwa kwa upendeleo, baadhi ya wasafiri hukaguliwa na kuachiwa huru bila hata kuwa na vitambulisho, lakini wengine wanaobainika kukosa vitambulisho hushikiliwa na maofisa hao.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa kadhia hiyo, maofisa Uhamiaji husimamisha kila gari na kumtaka kila abiria kuonyesha kitambulisho ama cheti chochote alichonacho kinachothibitisha kuwa ni mkazi wa Ngara au raia wa Tanzania.

Kwa wale ambao hubainika kusafiri bila kuwa na kitambulisho au cheti chochote hukutana na manyanyaso mbalimbali ikiwemo kupigwa na kufikishwa kituoni.

Kasoro zilizomo katika uhakiki huo ni pamoja na maofisa hao kuwakamata baadhi ya wananchi pasipo kuwaeleza makosa yao wala kuwapa nafasi ya kujieleza.

Cornel Kakoko, mzaliwa wa Wilaya ya Ngara, katika Kijiji cha Mjembwe kilichopo Tarafa ya Rulenge, anaeleza kuwa mwanzoni mwa mwezi huu alikamatwa na maofisa wa Uhamiaji wilayani humo na kufikishwa kituoni bila kuelezwa makosa yake.

Anasema: “Nakumbuka ilikuwa siku ya Jumatano niliposafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Kahama hadi Ngara nikiwa na dada yangu aitwaye Anitha. Wakati naelekea Ngara tulifika eneo moja linaitwa Nyakahura, pale tukakuta kizuizi.

“Tulivyofika kwenye kizuizi gari lilisimamishwa akaingia kijana mmoja kwenye gari akasema anakagua vitambulisho. Sikuwa na kitambulisho, nikaambiwa nishuke kwenye gari, wakati huo dada yangu akiwa na vitambulisho akaambiwa apande kwenye gari, na wakaamuru gari liondoke.”

Anaeleza kuwa wakati wa tukio hilo, kulikuwa na wazee wawili ambao pia walishushwa kwenye gari hilo kwa tuhuma sawa na zake,  lakini waliachiwa huru kwa maelezo kwamba watawasiliana na maofisa hao baadaye.

“Mimi niliambiwa nibaki. Walivyonipeleka kwenye gari lao wakaniuliza nina umri gani, nikawajibu. Yule kijana aliyeingia kwenye gari aliniuliza kuhusu kitambulisho nikamwambia sina, akanipiga kofi kwenye sikio la kushoto,” amedai.

Kwa mujibu wa Cornel, kofi hilo alilopigwa limemsababishia maumivu katika sikio hilo, na kwamba baada ya kupigwa walimpandisha kwenye gari na kumpeleka ofisi za Uhamiaji mjini Ngara.

Hata hivyo, anaeleza alivyofikishwa katika ofisi hizo maofisa hao walimwachia huru na kumwambia aendelee na safari zake pasipo kuchukua maelezo wala kumwambia makosa yake.

William Nanyungu, mkazi wa Ngara naye amepata kukutana na masaibu hayo mwaka 2016 wakati akifanya kazi katika mgodi wa Buzwagi uliopo wilayani Kahama.

Anasema wakati akifanya kazi katika mgodi huo, aliitwa kwenye ofisi za Uhamiaji wilayani Kahama na kutakiwa kujieleza kuhusu uraia wake.

“Niliitwa Ofisi ya Uhamiaji Kahama wakaanza kunihoji wakisema mimi ni Mnyarwanda. Tulikuwa watatu, nilikuwa na Wajaluo wawili kutoka Musoma, mmoja alikuwa Mkenya, huyo alirudishwa kwao nami nikaambiwa lazima wanirudishe kwetu Rwanda,” anasema Nanyungu.

Kwa mujibu wa maelezo yake, ni mzaliwa wa Ngara na wazazi wake wote ni wazaliwa wa wilaya hiyo na hana ndugu hata mmoja Rwanda.

“Nilivyojieleza, walisema kesho yake nirudi ofisini kwao nikiwa na wazazi wangu. Nilienda na baba yangu mdogo aliyepo Kahama, tukatoa maelezo halafu baadaye wakaniachia niendelee na kazi zangu,” anasema Nanyungu.

Hata hivyo, anasema uhakiki unaoendelea wa kukamata magari yote yanayokwenda Ngara na kuwashusha abiria wanaohisiwa kutokuwa raia wa Tanzania unatakiwa kuboreshwa.

“Unakuta mtu anakuja Ngara kwa mara ya kwanza kuja kutembelea ndugu zake akitokea mikoa mingine, lakini maofisa hao wanamshikilia.

“Muda mwingine zoezi hili huleta usumbufu mkubwa kwa mtu kama huyo kwani asipopata wa kuja kumtetea wanaweza kumuweka mahabusu kwamba si raia wa Tanzania,” anasema Nanyungu.

Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Luteni Michael Mntenjele, amesema hakuna kasoro katika uhakiki huo kwa kuwa mtu akihojiwa na kuonyesha vielelezo vyake huachiwa bila usumbufu wowote.

“Watu wengine wanataka kukwamisha zoezi hili kwa sababu ya masilahi binafsi, kwa sababu wana vyeo, sisi hatutakubali. Tukikutilia shaka tutakukamata na tutakuhoji, ukionyesha ushirikiano hatuna shida na wewe,” anasema Mntenjele.

Anasema mpaka sasa wapo Wanyarwanda na Warundi wanaoishi Mwanza na Dar es Salaam, na kwamba wanapokamatwa kuhojiwa hudai kuwa ni watu wa Ngara.

Amesisitiza kuwa suala la kukagua nyaraka zao ni muhimu kwa ajili ya usalama wa nchi.

Kwa upande wake, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji Mkoa wa Kagera, Buteng’e Buteng’e, amesema uhakiki huo ni hatua ya kawaida na unatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji, Sura ya 54 ya mwaka 2014.

“Ni jukumu la kawaida la Uhamiaji kufanya ukaguzi kwa mtu yeyote tunayemtilia shaka juu ya uraia wake,” anasema Buteng’e.

Anasema ili kuepuka usumbufu, wananchi wote wa Wilaya ya Ngara na maeneo yaliyopakana na nchi jirani wanapaswa kutembea na vitambulisho vyao.

“Nyinyi vyombo vya habari mtusaidie kuwaeleza wananchi wote wanaotembelea maeneo ambayo yapo mipakani mwa Tanzania kutembea wakiwa na vitambulisho vyao. Mkifanya hivyo mtakuwa mmetupunguzia lawama kama hizi ambazo zimeanza kujitokeza,” anaeleza Buteng’e.

By Jamhuri