Hofu vyombo vya habari mitandaoni yatanda kuelekea Uchaguzi Mkuu

Wadau wa vyombo vya habari wameonyesha wasiwasi wao juu ya wingi wa vyombo vya habari vya mtandaoni visivyo

na wahariri na kutoa tahadhari iwapo visipodhibitiwa vinaweza kusababisha makosa ya kimaadili katika Uchaguzi Mkuu ujayo na pengine kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani.

Wadau hao wanasema kuwa licha ya serikali kuanzisha sheria za usajili wa vyombo hivyo, ambapo kwa upande mmoja hatua hiyo inaisaidia serikali kupata mapato, lakini pia wameishauri kuangalia suala zima la maadili ya uandishi wa habari ili kuepuka makosa yanayoweza kusababisha taharuki katika jamii.

Katika warsha ya kuwajengea uwezo wadau wa vyombo vya habari juu ya nafasi yao katika kusimamia amani, umoja na

maendeleo ya wananchi kulijadiliwa pia suala la maadili, uzalendo na utaifa kama nyenzo za uandishi wa habari kabla, wakati na baada ya uchaguzi ili kulinda amani na umoja wa kitaifa.

Akizungumzia mada hiyo, mwandishi wa habari mkongwe, Kulwa Mayombi, alisema kuwa maadili na weledi ndiyo misingi ambayo ikizingatiwa itaviwezesha vyombo vya habari kuimarika katika kuchakata habari na kusaidia uchaguzi kuwa wa amani na salama.

Akiwasilisha mada nyingine juu ya ‘Dhima ya vyombo vya habari katika kudumisha amani na umoja wa taifa letu kabla, wakati na baada ya uchaguzi’, mwandishi mwingine mkongwe, Novatus Makunga, anasema kuwa ni jambo lililo wazi kuwa vyombo vya habari mtandaoni vitatumika kwa kiasi kikubwa wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao na kuna hofu kuwa wananchi watalishwa habari nyingi za kupotosha.

Makunga anasema kutokana na changamoto, waandishi wa habari wanalazimika kuhakikisha kuwa wagombea wote wanapata haki sawa bila kuangalia wingi wa wafuasi wao, kwa kuwa kinachoangaliwa ni sera na si idadi ya wafuasi.

Hata hivyo, washiriki hao walisema moja ya sababu ya waandishi kwenda kinyume cha maadili ya uandishi wa habari

ni kutokana na waandishi wengi kukosa nyenzo za utendaji kazi na badala yake kutegemea ufadhili kutoka kwa wanasiasa hivyo kulazimika kuandika habari ya kumfurahisha mhusika.

“Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao tunaomba vyombo vyetu vya habari vitusaidie tuweze kujitegemea kwa vitendea kazi na nyenzo nyingine ili kuepuka kuandika habari zinazokwenda kinyume cha maadili ya uandishi wa habari.

Tumeshuhudia wenzetu wakidhalilika kutokana na kuwategemea wanasiasa,” anasema mwandishi wa habari, Eliya Mbonea.

Katika kukabiliana na hilo, washiriki wanaitaka serikali kuhakikisha kuwa kila chombo cha habari kinakuwa na bodi

ya wahariri, lengo likiwa ni hakikisha kuwa kila habari inayotoka inazingatia vigezo vyote vya weledi na usahihi.

Aidha, washiriki wa warsha hiyo wanaitaka serikali kuwabana wamiliki wa vyombo vya habari kuwawezesha waandishi wao ili kuepuka kununuliwa na wanasiasa.