Moja ya kauli za Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, baada ya Mahakama ya Juu nchini humo kutengua ushindi wake wa awali Agosti mwaka jana, aliwahimiza Wakenya kuwa wamoja.

Rais Kenyatta akasema raia wa taifa hilo lililokabiliwa na machafuko ya baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007 uliosababisha mauaji ya wenyewe kwa wenyewe, ni majirani watakaoendelea kuwa majirani nje ya tofauti za kisiasa.  

Akawahimiza Wakenya (baada ya uamuzi wa Mahakama) washikane mikono na kupeana salamu za amani na ujirani mwema, na kwamba yeye (Kenyatta) alitofautiana na uamuzi huo ingawa hakuukubali.

Hivi sasa Watanzania wanashiriki kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Siha mkoani Kilimanjaro, na Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Ni uchaguzi mdogo wa kwanza wa ubunge kwa vyama hivyo vyenye ushindani mkubwa kushiriki, baada ya ule wa majimbo ya Longido, Songea Mjini na Singida Kaskazini uliosusiwa na Upinzani.

Pia ni uchaguzi unaofuatia ule wa madiwani katika kata 43 ukishirikisha vyama hivyo, lakini ukigubikwa na matukio yasiyostahili dhidi ya misingi ya demokrasia, amani na haki za raia.

Kampeni za uchaguzi huo zimeshazinduliwa mwishoni mwa wiki iliyopita, dalili za awali zikionesha kuwapo ushindani mkubwa.

Sisi wa JAMHURI tunajua wazi kwamba washiriki wa uchaguzi huo ni Watanzania. Wagombea wote ni Watanzania wanaoitafuta nafasi hiyo kuwawakilisha Watanzania wenzao.

Hivyo, hakuna sababu inayoweza kupata nguvu yenye kuungwa mkono, kuruhusu kuwapo vitendo vya hujuma vinavyoweza kuzua mifarakano na machafuko kama ilivyowahi kutokea kwenye mataifa mengine ikiwamo Kenya, mwaka 2007.

Tunazisihi pande zote zinazohusika katika mchakato wa uchaguzi huo, kuanzia wagombea, vyama vya siasa, majeshi ya ulinzi na usalama, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wananchi, asiwepo mwenye hisia za kuwa sababu ya mifarakano kwa watu, kwa sababu tu ya uchaguzi huo.

Ijulikane kwamba uchaguzi huo unarudiwa baada ya waliokuwa wabunge wake, Maulid Mtulia na Dk Godwin Mollel kuondoka upinzani na kujiunga Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mtulia alitoka Chama cha Wananchi (CUF) wakati Dk Mollel alikuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kabla ya kujiunga CCM.

Kuondoka kwao kutoka upinzani na kujiunga CCM kuliashiria jambo moja kubwa, kwamba ukiacha tofauti za kisiasa, wao (Mtulia na Dk Mollel) wanabaki kuwa Watanzania kama walivyo Watanzania wengine.

Watanzania wasidanganyike, siasa na uchaguzi visiwe sababu ya kufarakana na ikibidi kupigana wenyewe kwa wenyewe.

Wanaochaguliwa ni raia wa Tanzania wanaoomba kuwawakilisha Watanzania wenzao. Haki ‘isimame’ wakati wote wa kampeni ili atakayechaguliwa, ndiye anayestahili kutangazwa mshindi. Tutasonga mbele.

By Jamhuri