Na Alex Kazenga

MVOMERO

Wakati matokeo ya darasa la saba kwa mwaka jana nchini yakionesha ufaulu kuongezeka kwa asilimia 72.76 ikilinganishwa na 70.36 ya mwaka 2016, kubainika kwa waliofaulu bila kujua kusoma wala kuandika.

Uwepo wa hali hiyo, ya watoto kufaulu bila kujua kusoma wala kuandika umebainika hivi karibuni kupitia uchunguzi uliofanywa na JAMHURI katika Kijiji cha Kambala Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

Shule ya Msingi Kambala ni kielelezo cha shule zinazolalamikiwa na wananchi kufaulisha wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika.

Katika matokeo ya darasa la saba ya mwaka jana, Shule hiyo ya Msingi Kambala ilishika nafasi ya 32 kati ya shule 68 zilizopo kwenye Wilaya ya Mvomero na 328 kati ya shule 490 za mkoani Morogoro ‘ikiambulia’ nafasi ya 4,796 kitaifa, kati ya shule 9,736.

Katika mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka jana, shule hiyo ilikuwa na watahiniwa 51 ambapo 37 walifaulu, miongoni mwao wakiwamo wasiojua kusoma na kuandika.

Lucia Jacob (14) si jina lake halisi ni mmoja wa wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka jana shuleni hapo na kufaulu mtihani wakati hajui kusoma wala kuandika.

JAMHURI lilikutana na mtoto huyu na kujiridhisha pasipo shaka kwamba hajui kuandika na kusoma. Hata alipotakiwa kuandika majina yake ama kusoma mahali palipoandikwa jina la kijiji anapoishi na wazazi wake (Kambala), alishindwa.

Taarifa kutoka vyanzo tofauti zinaeleza kuwa tatizo hilo halipo kwa Lucia pekee, bali wanafunzi wengi hasa wasichana wanahitimu elimu ya msingi pasipo kujua kusoma ama kuandika.

Kwa mujibu wa utafiti wa kihabari uliofanyika kijijini hapo, wapo wanafunzi wa kike wanaoelekezwa na wazazi wao kuionesha jamii kwamba hawajui kusoma na kuandika ili ‘kufungua’ fursa ya kuolewa.

Sangaine Kanduru ni baba mzazi wa wa Lucia, anathibitisha kwamba tangu alipojiunga shuleni hapo, mwanae huyo hakuwa na maendeleo mazuri ya kitaaluma.

Shule ya Kambala haina walimu wa kufundisha watoto wetu, mimi nashangaa imewezekanaje mwanangu kufaulu kwenda sekondari wakati hajui kusoma wala kuandika,” amesema Sangaine.

Alipohojiwa kuhusu mbinu za wazazi kuwaozesha watoto wa kike kwa visingizio vya kutojua kusoma wala kuandika, amesema hata kama zipo lakini si kwa mtoto wake huyo.

Emmanuel Ibrahim ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kambala, anathibitisha kuwapo wanafunzi wanaofaulu mtihani wa darasa la saba pasipo kujua kusoma wala kuandika, hali anayoilezea kwamba inaustaajibisha umma hususani kijijini hapo.

Watu wengi wanailalamikia mitihani inayotungwa siku hizi, kwamba inakuwa na majibu, na anachotakiwa kufanya mtoto ni kufuta mahali penye jibu sahihi…huoni hilo kama ni tatizo?” alihoji Emmanuel.

Amesema suala la watoto kufaulu bila kujua kusoma wala kuandika linaweza kuchangiwa na ukosefu wa walimu shuleni hapo.

Pia amesema utoro wa wanafunzi uliokithiri ni miongoni wa vyanzo vya wanafunzi kuhitimu elimu ya msingi na pengine wakiwa hawajui kusoma ama kuandika.

Shule ya Msingi Kambala kwa mwaka jana ilikuwa na jumla ya wanafunzi 465 na walimu watatu tu wanaofundisha shuleni hapo.

Shule ya hiyo inakabiliwa na uhaba wa walimu tangu mwaka juzi, baada ya mwalimu mmoja kwenda masomoni na mwingine kustaafu baada ya muda wake wa kufanya kazi kuisha.

Mbelwa Joseph ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Kambala, yeye amesema wanajitahidi kadiri iwezekanavyo kuhakikisha watoto wanajua kusoma na kuandika, lakini wanakwamishwa na mahudhurio mabaya yanayochangiwa na wanafunzi wengi kujihusisha na uchungaji wa ng’ombe.

Tuliwapima watoto wote waliofanya mtihani wa darasa la saba shuleni hapo…suala la mtoto huyo kufaulu bila kujua kusoma wala kuandika haliwezekani,” amesema Mbelwa.

Hata hivyo, mwalimu huyo anakubali kuwapo changamoto ya watoto kutoyamudu vyema masomo ya darasani, hivyo wameanzisha utaratibu wa kuwakumbushia wanafunzi kuanzia darasa la nne hadi la saba masomo ya kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).

Kwa mujibu wa tafiti za taasisi ya Hakielimu kwa mwaka 2012, jumla ya wanafunzi 5,200 walibainika kufaulu kujiunga kidato cha kwanza bila kujua kusoma wala kuandika.

Idadi hiyo iligundulika baada ya udanganyifu uliokuwa umejitokeza katika mtihani wa darasa la saba na kusababisha watoto 9,736 kufutiwa matokeo.

Kutokana na hali hiyo, Wizara ya Elimu Mafunzo na Ufundi waliamuru wanafunzi wote wanaoripoti shuleni kwa kipindi hicho kupewa mtihani wa majaribio wa kupima uwezo wao wa kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).

Kwa upande wa ripoti ya taasisi ya Uwezo ya mwaka 2015, asilimia 16 ya watoto wa darasa la saba mwaka 2014 walihitimu bila kuwa na uwezo wa kusoma mafunzo ya hadithi rahisi ya Kiswahili ya darasa la pili.

Ripoti hiyo ilionesha asilimia 23 ya wanafunzi waliohitimu darasa la saba hawakuwa na uwezo wa kufanya hesabu rahisi za kiwango cha darasa la pili.

Mwalimu Naghuliwa Elisante ni Mratibu Elimu Kata ya Mkindo, amesema si rahisi kuwapo mwanafunzi anayehitimu darasa la saba pasipo kujua kusoma ama kuandika hasa katika shule zilizopo katani humo.

Amesema hali hiyo ni kutokana na wanafunzi wanapofika darasa la sita hawaingii darasa la saba pasipo kujua kusoma wala kuandika.

Elisante amesema muundo wa mitihani inayotungwa kwa kumuelekeza mwanafunzi kuchagua jibu sahihi, unaweza kuchangia wanafunzi wengi kufaulu pasipo kujua kusoma ama kuandika.

Mwakilishi wa Ofisi ya Afisa Elimu wilayani Mvomero, Mwalimu Nimrodi Mahenge, amesema “sina uhakika kama kuna watoto hao, kwani kabla ya kufanya mtihani wa darasa la saba wanafanyiwa majaribio.

Pia ameongeza kuwa mwanafunzi ambaye hawezi kusoma na kuandika hana uwezo wa kujaza fomu ya kujaza namba za mtihani inayojazwa kabla ya mwanafunzi kufanya mtihani wa darasa la saba.

 Kuokoa jahazi

 Mahenge amesema suala la watoto kutokujua kusoma wala kuandika katika Wilaya ya Mvomero ni changamoto ambayo wameamua kuishughulikia kwa nguvu zote.

 Amesema utafiti wao wa awali ulibainisha ili kuweza kuepukana na changamoto hiyo, wanatakiwa kuihusisha jamii nzima ya Mvomero hasa wafugaji ambao hawana mwamko wa elimu.

Mahenge amesema mradi wa ‘Tusome Pamoja’ ambao umetambulishwa mkoani Morogoro, utafanya vyema kwani umepunguza tatizo hilo mkoani  Shinyanga.

Shinyanga ni moja ya mikoa yenye historia ya kuwa na wanafunzi wasiojua kusoma wala kuandika.

Tusome Pamoja unadhaminiwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID) ukiwa na lengo la kuwawezesha kutumia mbinu bora katika utoaji wa elimu kwa shule za msingi zilizo katika maeneo yasiyo na mwamko wa elimu.

Kwa mujibu wa mujibu wa Mahenge, moja ya matokeo ya mradi huo ni kuundwa kwa Ushirikiano wa Wazazi na Walimu (Uwawa) unaoshughulikia uboresha mazingira katika sekta ya elimu ili yamuwezeshe mwanafunzi kufaulu.

Amesema ushirikiano huo ambao unalenga kubaini changamoto za mtoto mmoja mmoja kutoka kila familia, utamwezesha mwalimu kutambua maeneo sahihi ya kumsaidia darasani.

Mahenge amesema katika kuboresha mazingira hayo, wanafunzi wa madarasa ya tano, sita na saba wanalazimika kufundisha kusoma na kuandika kwa kila somo wanalofundisha.

Kutokana na watoto wengi kuonekana wanasumbuliwa na suala la KKK (Kuhesabu, Kusoma na Kuandika), tumepitisha utaratibu wa kufundisha masomo haya hadi kwa madarasa ya juu kwa kumtaka mwalimu ayagusie anapokuwa anafundisha masomo mengine kwa madarasa ya tano, sita na saba,” amesema Mahenge.

Mdau wa masuala ya elimu kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) (jina linahifadhiwa) amesema, kukosekana kwa ‘sauti ya pamoja’ kama taifa kuhusu elimu ya msingi ni chanzo cha matatizo yanayoikabili sekta hiyo.

Amesema Serikali ina sera ya kutokaririsha mtoto darasa, hivyo kinachofanyika ni kupitisha watoto wa shule za msingi kujiunga sekondari hata kama hawana sifa.

John Nchimbi, Msemaji wa Baraza la Mitihani (NECTA), amesema mtihani wa kuchagua jibu sahihi hauchangii watoto kufaulu bila kujua kusoma wala kuandika, bali sababu nyingine zinazopaswa kujulikana kwa kufanya utafiti.

Amesema karibu nchi zote za Afrika Magharibi zinatumia mtihani wa kuchagua katika mitihani yao, Ghana ikiwa kinara – iliyoanza kutumia mfumo huo tangu miaka 1960 na hawajapata madhara yoyote.

Ameongeza kuwa lengo la kuanzisha mfumo huo ni kupata njia bora ya kutahini wanafunzi na si vinginevyo.

Hali kama ilivyojionesha kwa Shule ya Msingi Kambala inaelezwa kuwapo kwa shule nyingine wilayani Mvomero, Mkoa wa Morogoro na pengine katika maeneo mengine ya nchi.

Hivyo, ni wajibu wa Serikali na wadau wengine kuhakikisha watoto wanapata elimu iliyo bora ili wanapohitimu wawe na uwezo ukiwamo wa kujua kusoma na kuandika.

Please follow and like us:
Pin Share