Home Michezo Huku Simba, kule Chalenji, tutampata mkali wetu?

Huku Simba, kule Chalenji, tutampata mkali wetu?

by Jamhuri

NA CHARLES MATESO

Bilionea wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ bado ana kazi kubwa pamoja na ‘sifa’ nyingi za kuwekeza katika uwanja wa Simba Complex, uliopo Bunju, Dar es Salaam.

Utazalisha nini? Hilo ndilo swali la msingi la kujiuliza. Una vigezo vyote au mbwembe tu za Watanzania? Nalo pia unatakiwa kujiuliza. Maswali ni mengi, majibu ni machache.

Achana na habari za uwanja wa Simba, lakini pia kuna michuano ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati ambayo imeanza Uganda. Tutavuna nini?

Unaweza kuwaza juu ya kuvuna kwa kutwaa taji, lakini ‘wenye akili’ tunafikiria kizazi kinachojengwa sasa cha soka kitaleta kitu kinachohitajika huko mbeleni?

Turudi nyuma

Umekuwepo uzoefu wa miradi mikubwa ya soka kuishia njiani. Inaanzishwa kwa mbwembwe nyingi, kila mtu anajawa hamasa ya kuona mafanikio halafu taratibu kilichoanzishwa kinafia njiani.

Labda tatizo ni kushindwa kwetu katika kuendana na mahitaji mengi, hasa yenye kujumuisha upatikanaji wa fedha na hata masuala ya uwezo wa kielimu wa kuiendesha miradi ya soka ni tatizo pia.

Miaka ya nyuma tumekuwa tukiishia njiani, naamini TFF na wadau kwa ujumla hawatapenda kuziona hizi juhudi za kulea wachezaji wa baadaye kama ilivyo kwa Alliance zikiishia njiani bila ya kuzalisha mamia kama si maelfu ya wanasoka bora. Nadhani TFF wamejipanga kukabiliana na changamoto nyingi zitakazoibuka.

Huu ni wakati mwafaka kwa TFF kuonyesha utofauti wake na taasisi nyingi za soka ambazo zimeshindwa kuleta kitu kipya. Ni wakati sahihi kwa TFF kujenga hoja kwa Serikali Kuu, juu ya nini hasa wanakifanya, kwa kuwatunza na kuwalea watoto ili waje kuwa wachezaji wa Taifa Stars ya ushindi na si ile ya wasindikizaji.

Ndani ya mpango wa muda mrefu wa kulipandisha hadhi soka la Tanzania, pia wapo watu wenye kujifikiria wao zaidi ya lengo la taasisi. Watu wa aina hiyo fedha kwao ni halali zikiwa zinamilikiwa na wao tu, hawa ndio wanaoitia laana dunia hii mpaka inaandamwa na majanga kila mwaka.

Zinapotengwa Sh milioni 300 kwa ajili ya maendeleo ya soka, wao huzitumia Sh milioni 100 tu, zinazobaki zinatumika katika ujenzi wa majumba ya kifahari kando ya bahari, pamoja na kufanyia starehe wakiwa na marafiki zao wa karibu. Yale yale ya FIFA yanaweza kufanyika kwenye soka letu.

Bahati mbaya mambo ya aina hiyo hukwamisha lengo la uanzishaji wa miradi ya soka. Kuanzia sasa ni bora TFF ikaitanguliza shule ya Alliance kwenye kila mkutano wenye kuhusiana na upatikanaji wa fedha kwa njia mbalimbali halali.

Uwepo wa taasisi ya Alliance yenye kushughulika na maendeleo ya wachezaji wa baadaye wa timu za vijana za taifa na ile ya wakubwa, ni kama vile familia inavyofurahia kuzaliwa kwa mtoto huku wazazi wakijiandaa kufanya kazi mara mbili zaidi ili malaika asiteseke tangu siku yake ya kwanza duniani.

Kuna suala la usimamiaji wa nidhamu binafsi za watoto, ili lipewe kipaumbele kikubwa zaidi, ili wachezaji wa baadaye wasiwe na zile tabia za utovu wa nidhamu. Wengi wa wachezaji wetu hushindwa kwenye majaribio kila mara, kwa sababu ya kupitia malezi ambayo yanawapa uhuru mwingi.

Ule ununda unaoanza kujengeka tangu utotoni, lazima utakuja kuyaharibu maisha ya mwanasoka. Wakati mwingine hata hawa watoto wenye umri chini ya miaka 13, huanzisha tabia za kijinga, kama vile kuanza kumlaumu na kumtukana mwamuzi, pamoja na ule uchezaji uliojaa uhuni wa mitaani. Walimu wenye uzoefu katika malezi ya watoto wanatakiwa kuajiriwa mapema ili waanze kazi sambamba na mradi mzima wa U13.

TFF ianze kazi ya kutafuta mawasiliano na klabu za mataifa makubwa kisoka, ili uwepo wa mradi wa Alliance uweze kuanza kujulikana. Kuna vipaji vyenye ubora wa kipekee, siku zote hutakiwa kujulikana mapema ili vianze kuandaliwa kitaalamu zaidi.

Lionel Messi alicheza na watoto wenzake wa Argentina, lakini wenye kuujua mpira walishauona uwezo wake, hivyo matajiri wakawa tayari kuyalipia matibabu yake kwa gharama yoyote ile.

Messi wa Tanzania anaweza kuwepo kati ya watoto watakaopata bahati ya kupita kwenye mchujo wa mwisho wa mwaka huu au ule wa miaka ijayo, asicheleweshwe.

Ni kazi ya TFF kuhakikisha anapata timu nje ya nchi mapema iwezekanavyo. Ukiritimba wowote utakaojitokeza katika kumpeleka nje ya Afrika, utakuwa unakwamisha jitihada zote za mradi wa kuweza kukua na kufaidika kiuchumi na Tanzania itajichelewesha yenyewe kisoka.

Nazungumzia mradi huu wa Alliance, ambao ulianzishwa vizuri na naamini hauwezi kufa kama ilivyokufa mingine, ujengwe muundo wa uongozi ambao utagawa majukumu ya kazi kadiri ya taaluma za watu. Uchukuliaji wetu wa mambo kienyejienyeji, umechangia katika kuua miradi mingi ambayo kwa kweli ingeweza kuleta kitu kipya chenye maendeleo kwenye soka.

TFF ijipange katika utafutaji wa fedha za mradi huu, lakini anayeombwa fedha lazima aone umakini wa yule anayeziomba kwenye usimamiaji wa  shughuli za kila siku akiwa kama mmiliki wa mradi.

Wale watoto ambao leo hii wanaonekana wakipambana uwanjani, miili yao bado ni dhaifu lakini watakapokuja kuvaa jezi ya Taifa Stars huku wakiwa wamepitia katika mradi uliowatunza vizuri, watakuwa na miili yenye afya njema. 

Kuna picha moja maarufu kwenye kurasa za michezo, inamuonyesha Yaya Toure akicheza soka na wenzake utotoni, akiwa miguu peku, mwembamba asiye na afya bora, lakini mtoto yule ndiye mchezaji huyu aliyekuja kutesa vilivyo barani Ulaya.

Alliance Mwanza inakuja na changamoto ya uendeshaji wenye kutegemea weledi wa hali ya juu, ili iweze kudumu kwa miaka mingi kadiri itakavyowezekana na ili iweze kumuandaa vema Yaya Toure wa Tanzania.

Wanachosema

Mo anaamini kwamba Simba itafikia lengo lake, lakini bado kuna maswali mengi ya kujiuliza hasa kama kweli wanazalisha.

Kuna wachezaji wangapi wanawazalisha kwa mwaka? Hapa ndipo tatizo linapoanzia.

“Tutaifanya Simba iwe moja kati ya timu kali zaidi na naamini katika hilo,” anasema Mo.

Mwenyekiti wa Yanga, Dk. Mshindo Msolla, naye anakiri Yanga kwa sasa lazima ijipange ili kutimiza malengo yake, kinyume cha hapo itakuwa balaa.

“Tunatakiwa tutoke hapa tulipo na ninaamini tutafanikiwa katika hilo.”

Rais wa TFF, Wallace Karia, anakiri soka la vijana lazima lipewe kipaumbele, lakini kutoka hapo ni lazima kuwe na ushirikiano wa kutosha.

“Lazima tutoke hapa tulipo, kuna kazi kubwa lakini ninaamini tutatoka.”

Ngoja tuone! 

You may also like