Idadi ya watu waliokufa katika tetemeko kubwa la ardhi nchini Japan imeongezeka na kufikia 73 mapema hii leo wakati shughuli ya kuwatafuta manusura ikiendelea.

Japan inaendelea kuwatafuta watu waliokwama chini ya vifusi baada ya tetemeko la ardhi
Mtu akitembea mbele ya jengo lililoanguka katika mji wa Anamizu, Ishikawa baada ya tetemeko la ardhi, Januari 3, 2024.

Vifo vyote vimeripotiwa kutokea katika eneo la Ishikawa lililoathirika zaidi na tetemeko hilo la ukubwa wa 7.6. Zaidi ya watu 33,000 wamehamishwa kutoka kwenye makazi yao na karibu nyumba 10,000 hazina huduma za maji hii ikiwa ni kulingana na serikali ya eneo hilo.

Maelfu ya wanajeshi wa uokozi wanakimbizana na muda ili kujaribu kuwaokoa watu wengi waliokwama chini ya vifusi katikati ya baridi kali na mvua kubwa, huku pia wakikabiliwa na changamoto za barabara mbaya na ugumu wa kuyafikia baadhi ya maeneo.

Bado haijulikani athari kamili ya tetemeko hilo zikiwa zimepita siku tatu tangu tetemeko hilo ambalo ni kubwa zaidi kutokea nchini humo tangu mwaka 2016.

By Jamhuri