Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia

Idadi ya watu wazima wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu nchini imepungua kutoka asilimia 80 ya mwaka 1961 hadi kufikia asilimia 77 .

Hali hii imesababisha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuanzisha program mbalimbali kuwawezesha kundi hilo kupata maarifa.

Hayo yamebainishwa na mratibu wa kongamano la kitaifa la maadhimisho ya Juma la Elimu kwa Watu Wazima, Dkt. Sempeo Siafu linalofanyika mkoani Pwani.

Amesema kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Kimataifa ya Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO idadi ya watu wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu imepungua tangu nchi ya Tanzania ipate uhuru kutokana na hali hiyo Wizara ya Elimu ilianzisha program maalum kwa ajili ya kuwasaidia watu wazima na vijana waliokatisha masomo.

“Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alianzisha kampeni mbalimbali zinazohamasisha wananchi kujua kusoma na kuandika na ukiangalia tulikotoka na sasa tumerudi nyuma, natoa rai kuweka mikakati ya pamoja ili kuondoa changamoto hii nchini, taifa ya watu walioelimika ni rahisi kuleta maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesema Dkt. Siafu.

Ameeleza kuwa program ya elimu ya awali itaendelea kufanya vizuri endapo watu wazima watajua kusoma na kuandika kwa ajili ya ushirikiano baina yao na walimu katika kufuatilia maendeleo ya watoto shuleni.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Msingi, Josephat Luoga amesema Serikali imekuwa ikitekeleza program mbalimbali za elimu ya watu wazima ili kuongeza idadi ya watu wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu.

Amezitaja program hizo kuwa ni Mpango wa Elimu Msingi kwa walioikosa MEMKWA, Mpango wa Elimu sekondari kwa njia mbadala, Mpango wa Elimu changamani walio nje ya shule, uzalishaji mali, shughuli za ugani na vikundi vya kuweka na kukopa VICOBA.

Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Watu Wazima, Elimu Maalum na Michezo kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Ernest Hinju, amesema wanao mtandao wa kutosha kuhakikisha kila mtu mzima mwenye lengo la kusoma atapata elimu hiyo katika eneo lake.

Afisa Elimu Mkoa wa Pwani, Sara Mlaki amesema mkoa huo unatekeleza programu mbalimbali kwa halmashauri zote kama vile Mpango wa Elimu ya Msingi kwa waliokosa MEMKWA jumla ya wanafunzi 1943 wakiwemo wavulana 1117 na wasichana 826 wamenufaika.

Ameongeza kuwa mkoa huo, unatekeleza program ya Mpango wa Uwiano kati ya Elimu ya watu wazima na Jamii MUKAJE yenye jumla ya wanafunzi 2080 ikitajwa kuwa program nzuri ya elimu nje ya mfumo rasmi kwani wanajifunza na shughuli za uzalishaji mali kama vile mapishi, ushonaji, mapambo, ufumaji, ususi na usindikaji.

Baadhi ya wanufaika wa programu ya Elimu ya watu wazima akiwemo Siri Kibinde amesema kwa sasa amejua kusoma na kufanya shughuli za ujasiriamali kama vile ushonaji, mapambo, ususi na usindikaji.

By Jamhuri