ISHI NDOTO YAKO (2)

Katika sehemu ya kwanza ya makala hii tuliona kuwa mtu unapaswa kuishi kwa kufuata ndoto yako. Ndoto  yako isiongozwe  na maneno  ya watu.  Acha  wakuseme  wawezavyo  lakini  wewe  pambana  kutimiza  ndoto  yako.  Acha  leo  wakuone  kichaa  ili  kesho  wakushangae. Endelea…

Ishi  kabla  ya  kufa. Kuna  watu  wanakufa  kabla  ya kuishi. Kivipi watu wanakufa  kabla ya kuishi? Ninakujibu nisikilize kwa umakini. Mtu yeyote aliyekata tamaa ya maisha ni kama amekufa ingawa bado anavuta hewa katika sayari  hii  ya  dunia.  

Kila  mara  tunapoacha kufanyia kazi ndoto zetu tulizonazo au tunapoamua kuacha kutumia vipaji ni kama tunaanza kufa. Tunapoacha kutenda matendo yenye kuleta ustawi kwetu na kwa wenzetu, tunaanza kufa. Tunapolalamika kwa kila jambo ni kama tunaanza kufa. Unaposoma makala ya kitabu hiki fufuka. Fufua ndoto zako upya.

Ota ndoto kubwa katika maisha yako. 

Ota kufanya mambo makubwa na mazuri katika dunia hii. Mwanahabari Ruge Mutahaba anasema: “Sipendi ndoto  ndogo.  Napenda  ndoto  kubwa.  Ukiwa  na  ndoto  ndogo  huwezi  kuifikia  ndoto  kubwa.” 

Penda ndoto kubwa. Ndoto yako haitakufa mpaka utakapokufa wewe.  Ndoto kubwa inaacha alama duniani.  Mfanyabiashara wa Nigeria, Aliko Dangote anasema: “Baada ya kifo changu, ninataka nikumbukwe kama mmiliki  mkubwa sana wa  viwanda  Afrika.”  Hii  ni  ndoto  inayoishi  milele.

Mwandishi Wayner Dyer katika kitabu chake cha The Power of Intention  anasema: “Nia yetu inaumba uhalisia wetu.” Nia njema ni roho ya mafanikio. Aliye na nia ya dhati ya kufanikiwa na anajua kuwa ana nia ya kufanikiwa ‘Atafanikiwa’. Siku  moja  bondia  Floyd Mayweather alionekana akifanya mazoezi saa 11 alfajiri na mwandishi wa habari alimuuliza: “Ni jambo gani linakufanya uzidi kufanikiwa?” Mayweather alimjibu: “Wakati wenzangu wamelala mimi ninafanya  mazoezi, wakiamka mimi ninafanya mazoezi, wakirudi kulala mimi ninafanya  mazoezi.”  

Hii  ndiyo siri ya mafanikio ya bondia  Floyd Mayweather. Hata wewe leo unaweza ukaitumia kanuni yamafanikio ya bondia Mayweather na ukafanikiwa. Mwandishi wa kitabu cha I Can, I Must, I Will, Dk. Reginald Mengi anasema: “Nimekulia kwenye umaskini, lakini siku zote nimekuwa  nikiona umaskini kama changamoto. Habari njema ni kwamba unaweza  kuushinda umaskini kama  uko tayari  kulipa gharama. Gharama hiyo ni kufanya kazi kwa bidii.” 

Mwanasayansi wa Ufaransa, Louis Pasteur, alipoambiwa na marafiki zake kuwa anafanya kazi kupita kiasi alisema: “Nahisi  kama ninaiba kama nikiruhusu siku ipite bila kufanya kazi.”

Tumeumbwa  kufanikiwa. Tumeumbwa  kushinda. Tazama huu ushuhuda wa John Paul DeJoria. John Paul DeJoria   akiwa  katika shule ya sekondari ya juu (kidato cha tano na sita) mwalimu wake alimwambia: “Wewe John hauwezi kufika popote kwa  sababu  hauna akili za kimasomo.” 

DeJeforia hakukatishwa tamaa na maneno ya mwalimu wake. Aliendelea kuhangaika kutafuta maisha yake. DeJeforia  alioa, lakini kuna wakati maisha yalimwendea kombo. Akayumba sana kiuchumi. Mke wake alipoona maisha yamekuwa magumu alimkimbia na kumwachia mtoto mmoja wa miaka miwili. 

DeJeforia alianza kuokota chupa tupu zilizotumika na kuziuza ili amtunze mwanae. Siku zote alimwambia mwanae: “Tutatoka kimaisha pamoja.” 

DeJeforia alianza pia kufanya biashara ya kuuza magazeti mlango mmoja baada ya mwingine. Ilifika hatua akaamua  kuanzisha  kampuni. Watu walimbeza na wakamwambia kwamba hana elimu yoyote ya biashara na hana pesa za kutosha za kuendesha biashara. DeJeforia aliendelea kukomaa. 

Mwaka 2015, jarida maarufu la Forbes lilimtaja kama tajiri namba 234 kati ya matajiri 400 kutoka Marekani akiwa  na  utajiri wa dola bilioni 2.8 za Marekani. Dejeforia pia ni mwanzilishi wa bidhaa za nywele zinazojulikana kama Paul Mitchel. Usikate tamaa katika maisha. Pambana.