Na Charles Ndagulla, Moshi

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Moshi, Aishiel Sumari, amenyang’anywa
jalada la kesi ya mauaji ya aliyekuwa
mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule
ya Sekondari ya Scolastica, Humphrey
Makundi (16), JAMHURI limebaini.
Hatua hii imekuja siku chache baada ya
JAMHURI kupata taarifa za kiuchunguzi
zenye kuonyesha kuwa Jaji Sumari alikuwa
analalamikiwa, gazeti likachapisha taarifa
hizo. Badala yake, jalada hilo sasa
limekabidhiwa kwa Jaji Huruna Songoro,
ambaye amewahi kuwa Jaji wa Mahakama
Kuu Divisheni ya Biashara.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya
kuwepo taarifa za Jaji Sumari kujipangia

kusikiliza shauri hilo linalowakabili
washtakiwa watatu akiwamo Mkurugenzi wa
Shule hiyo, Edward Shayo, licha ya katazo
la Jaji Kiongozi, Dk. Eliezer Feleshi.
Washtakiwa wengine katika shauri hilo la
jinai Na. 48/2018 ni pamoja na aliyekuwa
mlinzi wa shule hiyo, Hamis Chacha,
ambaye ni mshtakiwa wa kwanza na Laban
Nabiswa aliyekuwa Mwalimu wa Nidhamu
ambaye ni mshtakiwa wa tatu.
Jaji Kiongozi, Feleshi, amemwandikia barua
Jaji Sumari kumtaka asisikilize shauri hilo
kutokana na kuwapo malalamiko ya haki
kutotendeka yaliyotolewa na baba mzazi wa
Humphrey, Jackson Makundi.
Kutokana na malalamiko hayo, Jaji Feleshi
alimtaka Jaji Sumari amjulishe kesi hiyo
itakapofikia hatua ya kusikilizwa ateue jaji
wa kuisikiliza, lakini kinyume cha maelekezo
ya Jaji Kiongozi, Jaji Sumari alijipangia
kusikiliza kesi hiyo Agosti 27, mwaka huu,
baadaye Jaji Kiongozi akamnyang’anya
jalada hilo.
Gazeti la JAMHURI limeiona na kuisoma
barua ya Jaji Kiongozi ya Julai 31, mwaka

huu kwenda kwa Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Moshi ikimjulisha
kuhusu kuwepo kwa malalamiko ya haki
kutotendeka kutoka kwa Jackson Makundi,
ambaye ni mzazi wa Humphrey aliyeuawa.
Barua ya Jaji Kiongozi ya Julai 31, mwaka
huu yenye Kumb. Na. HA.59/190/02 “C”/3,
iliandikwa na kusainiwa na D. B. Ndunguru
ambaye ni Katibu wa Jaji Kiongozi na
nakala ya barua hiyo kunakiliwa kwa
Jackson Makundi ambaye ni baba mzazi wa
marehemu Humphrey Makundi.
“Kufuatia malalamiko hayo, mfahamishe
Mhe. Jaji Mfawidhi anifahamishe mara tu
kesi hiyo itakapopevuka kwa ajili ya ‘Plea
Taking’ and PH ili niteue Mheshimiwa Jaji
atakayeisikiliza. Pia toa jibu kwa
mlalamikaji,

” inasema sehemu ya barua

hiyo.
JAMHURI lilipopata ratiba ya usikilizwaji wa
mashauri ya jinai 21 yaliyopangwa
kusikilizwa na jaji huyo, limebaini kuwa
shauri la jinai Na. 48/2018 linalomkabili
Hamis Chacha Wisare na wenzake wawili
Jaji Sumari amejipangia kulisikiliza kinyume

cha maelekezo ya Jaji Kiongozi Feleshi.
Ratiba hiyo ilitolewa na Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Frank
Mahimbali, ambayo inaonyesha shauri hilo
lingesikilizwa Agosti 27, mwaka huu na Jaji
Sumari.

Kesi yaanza kunguruma

Agosti 27, mwaka huu, kesi hiyo ilianza
kunguruma katika Mahakama Kuu Kanda
ya Moshi chini ya Jaji Haruna Songoro
ambapo washtakiwa hao walisomewa
mashtaka na maelezo ya kosa, ambapo
upande wa Jamhuri umepanga kuita
mashahidi 34.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili
Mkuu wa Serikali, Joseph Pande,
akisaidiana na Wakili Mwandamizi wa
Serikali, Abdallah Chavula, uliwasilisha
mahakamani hapo maelezo ya namna
marehemu Humphrey Makundi alivyouawa.
Akisoma maelezo hayo, Pande alieeleza
kuwa Novemba 6, mwaka jana, Humphrey
aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha pili

katika Shule ya Sekondari ya Scolastica
iliyopo katika Mji Mdogo ya Himo, mkoani
Kilimanjaro alitoweka shuleni hapo jioni.
Amesema Novemba 10 mwili wa marehemu
ulidaiwa kupatikana ndani ya Mto Ghona
ambao upo mita 300 kutoka shuleni hapo
na ndipo taarifa ilipotolewa katika Kituo cha
Polisi Himo.
Aliieleza mahakama kuwa mwili huo
uliopolewa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa, Mawenzi, kabla ya kuzikwa
Novemba 11 katika makaburi ya Karanga
kutokana na mwili kuanza kuharibika, pia
kutokuwa umetambuliwa na ndugu.
Wakili wa Serikali alieleza kuwa baada ya
mwili kuzikwa polisi waliendelea na
uchunguzi na Novemba 17, mwaka jana
mwili huo ulifukuliwa baada ya mahakama
kutoa kibali na kwenda kufanyiwa
uchunguzi katika Hospitali ya Rufaa ya
KCMC.
Baada ya tukio hilo polisi waliwakamata
washtakiwa hao na katika maelezo ya
mshtakiwa wa kwanza, Hamis Chacha,
anakiri kumpiga marehemu kwa kutumia

ubapa wa panga alilokuwa nalo siku ya
tukio.
Chacha katika maelezo yake anadai kuwa
siku ya tukio alisikia kishindo cha mtu
akiruka ukuta wa shule na baada ya
kufuatilia aliona mtu akikimbia na kuanza
kukimbizana naye.
Ameeleza kuwa alimfikia mtu huyo na
kumpiga na ubapa wa panga huku
akiendelea kukimbizana naye na baadaye
aliendelea kumshambulia kwa kutumia
panga lake hadi akapoteza fahamu.
Kulingana na maelezo yaliyosomwa
mahakamani hapo, mshtakiwa huyo wa
kwanza anadai baadaye alimjulisha
mshtakiwa wa pili na wa tatu na wakafika
eneo la tukio.
Akaendelea kueleza kuwa, baada
washtakiwa hao kufika, alishauri marehemu
apelekwe hospitalini kwa ajili ya matibabu,
lakini mshtakiwa wa pili ambaye pia ni
mmiliki wa shule hiyo alikataa ushauri huo.
Chacha ameleeza katika maelezo yake
kuwa mshtakiwa huyo wa pili alishauri mwili
huo ukatupwe katika Mto Ghona kwa kile

alichodai italeta shida na washtakiwa hao
wa pili na wa tatu walitii agizo hilo na
kwenda kuutupa mwili huo mtoni.
Washtakiwa hao kupitia mawakili wao,
Eliakunda Kipoko na Gwakisa Sambo
walikana mashtaka huku wakikiri kuwa
majina yao ni sahihi na kwamba ni kweli
wameshtakiwa kwa kosa la mauaji ya
kukusudia.
Kesi hiyo sasa inasubiri kikao kijacho cha
Mahakama Kuu iendelee kusikilizwa huku
upande wa utetezi ukipanga kuwasilisha
orodha ya mashahidi na vielelezo kabla kesi
haijaanza kusikilizwa.
Upande wa mashtaka utawaita mashahidi
34 akiwamo baba mzazi wa Humphrey,
Jackson Makundi, maofisa wa Polisi kutoka
Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya
Jinai Mkoa (RCO) na kutoka Kituo Kikuu
cha Polisi Himo, ambako tukio hilo lilitokea.
Katika orodha ya mashahidi iliyosomwa
mahakamani hapo na Wakili Mkuu wa
Serikali, Joseph Pande, wamo madaktari
wawili kutoka Hospitali ya Rufaa ya KCMC
walioufanyia uchunguzi mwili wa

marehemu, Dk. Alex Mlemi na Dk. Samwel
Mwita na Hadija Saidi Mwema kutoka Ofisi
ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Wamo pia madaktari kutoka Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi,
mhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti
katika hospitali hiyo ya mkoa na mtaalamu
kutoka Kampuni ya simu za kiganjani ya
Vodacom.
Mbali na mashahidi hao 34, upande wa
mashtaka pia umepanga kuwasilisha
vielelezo na nyaraka 15 yakiwamo maelezo
ya kukiri kosa mbele ya Mlinzi wa Amani
yaliyotolewa na mshtakiwa wa kwanza,
Hamis Chacha.
Vielelezo vingine ni pamoja na ripoti ya
uchunguzi wa vinasaba (DNA), ripoti ya
uchunguzi wa kifo cha marehemu na ripoti
ya mawasiliano ya simu ya washtakiwa
ambayo yanaonyesha waliwasiliana siku ya
tukio.
Pia upande wa mashtaka uliieleza
mahakama hiyo kuwa utawasilisha kilelezo
cha panga ambalo linadaiwa kutumiwa na
mshtakiwa wa kwanza, Hamis Chacha,

simu saba na nguo za marehemu alizokuwa
amevaa siku ya tukio.

MWISHO

By Jamhuri